Friday, October 24, 2014

ASKARI WA USALAMA BARABARANI MBINGA ASWEKWA MAHABUSU KWA KUMJERUHI DEREVA WA PIKIPIKI




Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limeingia katika kashfa mpya kufuatia askari wake wa usalama barabarani kumjeruhi mwendesha pikipiki kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kichwani, na kumsababishia jeraha ambalo lilisababisha dereva huyo kutokwa na damu nyingi.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 20 mwaka huu majira ya mchana, eneo la stendi ya magari ya abiria mjini hapa, ambapo askari huyo anayejulikana kwa jina la Msafiri Kilango, ndiye aliyefanya kitendo hicho kwa kumchoma kichwani dereva wa pikipiki aitwaye Erick Shonga.

Kufuatia tukio hilo hali ilibadilika mjini hapa ambapo kundi la waendesha pikipiki liliandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi cha wilaya hiyo, kwa lengo la kupinga kitendo alichofanyiwa mwenzao.

Walipofika kituoni hapo walieleza malalamiko yao wakisema kuwa askari wa usalama barabarani wilayani hapa, wamekuwa na mazoea ya kuwanyanyasa mara kwa mara waendesha pikipiki hivyo wamechoshwa na hali hiyo.

“Sisi tumechoshwa na unyanyasaji huu ambao tunafanyiwa na hawa askari, muda mwingi wakitukamata wanatupiga faini wanachukua hela zetu halafu stakabadhi ya malipo halali hatupewi”, alisema Thito Mhina mmoja kati ya madereva hao wa pikipiki.

Aliyechomwa atoa ushuhuda:

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi dereva wa pikipiki aliyejeruhiwa Erick Shonga alisema, amepatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo ambapo ameshonwa nyuzi tatu kichwani katika eneo ambalo alichomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.

Saturday, October 18, 2014

TANROADS RUVUMA UTATA MTUPU, YANYOSHEWA KIDOLE KWA KUJENGA BARABARA KIWANGO CHA CHINI

Barabara iliyojengwa kilometa moja, kwa kiwango cha lami eneo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, tabaka lake la juu likiwa limebomoka ambapo mwanzo wa barabara hiyo hadi mwisho wake katika maeneo tofauti imebomoka kwa mtindo huu, kwa kile kinachoelezwa kuwa kutokana na kujengwa kwa kutokidhi viwango husika, ambapo barabara hiyo ujenzi wake unafanywa na kampuni ya FEI - MAC LTD kutoka mjini Songea na kusimamiwa na Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani hapa.


Kibao hiki kinaonyesha Mkandari husika aliyefanya kazi ya ujenzi wa barabara hiyo. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, ameshushiwa lawama nzito kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara kiwango cha lami katika eneo la Mbinga mjini mkoani humo, kutokana na barabara ambayo imejengwa na wakala huyo kuanza kubomoka tabaka la juu kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.

Barabara hiyo ambayo ujenzi wake ni wa kilometa moja, inagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja  na kwamba utekelezaji wake upo chini ya usimamizi wa wakala huyo.

Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na wakazi wa mji wa Mbinga walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa barabara hiyo baada ya magari kuruhusiwa kupita, hata kabla haijamaliza miezi miwili tabaka la juu la lami limeanza kubomoka.

Saturday, October 4, 2014

SHULE YAKOSA VYOO KAMATI YA UJENZI LAWAMANI

Baadhi ya watoto wa shule ya msingi Mbambi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa wakishuhudia kufanyika kwa tendo la mahafali kwa wanafunzi wenzao, ambao wamehitimu darasa la saba. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KAMATI ya ujenzi shule ya msingi Mbambi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa kuchukua hatua za haraka juu ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo ili kuwafanya wanafunzi, waweze kuondokana na tatizo la kupanga foleni pale wanapohitaji kujisaidia.

Aidha imeshushiwa lawama kwa kuzembea kutekeleza suala hilo huku ikielezwa kuwa mahitaji ya vyoo katika shule hiyo ni matundu 18 lakini yaliyopo sasa ni nane tu, ambayo hutumia wanafunzi hao na kufanya tatizo hilo kuwa kero miongoni mwao.

Hayo yalisemwa na Gerold Ndunguru alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba shule ya msingi Mbambi, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

“Ndugu zangu hii ni aibu kwa shule hii ambayo ipo hapa Mbinga mjini kusikia haina vyoo, napenda kusisitiza kamati ya ujenzi ione umuhimu juu ya jambo hili kupewa kipaumbele na namna gani inashirikisha wazazi kwa karibu katika kutatua kero hii”, alisema Ndunguru.

Thursday, October 2, 2014

WAKULIMA WA KAHAWA WAIANGUKIA SERIKALI, WAITAKA KUENDELEA KUIWEZESHA TaCRI

Meneja Kanda ya kusini wa Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa kituo cha TaCRI - Ugano kilichopo makao yake makuu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Godbless Shao akitoa maelezo mafupi juu ya maendeleo ya zao la kahawa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) walipokuwa katika kijiji cha Kilimani wilayani humo hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WAKULIMA wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitaka serikali kuendelea kuiwezesha taasisi ya utafiti wa zao hilo hapa nchini (TaCRI) kwa lengo la kuboresha uzalishaji kwa wakulima binafsi na waliopo katika vikundi, ili waweze kuzalisha miche ya kahawa kwa wingi.

Sambamba na hilo pia wameshauri halmshauri za wilaya mkoani humo ambazo hujishughulisha na kilimo cha kahawa, kuongeza maeneo ya uzalishaji kwa kufuata kanuni bora za kilimo, ikiwemo matumizi ya aina mpya ya miche ya kahawa (vikonyo) ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu kwa urahisi.

Rai hiyo ilitolewa na wakulima hao walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, ambao waliwatembelea kuona changamoto wanazokabiliana nazo na faida wanazopata baada ya TaCRI kutoa huduma zake.

Wednesday, October 1, 2014

JENEZA LAIBWA, LAKUTWA KWA AFISA MTENDAJI

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela

Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wasiofahamika wanaotuhumiwa kuingia msikitini na kuiba jeneza, wilayani Namtumbo, mkoani humo.

Baada ya kuiba jeneza hilo watu hao wanadaiwa kwenda nyumbani kwa Afisa mtendaji wa kijiji cha Kitanda wilayani humo, Fidea Mbawala (30) na kuliweka mlangoni, likiwa limesheheni matofali.

Kamanda wa Polisi mkoa huo Mihayo Msikhela, alisema  tukio hilo lililotokea juzi majira ya asubuhi katika kijiji hicho.

Alisema tukio hilo limesababisha kuwapo utata na kwamba uongozi wa msikiti umedai kuwa tukio hilo ni la aina yake, ambalo halijawahi kutokea.

IDADI YA WALIOKUNYWA TOGWA YENYE SUMU WAONGEZEKA


Na Muhidin Amri,
Songea.


IDADI ya watu walioathirika kutokana na kunywa kinywaji aina ya togwa ambacho kinasadikiwa kuwa na sumu, katika kijiji cha Litapaswi kata ya Mpitimbi wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imeongezeka kutoka 250 na kufikia watu 325.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema tukio ilo limetokea juzi katika kijiji hicho, wakati watu hao wakiwa kwenye sherehe ya kipaimara ya mwanafunzi wa darasa la sita Dickson Nungu ambaye anasoma  shule ya msingi  Litapwasi.

Kamanda Mihayo alifafanua kuwa kati ya waathirika hao watu 29 wamelazwa katika hospitali ya misheni Peramiho, ambapo kati yao wanaume wapo wane na wanawake 22.

WASHUSHIWA KIPIGO NA KUFARIKI DUNIA



Na Mwandishi wetu,
Ruvuma.

WATU wawili kati ya watatu ambao majina yao hayajafahamika hadi sasa mjini hapa, wanaodaiwa kuwa ni wezi  wamefariki dunia baada ya kushushiwa kipigo na wananchi wenye hasira kali, wakati wakiiba pikipiki.

Wezi hao walikamatwa wakiiba pikipiki tatu zenye namba za usajili T 5888 CJC, T363 BFL na T445 CJT zote aina ya Sanlg.

Katika tukio hilo wezi hao walimjeruhi kwa nondo  Vasco Dagama fundi pikipiki mkazi wa Matogoro Manispaa ya Songea na kumnyanganya pikipiki yenye namba za usajili T363 BFL aina ya Sanlg.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA DAWA KWA MGANGA WA KIENYEJI



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA



ANUANI YA SIMU:  POLISI RUVUMA   
NAMBARI YA SIMU 025-26 KAMANDA  WA POLISI  025-2602266    MKOA WA RUVUMA
FAX NO. 025-2600380 S.L.P.19,
 SONGEA.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MTU MMOJA AMEFARIKI KWA IMANI ZA KISHIRIKINA MKOANI RUVUMA

Mnamo tarehe 22/09/2014 majira ya saa kumi na moja jioni huko mtaa wa Ruvuma manispaa ya Songea Emeresiana Goliama (70), Mngoni, Mkristo na mkazi wa Ngahokola amefariki dunia wakati akipelekwa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa matibabu, baada marehemu na wana ukoo wenzake wapatao kumi, kwenda kwa mganga wa kienyeji maarufu kwa jina la Angaza aliyewaambia kuwa kati yao wanne ni wachawi akiwemo marehemu walinyolewa nywele na kunyweshwa dawa kitendo kilicho pelekea hali ya Emeresiana kubadilika ghafla.

Wanaukoo hao walifikia uamuzi wa kwenda kwa mganga baada ya kukaa kikao na kujadili matatizo ya ukoo wao ikiwa ni pamoja na kupata kichaa na ugonjwa wa kifafa, hivyo mganga aliwataja watu wanne kuwa ni wachawi 1. Meresiana Goliama, ambaye ndiye marehemu 2. Oruban Goliama, (75), mkulima, Mkristo, Mngoni na mkazi wa Ngahokola 3. Nikola Huma, (68), mkulima Mristo na mkazi wa Ngahokola 4. Razaria Matembo, (64), Mkristo, Mngoni, mkulima na mkazi wa Ngahokola.

Kufuatia hali hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linawashikilia watu watatu 1. Daudi Goliama (49), Mngoni, Mkristo na mkazi wa Ngahokola 2, Samson Goliama (40), Mngoni, Mkristo na mkazi wa Ngahokola wote hao wanamuita marehemu shangazi na 3. Rafael Goliama (29), Mngoni, Mkristo na mkulima wa Ngahokola ambaye ni mjukuu wa marehemu, kwa hatua zaidi za kisheria.

Aidha kufuatia hali hiyo wananchi wanatakiwa kutojihusisha na imani za kishirikina ambazo mwisho wake zinapelekea kupoteza maisha na chuki kwa jamii.