Saturday, October 18, 2014

TANROADS RUVUMA UTATA MTUPU, YANYOSHEWA KIDOLE KWA KUJENGA BARABARA KIWANGO CHA CHINI

Barabara iliyojengwa kilometa moja, kwa kiwango cha lami eneo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, tabaka lake la juu likiwa limebomoka ambapo mwanzo wa barabara hiyo hadi mwisho wake katika maeneo tofauti imebomoka kwa mtindo huu, kwa kile kinachoelezwa kuwa kutokana na kujengwa kwa kutokidhi viwango husika, ambapo barabara hiyo ujenzi wake unafanywa na kampuni ya FEI - MAC LTD kutoka mjini Songea na kusimamiwa na Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani hapa.


Kibao hiki kinaonyesha Mkandari husika aliyefanya kazi ya ujenzi wa barabara hiyo. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, ameshushiwa lawama nzito kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara kiwango cha lami katika eneo la Mbinga mjini mkoani humo, kutokana na barabara ambayo imejengwa na wakala huyo kuanza kubomoka tabaka la juu kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.

Barabara hiyo ambayo ujenzi wake ni wa kilometa moja, inagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja  na kwamba utekelezaji wake upo chini ya usimamizi wa wakala huyo.

Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na wakazi wa mji wa Mbinga walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa barabara hiyo baada ya magari kuruhusiwa kupita, hata kabla haijamaliza miezi miwili tabaka la juu la lami limeanza kubomoka.


“Kwa kweli hatukutarajia kama leo barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami halafu kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali, inabomoka na kinachofuata hapa ni kuwekwa viraka, maana viongozi walituhakikishia barabara yetu itajengwa vizuri na kwa kiwango bora”, walisema.

Ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa fedha zinazotolewa na mfuko wa barabara hapa nchini, ambapo walisema huenda kubomoka kwa barabara hiyo kunatokana na wataalamu husika kutozingatia ipasavyo vipimo vya kimaabara na ndio maana imeanza kubomoka kabla hata haijatumika kwa muda mrefu.

Aidha walieleza kuwa uzembe huo uliofanywa wa kutozingatia viwango husika, ni hasara kubwa kwa serikali kutokana na fedha nyingi zilizotumika ambazo ni kodi za wananchi kujengea barabara hiyo, kutofanya kazi yake kama ilivyokusudiwa.

Kampuni ya FEI – MAC LTD kutoka mjini Songea mkoani Ruvuma, ndiyo imekabidhiwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami  na kwamba ujenzi wake hadi kukamilika umechukua zaidi ya miezi sita.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwaikambo alipoulizwa kwa njia ya simu ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya ujenzi wa barabara hiyo alisema, “hili tatizo ndugu yangu ni dogo sana, ni jambo la kawaida kwa barabara ya lami kufumuka au kubanduka tabaka la juu sina cha nyongeza zaidi ya haya”.

Mtandao huu ulipomtafuta Meneja wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, Abraham Kissimbo ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alisema yeye hana nafasi ya kuweza kuzungumzia kwa kina juu ya ujenzi wa barabara hiyo.

“Siwezi kuzungumzia lolote kwa sasa, hapa nilipo nina kazi nyingi za kufanya siwezi kuacha kazi nilizonazo na kuanza kukupatia wewe maelezo juu ya kwa nini barabara hii imebomoka, lakini ninachoweza kukuambia tutafuatilia suala hili”, alisema Kissimbo.




No comments: