Monday, August 31, 2015

DOKTA MAGUFULI: SERIKALI ITAJENGA BARABARA YA MBINGA MBAMBA BAY BAADA YA UCHAGUZI MKUU


Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

MGOMBEA urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta John Magufuli amesema kuwa, mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu serikali itaanza mchakato wake wa kujenga barabara ya kutoka wilaya ya Mbinga kwenda Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami.

Sambamba na hilo alieleza pia serikali itaunganisha umeme wa gridi ya Taifa kutoka Makambako mkoa wa Njombe hadi hapa Ruvuma.

Dokta Magufuli alisema hayo leo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi wa wilaya hiyo, ambao walikusanyika kumsikiliza  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.

“Ndugu zangu nataka niwahakikishie haya ninayosema nilazima niyatekeleze, Tanzania ijayo ya Magufuli haitafanya mzaha juu ya kuleta maendeleo ya wananchi, nchi hii najua ina fedha nyingi sana lazima zitumike ipasavyo kwa manufaa ya jamii”, alisema Dokta Magufuli.

Saturday, August 29, 2015

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUTAMBUA MCHANGO WA KUINUA TAALUMA TUNDURU

Mkuu wa shule ya sekondari Frankweston mwalimu Hassan Mussa, akionesha cheti cha pongeza kwa baadhi ya walimu walioshiriki katika hafla hiyo.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WALIMU wanaofundisha katika shule za sekondari wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kujali na kutambua mchango wao katika kuinua elimu ambapo wilaya hiyo, ilianza kuporomoka.

Kwa nyakati tofauti walimu hao walitoa pongezi hizo, walipokuwa wakipokea vyeti vyao vya pongezi kutokana na shule zao kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, mwaka 2014.

Mkuu wa shule ya sekondari Frankweston Hassan Mussa, George Martin wa Mataka Sekondari na Elis Banda wa shule ya wasichana Masonya wilayani humo walieleza kuwa kitendo cha serikali kuwapatia vyeti hivyo, kimeonesha kujali ukuzaji wa taaluma na ujuzi ambao walimu wamekuwa wakiutoa kwa wanafunzi wao.

TAMCU TUNDURU YAPITISHA MAKISIO YAKE BILA MABADILIKO

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUTANO mkuu wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma (TAMCU – LTD) kimepitisha bila ya kuyafanyia mabadiliko, makisio ya mapato na matumizi shilingi milioni 345 katika msimu wa ununuzi wa mazao mwaka 2015 na 2016, huku kukiwa na ongezeko la asilimia 0.01 ikilinganishwa na makisio ya mwaka uliopita.

Aidha katika mkutano huo, wajumbe waliridhia kuuzwa kwa hisa 500,000 kati ya hisa zake 720,000 ili fedha zitakazopatikana zitumike kulipia deni la chama hicho, ambalo wanadaiwa na benki ya CRDB.

Maamuzi hayo yalifikiwa na Wajumbe wa mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi za chama hicho, zilizopo katika mtaa wa Kalanje mjini hapa ambapo maamuzi hayo yalifikiwa pia kutokana na chama hicho, kukua kwa mapato yake.

NAMATUHI SONGEA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Na Muhidin Amri,
Songea.

WAKAZI wa kijiji cha Namatuhi Halmashauri ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, watanufaika na kilimo cha umwagiliaji zao la mpunga baada ya halmashauri ya wilaya hiyo, kukamilisha ujenzi wa skimu ya kilimo hicho.

Halmashauri ilichukua maamuzi ya kujenga miundombinu hiyo, baada ya kuona wakazi hao wanashindwa kunufaika ipasavyo na shughuli za kilimo cha zao hilo kutokana na kukosekana kwa miundombinu husika ya uzalishaji mpunga, licha ya juhudi kubwa walizokuwa wakizifanya za uzalishaji wa zao hilo kila mwaka.

Sixbert Kaijage, ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini alisema hayo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kijijini humo, akizungumza na wakulima wa zao hilo.

Friday, August 28, 2015

KAPINGA KUWALETEA NEEMA WANANDILIMALITEMBO SONGEA

Cresensia Kapinga.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

CRESENSIA Kapinga ambaye ni mgombea udiwani kata ya Ndilimalitembo, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema atatumia nafasi hiyo ya uongozi mara baada ya kuingia madarakani, kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo wa kata hiyo hasa katika suala zima la kusukuma mbele maendeleo yao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha Kapinga amewashukuru wanachama wa CCM ndani ya kata hiyo, kwa maamuzi yao ya kumpatia heshima ya kugombea udiwani licha ya kukiri kwamba mchakato wa kura za maoni kwa tiketi ya chama hicho ulikuwa mgumu, hivyo atakapotimiza ndoto yake mara baada ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu, ataendeleza ushirikiano na wananchi wake katika kutekeleza yale yaliyopo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

“Endapo nitashinda kwenye kinyang’anyiro hiki cha uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, kubwa nitakalolifanya ni kutekeleza ilani ya chama changu ili niweze kuwaletea wananchi wangu maendeleo kwa haraka zaidi”, alisema Kapinga.

MANISPAA YA SONGEA YAPATA FEDHA ZA KUWAJENGEA UWEZO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Muhidin Amri,
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepokea kiasi cha shilingi milioni 345,213,000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watu wanaoishi katika mazingira magumu na kuziwezesha kaya maskini kuongeza kipato, ili waweze kuwa na uwezo wa kugharimia mahitaji yao muhimu katika maisha yao.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Nachoa Zakaria alisema hayo alipokuwa akizindua zoezi la malipo kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini, kutoka mitaa mitatu ya kata ya Ruvuma wilaya ya Songea ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu, uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mapema mwaka huu.

Nachoa alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 306,856,000 ni fedha za walengwa wenyewe, shilingi milioni 5,230,000 ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ni fedha zitakazokwenda ngazi ya mitaa kwa ajili ya shughuli za usimamizi.

Thursday, August 27, 2015

WANAFUNZI NAMTUMBO WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO YAO

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

MWITO umetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kuongeza juhudi katika masomo yao na kujiepusha kushiriki vitendo viovu vinavyoweza kukatisha ndoto yao ya kujiendeleza kimasomo kama vile kwa wanafunzi wa kike kupata mimba wakati wakiwa na umri mdogo, au virusi vya Ukimwi.

Aidha wametakiwa kuwa na dhamira ya kweli juu ya kusukuma maendeleo ndani ya wilaya yao, ili watakapohitimu masomo yao na kupata ajira warudi kwenye maeneo yao kuwatumikia wananchi na sio kwenda kufanya kazi katika mikoa au wilaya zingine ambako tayari wamepiga hatua kimaendeleo.

Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la watumishi, hasa kwa idara ya afya, elimu na kilimo ambako mahitaji ya watumishi wake ni makubwa.

Tuesday, August 25, 2015

DOKTA MAGUFULI KUTIKISA RUVUMA AGOSTI 30 MWAKA HUU

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

DOKTA John Pombe Magufuli, ambaye ni mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini anatarajiwa kupokelewa na maelfu ya wananchi na wapenzi chama hicho, katika kijiji cha Igawisenga wilayani Songea mkoani humo akitokea mkoa wa Njombe tayari kwa kuanza kampeni ya chama hicho ndani ya mkoa huo.

Waandishi wa habari waliozungumza na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kampeni ya CCM hapa Ruvuma, Ramadhan Kayombo alisema kuwa Dokta Magufuli na msafara wake unatarajiwa kupokelewa Agosti 30 mwaka huu, majira ya asubuhi katika kijiji hicho.

Kayombo alisema Chama hicho, kimejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kwamba mgombea huyo, wabunge na madiwani ndani ya mkoa huo wanafanyiwa kampeni zenye ustaarabu na sio vinginevyo.

NAMTUMBO WAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa minne ya maji iliyogharimu shilingi bilioni 2.7 ikiwa ni sehemu ya mikakati katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo, kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi sasa 2015. 

Miradi hiyo ya maji imejengwa kwenye kijiji cha Milonji, Mkongo njalamatata, Mkongo gulioni na Magazini sambamba na uchimbaji wa visima vifupi 12 vya maji ambavyo tayari wananchi wa maeneo hayo wameanza kuvitumia, jambo ambalo linawafanya waweze kuondokana na adha ya kutafuta maji umbali mrefu kama ilivyokuwa hapo awali.

Afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tekra Nyoni alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake mjini Namtumbo huku akiongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo, kumetokana na ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na wananchi wa maeneo hayo.

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU

Baadhi ya Waandishi wa habari mkoani Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Ushirika mjini Songea mara baada ya kumaliza mkutano wao wa kuwachagua viongozi watakaoingoza Klabu ya waandishi hao, mkoani humo.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ANDREW Kuchonjoma ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma (RPC) amewataka wanachama wake ndani ya klabu hiyo, kujiendeleza kielimu katika tasnia ya habari ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi, katika ulimwengu huu wa sayansi na tekinolojia.

Sambamba na hilo alieleza kuwa kuna kila sababu kwa mwandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, wakati wa kutekeleza majukumu ya kazi zake ya kila siku hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuweza kuepukana na matatizo au migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.

“Ndugu zangu kusoma ni jambo muhimu sana ambalo tunapaswa kulipatia kipaumbele, hapa Ruvuma kuna chuo cha habari ambacho nawashauri wenzangu tujiunge na tuweze kupata fursa ya kujiendeleza kielimu tusiishie kukaa tu bila kuwa na mawazo mapya ya kujiendeleza kielimu, katika taaluma hii tuliyonayo”, alisema Kuchonjoma.

NALICHO: TUMIENI KALAMU ZENU KUTANGAZA FURSA ZA MAENDELEO

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wamepewa changamoto ya kutumia kalamu zao ipasavyo kwa ajili ya kuandika na kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo ndani ya mkoa huo, hatua ambayo itaweza kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani humo.

Mbali na hilo wametakiwa kutumia nafasi waliyonayo kuhamasisha wananchi kupenda kushiriki katika shughuli za kimaendeleo, hususani kwa zile za kujitolea ili kuweza kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Chande Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, alitoa rai hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa chumba cha upasuaji akina mama wajawazito kinachojengwa na serikali katika hospitali ya wilaya hiyo, huku akiongeza kuwa ujenzi huo utatoa fursa kwa akina mama hao kuweza kupata huduma za matibabu kwa ufanisi zaidi.

Friday, August 21, 2015

ALIYEONGOZA KUNDI LA KUVAMIA WAANDISHI WA HABARI APANDISHWA KIZIMBANI

Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

DANIEL Komba (53) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kwa kosa la kumshambulia Mwenyekiti wa kijiji hicho na waandishi wa habari waliokwenda kijijini hapo, kutekeleza majukumu yao ya kikazi.

Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta, Seif Kilugwe alisema hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Issa Magori kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 7 mchana.

Inspekta Seif alisema kwamba, Komba akiwa na wenzake alimshambulia Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle na kumjeruhi eneo la usoni kitendo ambacho kilimsababishia maumivu makali mwilini mwake.

Tuesday, August 18, 2015

GAUDENCE KAYOMBO ADAIWA KUPANDIKIZA GENGE LA WAHUNI NA KUWADHURU WAANDISHI WA HABARI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kikundi cha zaidi ya watu 40 wanaodaiwa kupandikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gaudence Kayombo, katika kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kimewashambulia na kuwarushia mawe waandishi wa habari waliokwenda kijijini hapo, kutekeleza majukumu yao ya kikazi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela amezungumza na vyombo mbalimbali vya habari na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Agopsti 17 mwaka huu majira ya saa 6:30 kijijini humo, ambapo waandishi hao walivamiwa na kikundi hicho akiwemo na Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle kwa kupigwa na kurushiwa mawe.

Alisema Mwenyekiti Haulle ameumizwa mdomoni na puani ambako alipigwa na jiwe na mtu asiyejulikana na kwamba amepatiwa matibabu, katika hospitali ya wilaya hiyo na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Msikhela aliwataja waandishi wa habari mkoani Ruvuma, ambao walikumbwa na mkasa huo kuwa ni; Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya kampuni ya Businesstimes, Aden Mbelle na Pastory Mfaume kutoka redio Jogoo FM iliyopo mkoani hapa.

WANANCHI WATAKIWA KUPEWA ELIMU SAHIHI UTUNZAJI WA MISITU

Na Steven Augustino,
Masasi.

UKOSEFU wa ushirikishwaji na utoaji wa elimu ya kutosha juu ya uhifadhi shirikishi wa misitu ndiyo chanzo cha jamii, kuendelea kufanya shughuli za uvunaji holela wa mazao ya misitu.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji cha Ulungu kata ya Sindano wilayani Masasi mkoa wa Mtwara wameamua kufunga kwa muda usiofahamika ufanyaji wa shughuli zote za uvunaji mazao ya misitu, hadi pale watakapojiridhisha na maendeleo ya uoto wa asili katika msitu wa kijiji hicho.

Wananchi hao walibainisha hayo walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, ambao walitembelea kijijini hapo kutaka kujua mgawanyo wa mamlaka na majukumu katika usimamizi wa misitu kati ya Meneja wa misitu wa wilaya (TFS) na Afisa misitu wilaya (DFO) pamoja na kamati za maliasili za vijiji.

Saturday, August 15, 2015

GAUDENCE KAYOMBO ANYANG'ANYA VIFAA VYA MATANGAZO ALIVYOKINUNULIA CHAMA CHA MAPINDUZI MBINGA BAADA YA KUSHINDWA KWENYE UCHAGUZI KURA ZA MAONI

Gaudence Kayombo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MBUNGE wa Jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ambaye aliingia katika mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewashangaza wanachama wa chama hicho baada ya mbunge huyo kwenda ofisi za CCM wilayani humo kunyang’anya vifaa vya matangazo, ambavyo ni vipaza sauti baada ya kushindwa kwenye kinyanga’nyiro hicho cha kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini hapa, wanachama hao walisema kuwa Kayombo alifanya hivyo baada ya kuwasili katika ofisi hizo za chama Agosti 14 mwaka huu majira ya asubuhi, akionekana mtu mwenye hasira.

“Huyu Mbunge alipowasili pale ofisi za chama alitushangaza sana, alikuwa mtu mwenye hasira huku akizungumza kwa ukali anataka vifaa vyake vya matangazo ambavyo alikinunulia chama, huku akitamka maneno kwamba ameamua kufanya hivyo kwa sababu viongozi wa chama wilaya hawamtaki”, walisema.

TASAF TUNDURU YAWANOA WATAALAMU WA KUNUSURU KAYA MASKINI

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewaasa washiriki wa mafunzo ya uibuaji miradi kwa jamii kuwa wasikivu ili waweze kwenda kutoa ushirikiano katika hatua zote zitakazotakiwa kutekelezwa wakati wa utambuzi wa matatizo ya wananchi vijijini, hususani kwa yale yatakayolenga kuinua kipato katika jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku saba kwa wataalamu 26 kutoka ngazi ya kata wilayani humo wanaojengewa uwezo, kuhusu utaratibu wa kutekeleza miradi ya kutoa ajira kwa muda ambayo inatekelezwa chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu.

Sekambo alifafanua kuwa baada ya wataalamu hao kukamilisha mafunzo hayo, watakwenda kuungana na wenzao 46 vijijini kwa ajili ya kubaini fursa na kuibua miradi itakayotoa ajira za muda, hasa kwa uboreshaji wa mindombinu kwenye maeneo yao huku walengwa hao wakinufaika kwa kuongeza kipato chao.

Thursday, August 13, 2015

HATIMAYE KAMATI KUU YA CCM TAIFA YATENGUA MAAMUZI YA KURUDIA UCHAGUZI MBINGA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete, akiwa pamoja na Katibu mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

HATIMAYE Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, leo imetengua maamuzi ya kurudia kufanya uchaguzi wa kura za maoni katika kata ya Kihangimahuka na Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia vurugu zilizoendelea kushika kasi Ofisi za CCM wilayani humo kwa masaa kadhaa, ikidaiwa kwamba kurudiwa kwa uchaguzi huo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye alishindwa katika uchaguzi wa kura hizo zilizofanyika, Agosti Mosi mwaka huu.

Aidha maamuzi hayo yalifikiwa leo jioni hii, baada ya Kamati ya siasa ya wilaya hiyo kuketi kwa muda wa masaa matano wakijadili suala hilo ikiongozwa na Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kufuatia wanachama wa chama hicho baada ya kuandamana kuelekea kwenye Ofisi za Chama wilaya, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi huo kwenye kata hizo.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda alisema hayo mbele ya wanachama wa chama hicho ambao walikusanyika kwenye viwanja vya chama hicho, kusubiri hatma ya majibu hayo yaliyotolewa na Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi.

“Ndungu zangu wananchi wa Mbinga, kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu ya chama baada ya kuketi na kujadili suala hili, wamekubaliana kwamba hakuna uchaguzi utakaoendelea kufanyika, hivyo endeleeni na shangwe na vifijo msilete fujo”, alisema Mbunda.

VURUGU ZAENDELEA KUJITOKEZA KUPINGA KURUDIWA UCHAGUZI KURA ZA MAONI MBINGA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, wameandamana kuelekea kwenye Ofisi za chama hicho wakipinga kurudiwa uchaguzi kura za maoni katika kata ya Kihangimahuka na Ruanda wilayani hapa, kwa madai kwamba kufanya hivyo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye aliangukia pua katika uchaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, Agosti Mosi mwaka huu.

Tukio hilo la aina yake limetokea leo majira ya asubuhi katika makao makuu ya Ofisi za CCM wilaya, ambapo wanachama hao walionekana kujawa jazba huku wakidai maamuzi ya kurudiwa kwa uchaguzi huo sio sahihi na kwamba huenda ukakigawa chama na kuzua migogoro miongoni mwa wanachama.

Hali ya kata hizo ambako uchaguzi uliamriwa urudiwe na Kamati kuu ya chama hicho Taifa, hivi sasa imeendelea kuwa tete ambapo wanachama waliopo katika maeneo hayo nao wameandamana kupinga uchaguzi huku wengine wakitishia kukihama chama.

WATAKIWA KUJITOKEZA KUHAKIKI MAJINA YAO KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Mgombea ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, Manjolo Kambili akionesha baadhi ya kadi za CCM ambao waliamua kuukana uanachama wao na kuamua kujiunga na Chama cha wananchi CUF.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenda katika vituo vyao walivyojiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili wajiridhishe na kuhakiki kama majina yao, yameorodheshwa katika daftari hilo.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha wananchi CUF wilayani humo, Abdalah Rajabu Abdalah wakati alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea udiwani na ubunge, uliofanyika viwanja vya baraza la Idd mjini hapa.

Alisema kuwa katika tukio hilo la uhakiki wa majina hayo, tume ya uchaguzi nchini imetoa muda wa siku tano tu, hivyo ni muhimu wakaenda mapema kufanya uhakiki wa majina yao ili wasikose haki yao ya kumchagua kiongozi wanayemtaka katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Wednesday, August 12, 2015

GAUDENCE KAYOMBO AFUKUZWA NA WAPIGA KURA WAKE GARI LANUSURIKA KUPIGWA MAWE

Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

GAUDENCE Kayombo ambaye ni mgombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, amejikuta akiendelea kuwa katika wakati mgumu kwa madai kwamba baadhi ya wananchi wa kijiji cha Paradiso kata ya Ruanda kumfukuza kijijini hapo huku wakimwambia kwamba, wananchi hawataki kusikia taarifa ya kurudia tena kufanya uchaguzi wa kura za maoni katika kata hiyo.

Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa leo, Agosti 12 mwaka huu majira ya saa 2:20 wakati mgombea huyo akionekana katika maeneo ya kijiji hicho akiwa na gari lake ikidaiwa anapita kwenye kata hiyo kuhamasisha wapiga kura, wajitokeze kupiga kura ya maoni kwenye matawi yao kesho, Agosti 13 mwaka huu.

Hasira za wananchi hao zinafuatia baada ya CCM mkoani hapa, kutoa taarifa kwamba kutafanyika marudio ya uchaguzi wa kura za maoni katika kata ya Ruanda na Kihangimahuka kwenye jimbo hilo, baada ya matokeo ya awali kufutwa kwa sababu mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye jimbo hilo.

Marudio ya uchaguzi huo yanatokana pia na Kayombo kulalamikia juu ya hali hiyo kutoridhishwa nayo, huku wagombea wenzake wakibaki kumshangaa wengine wakisema amekosa kazi ya kufanya na huenda ni tamaa ya madaraka aliyonayo au hajakomaa kisiasa.

WATATU WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGANA NA LORI

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Na Steven ASugustino,
Tunduru.

WATU watatu ambao ni wakazi wa mtaa wa machinjioni mjini Tunduru mkoani hapa, wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha pikipiki waliyokuwa wamepanda baada ya kugongana na lori.

Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa ajali hiyo, ilitokea kijiji cha Chingulungulu nje kidogo ya mji wa Tunduru.

Imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi aliokuwa nao mwendesha pikipiki, ambaye alianguka ghafla mbele ya lori wakati akijaribu kupita.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema wanamshikilia dereva wa lori hilo anayefahamika kwa jina la Hassan Chimgege, ambaye alijisalimisha polisi baada ya tukio hilo.

Msikhela aliwataja waliopoteza maisha kwamba ni wachimbaji wa vito, ambao walitambulika kwa majina ya Peter Nyange na mwingine kwa jina la Dotho Msukuma ambaye alikwenda mjini Tunduru, kwa lengo la kutafuta maisha katika machimbo hayo.

CUF YATAMBA MAJIMBO YA TUNDURU KASKAZINI NA KUSINI


Wagombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF, Sadick Songoni kushoto wa jimbo la Tunduru kusini na Manjoro Kambili Tunduru kaskazini, wakiwapungia mkono wananchi wa Tunduru mjini wakati walipokuwa wamewasili kwenye viwanja vya baraza la Idd mjini hapa. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA cha wananchi (CUF) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimewataka wananchi wake kujipanga na kuweza kufanya mageuzi ya viongozi katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 25 mwaka huu wa kumchagua diwani, mbunge na Rais.

Katibu wa chama hicho wilaya ya Tunduru, Abdalah Rajabu Abdalah alisema hayo alipokuwa akiwatambulisha wagombea wa ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, Manjolo Kambili na kwa upande wa Tunduru Kusini, Sadick Songoni aliyeteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera kwenye jimbo hilo.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi ambao walihudhuria kwenye mkutano huo, uliofanyika viwanja vya baraza la Idd mjini hapa, Abdalah alisema kuwa chama hicho kimechukua jukumu la kuwatambulisha wagombea hao ili wanachama waweze kuwafahamu, kabla ya kuanza kwa mpambano wa kampeni Agosti 22 mwaka huu.

KATIBU CCM NYASA AENDELEA KUSHUSHIWA LAWAMA

Na Muhidin Amri,
Nyasa.

MAKADA tisa kati ya kumi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambao waliangukia pua katika mchakato wa kura za maoni kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Nyasa, wamemnyoshea kidole katibu wa chama hicho wilayani humo Grayson Mwengu, kuwa ndiye aliyechangia wao kushindwa vibaya katika mchakato huo.

Wanachama waliogombea nafasi hiyo na kushindwa kuwa ni Christopher Challe, Ebehard Haule, Adolph Kumburu, Dokta Stephen Maluka, Frank Mvunjapori, Alex Shauri, Gerome Mathayo, Cassian Njowoka na Oddo Mwisho walisema katibu huyo wa chama alikuwa akimpendelea mgombea mwenzao Stella Manyanya ambaye aliwashinda kwa idadi kubwa ya kura.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu; Alex Shauri, Christopher Challe na Stephen Maluka walisema kuwa katibu huyo wa chama wilaya hakuweza kutoa ushirikiano kwao, badala yake alikuwa akimkumbatia mgombea mmoja na kuwasusa wengine.

VITA KAWAWA AGARAGAZWA CHINI BAADA YA UCHAGUZI KURUDIWA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

HATIMAYE mchakato wa kura za maoni kuwapata wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo mawili ya Tunduru kaskazini na Namtumbo hapa mkoani Ruvuma, ambapo majimbo hayo yalichelewa kukamilisha mchakato huo kutokana na sababu mbalimbali, hivyo ulifanyika tena mwishoni mwa wiki na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwachagua Mhandisi Ramo Makani kuwa mgombea kwa jimbo la Tunduru kaskazini na Edwin Ngonyani jimbo la Namtumbo.

Mchakato haukukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kujitokeza kwa baadhi ya kasoro, ambazo zilisababisha wanachama walioshiriki kugombea nafasi hiyo kugomea matokeo husika kwa madai kwamba walichezewa rafu na wagombea wenzao.

Jimbo la Namtumbo uchaguzi kura za maoni ulilazimika kurudiwa kutokana na kuwepo kwa madai ya idadi kubwa ya kura zilizopigwa, tofauti na wanachama halisi waliostahili kupiga kura kitendo ambacho kililalamikiwa na wagombea wengine waliokuwemo kwenye mchakato huo.

Monday, August 10, 2015

CCM MBINGA YAMEGUKA BAADHI YA WENYEVITI WAKE WAHAMIA CHADEMA

Wenyeviti wawili wa vitongoji, Steven Mateso wa Mbinga mjini A akiwa na mwenzake wa kutoka kata ya Masumuni wakiwa pamoja kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA wakati waliporudisha kadi za CCM na kujiunga na chama hicho, kwenye eneo la viwanja vya soko kuu mjini hapa. 

Wananchi waliohudhuria mkutano wa CHADEMA Mbinga mjini eneo la soko kuu, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimesema kitaendelea kujenga misingi ya kutetea na kupigania haki na maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo, ili waweze kusonga mbele katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waondokane na umasikini.

Aidha chama hicho kimeeleza kuwa, katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu, watahakikisha wanashinda kwa kishindo kwa kuchukua viti vingi vya udiwani na ubunge katika majimbo ya Mbinga vijijini na mjini, hivyo wamewaomba wananchi waendelee kuwaunga mkono siku uchaguzi huo utakapofanyika ili waweze kufikia malengo husika.

Kenan Mkuzo ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Mbinga, alisema hayo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika kusikiliza mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya soko kuu, mjini hapa.

“Ndugu zangu wanambinga naomba niwaeleze, wakati wa kuburuzwa sasa umepita tunahitaji tupate viongozi bora watakaokaa madarakani na kuweza kupigania maendeleo yetu kwa moyo wa dhati, hatuhitaji viongozi lege lege ambao watalifikisha taifa hili mahali pabaya”, alisema Mkuzo.

TUNAPASWA KUWASAIDIA WALEMAVU

Mlemavu ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alinaswa na kamera yetu akiwa amefuatana na familia yake wakikatisha katikati ya mitaa mjini Tunduru mkoani Ruvuma kwa lengo la kuomba msaada kwa wasamaria wema, ili aweze kuendesha maisha yake ya kila siku. (Picha na Steven Augustino)

Saturday, August 8, 2015

KATIBU WA CHAMA CHA MAPINDUZI NYASA ALALAMIKIWA NA WANACHAMA WAKE

Abdulrahman Kinana.
Na Muhidin Amri,
Nyasa.

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kukamilisha mchakato wa kura za maoni hapa nchini, hali imekuwa si shwari kwa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambapo baadhi ya wanachama wake wameonekana kukatishwa tamaa kwa kile kinchodaiwa kuwa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Grayson Mwengu amekuwa akitengeneza makundi ndani ya chama hicho wilayani humo, jambo ambalo linahatarisha ustawi wake.

Kufuatia hali hiyo wanachama wa chama hicho walisema kuwa, huenda CCM ndani ya wilaya hiyo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, kisifanye vizuri katika nafasi ya Diwani, Mbunge na Rais kutokana na mambo yanayofanywa na katibu huyo ambayo yanaashiria kukipeleka chama kubaya.

Walifafanua kuwa tayari baadhi ya wanachama wameanza kujiondoa ndani ya chama na kujiunga na vyama vya upinzani, kwa kile kinachoelezwa kuwa wamechoshwa  na vitendo vya dharau na kukosekana kwa umoja na mshikamano uliokuwepo kwa muda mrefu na haya yote kukosekana huko, kumesababishwa na katibu huyo.

Friday, August 7, 2015

MOHAMED LAWA ALALAMIKIWA TUNDURU KWA KUMBEBA MGOMBEA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

SEKRETARIETI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, imeridhia kumtoa katika mchakato wa kusimamia uchaguzi wa kura za maoni, katibu wa chama hicho wilayani Tunduru mkoani humo, Mohamed Lawa ikiwa ni lengo la kukiondoa chama katika mgogoro uliojitokeza kati ya katibu huyo na wagombea ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini.

Akitangaza maamuzi hayo hivi karibuni, Katibu wa Chama hicho mkoani hapa, Verena Shumbusho alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kujiridhisha uwepo wa hoja za msingi, zilizotolewa na wagombea hao.

Shumbusho alifafanua kuwa maamuzi hayo yametokana na sekretarieti ya mkoa huo kuketi na kujadili hilo na kuchukua maamuzi ya kumteua Katibu wa jumuiya ya wazazi mkoani Ruvuma, Haji Tajiri ambaye alikuwa miongoni mwao kubakia Tunduru ili aweze kuendelea kusimamia mchakato huo hali ambayo iliweza kuleta matumaini kwa wagombea na kukubali, kuendelea na mikutano ya kujinadi katika jimbo hilo.

MWAMBUNGU AWAPA SOMO WANACCM RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa kuwa na upendo, umoja na ushirikiano katika maisha yao ya kila siku jambo ambalo litasaidia chama kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Aidha wamekumbushwa kuacha tabia ya kukatishana tamaa, kwani hali hiyo inaweza kuwaamsha wapinzani wao kutoka kwenye vyama mbalimbali vya kisiasa waweze kujipanga vizuri na kuleta ushindani mkubwa, kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi.

Rai hiyo ilitolewa na MKuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alipokuwa akizungumza na wanawake wa CCM kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa wabunge wa viti maalum, uliofanyika ukumbi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia Bombambili mjini Songea.

MWANDISHI WA HABARI KAPINGA AIBUKA KIDEDEA KATIKA KURA ZA MAONI

Cresensia Kapinga.
Na Muhidin Amri,
Songea.      

MWANDISHI wa habari mwandamizi, Cresensia Kapinga (40) ameibuka kidedea baada ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,  kumchagua kwa kura nyingi kupitia kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, kuwa mgombea kwa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama hicho Oktoba 25 mwaka huu.

Kapinga amefanikiwa kupata kura 527, dhidi ya wagombea wenzake Hashimu Fungafunga aliyepata kura 127, Francis Lungu kura 111 na Issa Kiwaneke aliyepata kura 27 ambapo huyu ni mwandishi wa pili mkoani hapa kushinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Mbali na Kapinga mwandishi wa habari mwingine ni, Dustan Ndunguru ambaye naye ameshinda kupitia mchakato huo wa kura za maoni kwa nafasi ya udiwani katika kata ya Kihungu, wilayani Mbinga mkoani humo.

Tuesday, August 4, 2015

MATOKEO UCHAGUZI KURA ZA MAONI NAFASI YA UBUNGE MBINGA VIJIJINI MARTIN MSUHA AIBUKA KIDEDEA

Kushoto ni Martin Msuha siku alipokuwa akichukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ofisi ya chama hicho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Anayemkabidhi fomu hiyo ni Katibu msaidizi wa chama hicho ndugu Mrope.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KUFUATIA vuguvugu la kisiasa ambalo limeendelea kushika kasi na kutishia hali ya amani katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kutokana na wananchi kuutaka uongozi husika wa chama hicho wilayani humo utangaze matokeo ya nafasi ya ubunge, hatimaye matokeo hayo yalitangazwa kwa jimbo la Mbinga vijijini majira ya saa 5:45 usiku.

Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwa jimbo hilo, kulikuwa na mvutano mkali ambao ulidumu kwa masaa 12, kutokana na kati ya wagombea nane waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho, mgombea Gaudence Kayombo kudaiwa kufanya mchezo mchafu wa kutaka kuchakachua matokeo kwa kata ya Ruanda na Kihangimahuka, ili yaweze kumpatia ushindi baada ya kuona hali ya upepo wa ushindi kwa upande wake inamwendea vibaya.

Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo lililazimika askari wake kuweka ulinzi mkali katika eneo la ofisi hizo za CCM, kutokana na baadhi ya wanachama kuleta vurugu huku wengine wakirusha mawe.

Monday, August 3, 2015

MATOKEO KURA ZA MAONI MBINGA UTATA MTUPU, HALI NI TETE WANACHAMA WAVAMIA ENEO LA OFISI ZA CCM WILAYA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALI ya kisiasa wilayani mbinga mkoa wa Ruvuma, si shwari au kwa maneno mengine imechafuka ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kimeingia katika hali tete kufuatia baadhi ya wanachama wa chama hicho wilayani humo, kuvamia katika eneo la ofisi za chama hicho na kuutaka uongozi wa CCM wilaya kutangaza matokeo ya uchaguzi kura za maoni kwa nafasi ya ubunge, kufuatia matokeo ya nafasi hiyo kukaa muda mrefu kwa siku mbili, bila kutangazwa.

Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo limeonekana askari wake wakidhibiti hali hiyo huku wengine wakionekana kubeba silaha za moto, na mabomu ya machozi.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho wameendelea kuandamana maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za CCM na kuonekana kuranda randa wakitamka maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka ni matokeo na sio vinginevyo”.

Hali hiyo imejitokeza leo kufuatia kutotangazwa kwa matokeo ya kura za maoni ya chama hicho tawala kwa muda wa siku tatu sasa, ambao umefanyika mapema Agosti Mosi mwaka huu, kwa jimbo la Mbinga mjini na Mbinga vijijini.