Sunday, April 30, 2017

WANANCHI MBINGA WASISITIZWA JUU YA MATUMIZI YA KONDOMU

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, wakijadiliana jambo mara baada ya kuhitimisha kikao chao cha baraza la Madiwani kilichoketi juzi mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa kuwa na mazoea ya kutumia Kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Vilevile kutokana na maambukizi hayo kuendelea kushika kasi katika mji huo, halmashauri hiyo imejiwekea utaratibu wa kusambaza Kondomu hizo katika maeneo ya starehe na kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali namna ya kuepukana na maambukizi hayo.

Hayo yalisemwa juzi na Kaimu Afisa maendeleo ya jamii wa mji huo, Alphonce Njawa wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya Kamati ya kudhibiti ugonjwa wa ukimwi katika halmashauri hiyo.

NAMTUMBO WAPOKEA WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI

Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

WAKATI Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini, Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma inatarajia kukamilisha kupokea walimu 25 wa masomo ya sayansi, ambao wamepangiwa kwenda kufundisha katika shule mbalimbali zilizopo wilayani humo.

Taarifa iliyotolewa na Afisa elimu wa halmashauri hiyo, Patrick Athanas inafafanua kuwa walimu hao watapelekwa katika shule hizo za sekondari ambapo kati yao wakiume wapo 22 na wa kike watatu.

“Mpaka sasa halmashauri yetu imepokea walimu 24 na kwamba mmoja bado hajaripoti, lakini baada ya siku chache atakuwa tayari ameripoti na kupelekwa katika kituo chake cha kazi”, alisema Athanas.

Saturday, April 29, 2017

DC NA MADIWANI WAKERWA NA HALI YA MJI WA MBINGA KUWA MCHAFU

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye, akihutubia jana baraza la Madiwani halmashauri ya mji wa Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


KUFUATIA kuwepo kwa hali ya kushamiri kwa uchafu katika mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye ameutaka uongozi wa mji huo uchukue hatua kwa kuhakikisha kwamba taka zote zilizopo kwenye maghuba zinaondolewa haraka iwezekanavyo na maeneo mengine ya mji yanakuwa katika hali nzuri ya usafi.

Aidha Nshenye alisema kila siku amechoka kupokea malalamiko Ofisini kwake kutoka kwa wakazi wa mji huo, ambapo ametaka kero hiyo ya kuuweka mji katika hali ya usafi kwa kuondoa taka zilizorundikana kwa muda mrefu kwenye maghuba inatekelezwa ili kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Nshenye alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Mji wa Mbinga, lililoketi katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Kila siku watu wanakuja kulalamika ofisini kwangu juu ya suala hili la uchafu, naagiza wekeni mikakati ya kuondoa taka hizi mapema ili zisiweze kuleta madhara kwa wananchi”, alisisitiza Nshenye.

SHIRIKA LA NDEGE ATCL KUANZA SAFARI ZAKE KESHO MKOANI RUVUMA


Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

SHIRIKA la Ndege ATCL hapa nchini kupitia ndege zake za Bombadier kwa mara ya kwanza litaanza safari zake Aprili 30 mwaka huu, kusafirisha abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma.

Kuanza kwa safari hizo mkoani hapa ni ishara nzuri kwa serikali ya awamu ya tano iliyodhamiria kuboresha huduma zake kwa wananchi,hususani katika sekta ya anga kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa, Mkuu wa mkoa  wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa ndege hiyo itawasili uwanja wa ndege wa Songea majira ya saa mbili asubuhi ambapo itafanya safari zake mara tatu kwa wiki yaani siku ya Jumatatu, Jumatano na Jumamosi.

Dkt. Mahenge amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kitendo chake cha kujenga historia kwa muda mfupi tangu aingie madarakani na kuweza kuboresha sekta ya anga, kwa kufungua viwanja vya ndege ambavyo vilikuwa havifanyi kazi inayostahili kwa muda mrefu.

Alisema kuwa kiwanja cha ndege Songea ni mojawapo kati ya viwanja hapa nchini ambavyo vilishindwa kufanya kazi vizuri, tena kwa muda mrefu na kusababisha kukosekana kwa usafiri huo ambao ni wa haraka na kuaminika na wananchi wengi ndani ya mkoa huo.

BABU ALIYEMPATIA UJAUZITO MJUKUU WAKE ATOKOMEA KUSIKOJULIKANA

Na Yeremias Ngerangera,     
Namtumbo.

PAMOJA na Serikali kuendelea kusisitiza wahalifu wanaowapatia mimba wanafunzi wa kike kufungwa miaka thelathini jela, bado baadhi ya jamii imekuwa ikiendelea na tabia hiyo kitendo ambacho kimekuwa kikikatisha ndoto za maendeleo ya maisha kwa watoto hao.

Aidha wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, tabia hiyo imekuwa ikiendelea kufanyika licha ya viongozi husika wilayani humo kukemea kwa nguvu na kupiga marufuku baada ya kuona kwamba imekuwa ikitishia maendeleo ya wanafunzi hao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa tatizo hilo limekuwa likiendelea kushamiri wilayani hapa, kutokana na jamii kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali hasa pale inapotaka kusimamia sheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wenye tabia hiyo.

Imeelezwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha badala yake ndiyo wamekuwa chanzo cha kuvuruga madai husika yasiweze kusonga mbele katika vyombo vya sheria ikiwa ni lengo la kuepuka kufungwa miaka 30 jela.

RAIS DOKTA MAGUFULI APOKEA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe na kufungua boksi kubwa lenye majina ya watumishi zaidi ya 9,932 waliobainika kuwa na vyeti vya kugushi mara baada ya jana kupokea taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti hivyo kwa watumishi wa umma kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Angela Kairuki katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia majina hayo pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kufungua boksi hilo kubwa lenye majina ya watumishi hao wa umma ambao wamegushi vyeti vyao. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakiangalia vitabu vyenye majina ya watumishi wa umma zaidi ya 9,932 waliogushi vyeti vyao vya elimu ya Sekondari. (Picha na IKulu)


JENISTA MHAGAMA AKUTANA NA UONGOZI WA SHIVYAWATA DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akizungumza jambo wakati wa mkutano wake juzi na viongozi wa SHIVYAWATA kujadili utekelezaji wa majukumu yao katika ukumbi wa ofisi yake Bungeni Dodoma.
Wajumbe wa mkutano wa uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa kikao chao mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiendesha mkutano na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) walipokutana ofisini kwake Dodoma kujadili utekelezaji wa majukumu yanayowahusu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa SHIVYAWATA mara baada ya kumaliza mkutano wao, kushoto kwake ni Naibu wake Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma)

Wednesday, April 26, 2017

RAIS DKT. MAGUFULI AONGOZA MAADHIMISHO MIAKA 53 YA MUUNGANO WA TANZANIA MJINI DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Alli Mohamed Shein kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na walioshiriki katika zoezi la kuchanganya udongo kuasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Gadi ya "Komando" la vijana likiwajibika kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Onesho la ndege za kivita kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Onesho la mbwa wa polisi kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Onesho la Komandoo wawili kuvuta lori la tani 7 kwa mikono kwenye sherehe za miaka 53 ya muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kikosi cha Komandoo wa JWTZ kikitoa heshima kwenye sherehe za miaka 53 ya Muungano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.(Picha zote na Ikulu)


NYASA WAIOMBA SERIKALI KUFANYA DORIA KANDO KANDO YA ZIWA

Na Muhidin Amri,      
Nyasa.

BAADHI ya wananchi wanaoishi katika vijiji vya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi wilayani humo kufanya doria ya mara kwa mara kando kando mwa ziwa Nyasa, ili kuweza kuwachukulia hatua   watu wenye mazoea ya kuoga ziwani wakiwa uchi wa mnyama.

Walisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikichochea na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya ngono zembe, miongoni mwa baadhi ya wananchi wanaoishi wilayani humo na kusababisha maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Kelvin Komba (42) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nkiri wilayani hapa alisema kwamba katika wilaya hiyo hususani vijijini kwenye makambi ya wavuvi, wanaume na wanawake wamekuwa na tabia hiyo tena huoga bila nguo huku wakiwa jinsia tofauti.

MSAMAHA WA RAIS KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 53 YA MUUNGANO TANZANIA

Dkt. John Magufuli.
KATIKA Maadhimisho ya Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania Aprili 26 mwaka huu 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

Wafungwa wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wawe wametumikia nusu (½) ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

WAAJIRI WATAKIWA KUHAKIKISHA MITAMBO NA VIFAA VYA KAZI VINAFANYIWA UKAGUZI MARA KWA MARA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde akitoa hotuba yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi uliofanyika Aprili 25 mwaka huu mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.     (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma)
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

SERIKALI imewataka waajiri wote na wadau kwa ujumla hapa nchini kuhakikisha kwamba maeneo au sehemu za kazi, mitambo na vifaa vya kufanyia kazi vinafanyiwa ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa havileti madhara kwa wafanyakazi.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

“Kwa upande wa Serikali jukumu letu kubwa ni kuweka na kusimamia sera ya Usalama na Afya mahali pa Kazi, kutunga na kusimamia sheria za usalama na afya mahali pa Kazi na kuweka viwango mbalimbali vya usalama na afya sehemu za kazi” alisisitiza Mavunde.

Mavunde alisema kuwa kwa sasa kanuni ya kuripoti ajali na magonjwa imekamilika na kuanza kutumika tangu mwezi Septemba, mwaka 2016.

DKT. MAGUFULI MGENI RASMI SHEREHE ZA MEI MOSI

RAIS Dkt. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa, huku kilio kikubwa cha vyama vya wafanyakazi kikiwa kukosekana kwa mikataba ya hali bora kazini.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na waajiriwa milioni 3.7 katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000 pekee, hali inayoashiria kutokuwa na mikataba.

Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Yahaya Msigwa alisema hayo juzi mjini Moshi ikiwa ni maandalizi ya Mei Mosi itakayofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

MSHAWEJI: MSIKUBALI KUGAWANYWA KWA MISINGI YA DINI, KABILA AU ITIKADI ZA KISIASA

Na Muhidin Amri,     
Songea.

VIJANA katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameaswa wasikubali kugawanywa au kutumika kwa misingi ya dini, kabila au itikadi za kisiasa kwa maslahi ya watu wachache kwani kufanya hivyo watakuwa wana tenda dhambi kubwa kwa makundi mengine katika jamii ambayo inahitaji haki na usawa.

Aidha wametakiwa kuwa imara na kujitambua kutumia muda wao mwingi katika shughuli za kujiletea maendeleo, sambamba na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kukatisha ndoto za maisha yao ya baadaye.

Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na vijana hao kutoka kata za Manispaa hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya namna ya kutafuta njia bora katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao.

Tuesday, April 25, 2017

SERIKALI YAMTIMUA MKURUGENZI WA UNDP HAPA NCHINI

Bi. Awa Dabo.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeliagiza Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (United Nations Development Programs – UNDP) kwa upande wa Tanzania kumuondoa nchini Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Awa Dabo.

Serikali ilifikia uamuzi huo kutokana na Bi. Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya Watumishi wenzake na Menejimenti ya Shirika hilo, hivyo kupelekea kuzoretesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.

Baada ya kuthibitishiwa kuondoka nchini, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP kuwakumbusha Watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na Serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya Mwaka 2030.

Mwisho.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasilino ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 25 Aprili, 2017.

JENISTA MHAGAMA AWATAKA WATANZANIA KUWA WAZALENDO NA KUDUMISHA AMANI ILIYOPO

Waziri Mhagama akikagua maandalizi ya kuadhimisha sherehe za miaka 53 ya Muungano katika viwanja vya Jamhuri leo mjini Dodoma.

Na Immaculate Makilika,

Maelezo Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Ajira na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama amewaasa Watanzania kuwa wazalendo pamoja na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza mjini Dodoma wakati akifuatatilia maandalizi ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yatakayofanyika Aprili 26 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri uliopo mjini hapa.

“Tunapoadhimisha miaka 53 ya Muungano ninawaomba watanzania kuwa wazalendo pamoja na kulinda amani ya nchi”, alisema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama aliwaomba watanzania hasa wakazi wa Dodoma, kuhudhuria pia kwa wingi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Aprili 26 mwaka huu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema kuwa mkoa wake umejipanga vizuri katika kufanikisha maadhimisho hayo ambapo pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuhamasisha wananchi juu ya sherehe hizo.

TAKUKURU RUVUMA YAFANYA JITIHADA YA KUOKOA MAMILIONI YA FEDHA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma, imeweza kuokoa kiasi cha shilingi milioni 91.811 katika idara ya elimu na kilimo mkoani humo ikiwa ni mishahara hewa ambayo walikuwa wakilipwa watumishi ambao hawakuwa kazini.
Yustina Chagaka.

Uokoaji huo umefanywa kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu ambapo kati ya fedha hizo, sekta ya elimu iliokoa shilingi milioni 61.078 na kilimo milioni 2.233.

Aidha katika sekta ya ujenzi sehemu ya fedha hizo waliweza kuokoa milioni 28.5 baada ya kulipwa mkandarasi ambaye alikuwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mpitimbi B hadi Mbinga Mhalule, halmashauri ya wilaya ya Songea kwa kazi ambazo hazikufanyika na kwamba aliamriwa kuzirejesha.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoani hapa, Yustina Chagaka alibainisha hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji wa TAKUKURU katika miezi hiyo, kwa waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea.

Katika hatua nyingine alifafanua kuwa wameweza kupokea taarifa 173 kutoka kwa wananchi katika kipindi hicho kupitia vyanzo mbalimbali.

TUKIO KATIKA PICHA: DED NAMTUMBO AKIPATA MAELEZO JUU YA UTAALAMU WA KUZALISHA MAZAO KWA WINGI SHAMBANI

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Christopher Kilungu mwenye koti na tai akipata maelezo kutoka kwa Abiud Gamba ambaye ni Mratibu wa mradi wa kilimo hifadhi mwenye vitabu mkononi juu ya namna ya kuzalisha mazao kwa wingi kwa njia ya kilimo hifadhi katika kijiji cha Namanguli wilayani humo, upande wa kulia kwa Mkurugenzi huyo ni Afisa kilimo wa wilaya ya Namtumbo Ally Lugendo wakiangalia shamba la mkulima Stephen Nguru aliyezalisha kwa kutumia utaalamu huo.

Sunday, April 23, 2017

TCB YAWAPIGA JEKI WAKULIMA WA KAHAWA

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MWENYEKITI wa Mfuko wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Hyasint Ndunguru amesema kuwa bodi hiyo hapa nchini, imetoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya kugharimia nusu ya bei ya miche bora ya kahawa kwa wakulima.

Ndunguru alisema kuwa gharama hiyo imelipwa kwa Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) ambao ndiyo wanaozalisha miche hiyo kwa gharama ya shilingi 300 kwa kila mche mmoja wa kahawa.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo katika kikao cha Wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma kilichofanyika mjini Songea kwenye ukumbi wa Hanga, ambapo wadau hao walikutana kwa lengo la kuhamasishana namna ya kudumisha ubora wa zao la kahawa mkoani hapa. 

MADIWANI NA WABUNGE WANGING'OMBE WADAIWA KUHAMASISHA WANANCHI KUHARIBU VYANZO VYA MAJI

Uharibifu namna unavyoendelea.
WANANCHI waishio katika tarafa ya Wanging'ombe mkoani Njombe wapo hatarini kukumbwa na baa la njaa, kufuatia eneo la tarafa hiyo kukosa mvua kwa muda mrefu na mazao yao kushindwa kuendelea kustawi kutokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji.

Hayo yamebainika kufuatia kikosi kazi kilichoundwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutembelea katika eneo hilo na kushuhudia uharibifu uliofanyika.

MAOFISA UGANI WAZEMBE MKOANI RUVUMA WATAFUTIWA MWAROBAINI WAO

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amesema kwamba Maofisa ugani waliopo katika mkoa huo wengi wao wamekuwa wakifanyabiashara zao binafsi, badala ya kutekeleza majukumu ambayo wamepewa na serikali katika kuwatumikia wananchi vijijini kwenye shughuli za kilimo.

Aidha amewanyoshea kidole akieleza kuwa serikali itawachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

DKt. Mahenge alisema hayo juzi alipokuwa akihutubia kwenye kikao cha Wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hanga uliopo katika Manispaa ya Songea mjini hapa.

Alisema kuwa wataalamu hao wa masuala ya kilimo wanapaswa kwenda vijijini kuwatumikia wakulima kwa kuhakikisha wanawapatia mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili yaweze kuwa yenye ubora unaokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Sunday, April 16, 2017

DC MBINGA KUWACHUKULIA HATUA WATAKAOKIUKA AMRI HALALI KATIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA NGURUWE

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ametoa amri ya kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaokiuka amri halali ya kupambana na ugonjwa wa homa ya nguruwe, African Swine Fever ambao umeingia katika halmashauri ya wilaya hiyo.
Cosmas Nshenye.

Aidha ugonjwa huo ambao umeingia katika kata ya Kitura na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji wa wanyama hao, ambapo nguruwe 18 wamekufa na hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa ili usiweze kusambaa katika maeneo mengine jirani na kuleta hasara zaidi.

Nshenye ametoa amri hiyo kupitia nakala yake ya barua ya Aprili 10 mwaka huu yenye kumbukumbu namba AB. 120/475/01/18 iliyosambazwa kwa viongozi wa wilaya hiyo ambayo mwandishi wetu anayo nakala yake ikisisitiza juu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Mimi Mkuu wa wilaya hii kwa mujibu wa sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na sheria ya magonjwa ya mifugo natoa amri ya kuwachukulia hatua wale wote watakaoshindwa kufuata maelekezo, amri, zuio na katazo hili ambalo limetolewa kisheria chini ya mamlaka halali ya sheria kifungu cha 62 – 1 cha masharti ya karantini dhidi ya ugonjwa wa homa ya nguruwe”, alisema Nshenye.

KAMPUNI YA PANNAR TANZANIA LIMITED YAENDELEA KUJIVUNIA MAFANIKIO YAKE MKOANI RUVUMA

Ofisa masoko wa Kampuni ya Pannar Tanzania Limited mikoa ya Nyanda za juu kusini, Sabasaba Manase upande wa kushoto mwenye miwani akiwaonesha baadhi ya wakulima ambao hawapo pichani shamba darasa lililofanikiwa uzalishaji wa mahindi baada ya kutumia mbegu aina ya Pannar 691 katika kijiji cha Namabengo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kulia kwake ni mmiliki wa shamba hilo Agnellus Komba.
Na Julius Konala,     
Namtumbo.

MKULIMA mmoja wa kijiji cha Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Agnellus Komba ameipongeza Kampuni ya Pannar Tanzania Limited kwa kumwezesha elimu juu ya kilimo bora cha kisasa kwa kutumia mbegu za kampuni hiyo akidai kwamba, imeweza kumuinua kiuchumi na kumfanya aondokane na umaskini.

Hayo yalisemwa juzi na mkulima huyo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kijijini hapo, akielezea siri ya mafanikio na mbinu mbalimbali zilizomfanya aweze kufanikiwa katika kuendesha shughuli zake za kilimo kwa kutumia mbegu bora za mahindi za Pannar.

Komba alisema kuwa tangu aanze kuendesha kilimo hicho kwa kutumia mbegu hizo ameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kujenga nyumba bora, kufungua duka, kununua usafiri, kusomesha watoto wake pamoja na kufuga kuku na ngombe ambapo amedai kuwa awali kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa analima kwa njia za kawaida ambazo zilikuwa hazina tija kwake.

Saturday, April 15, 2017

MKUU WA WILAYA MBINGA AWATAKA WAKURUGENZI WAKE KUFUATILIA MAENDELEO YA WAKULIMA VIJIJINI

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MKURUGENZI wa halmashauri ya mji, Robert Mageni na wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito mkoani Ruvuma wametakiwa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya wakulima wa kahawa vijijini, ili waweze kujua ni matatizo gani wanakabiliana nayo katika uzalishaji na uendelezaji wa zao hilo na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.

Aidha maofisa ugani katika halmashauri hizo nao wamenyoshewa kidole wakilalamikiwa kwamba muda mwingi wamekuwa wakikaa maofisini kwa kutotembelea mara kwa mara wakulima hao kwa lengo la kuweza kuwapatia elimu namna ya uzalishaji bora wa zao hilo.

Hayo yalitokea juzi katika kikao cha wadau wa kahawa kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye aliwataka viongozi hao na maofisa kilimo kuhakikisha kwamba sasa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kwenda kwa wakulima vijijini kutatua matatizo katika sekta ya kilimo yanayowakabili.

“Nawataka Wakurugenzi wote wawili na maofisa kilimo simamieni na fuatilieni hili suala la maendeleo ya wakulima hawa ni lazima wapitieni huko waliko ili kuweza kujua wana matatizo gani yanayowakabili”, alisisitiza Nshenye.

DC MBINGA APIGA MARUFUKU MAKAMPUNI KUHIFADHI KAHAWA KWENYE MATURUBAI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akihutubia katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika juzi mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MAKAMPUNI yanayonunua zao la kahawa katika halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yamepigwa marufuku kuhifadhi zao hilo kwa kutumia maturubai, badala yake wanapaswa kuhifadhi kwenye maghala ili kuweza kudhibiti ubora wake.

Vilevile agizo limetolewa kwamba ili kuweza kuendelea kuongeza ubora wakati wa mavuno ya zao hilo, makampuni hayo yanapaswa kukoboa kahawa kwa kutumia mashine za CPU’S kuliko kuwaachia wakulima wakoboe majumbani kwa njia ya kawaida.

Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha wadau wa kahawa ambacho kiliketi mjini hapa kwa lengo la kujenga mikakati ya uendelezaji wa zao hilo.

“Sisi kama viongozi tutaendelea kusimamia sheria za kilimo cha zao hili nawataka pia makampuni yote yanayonunua kahawa jengeni ushirikiano na serikali tuweze kuwa pamoja, sote tunaamini wafanyabiashara na serikali tukiwa pamoja ndiyo tunaweza kuendesha maendeleo ndani ya nchi yetu”, alisema.

Kadhalika aliongeza kuwa kwa makampuni, vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima ambavyo vitaonekana kufanya vibaya kwa kukiuka taratibu na sheria ameapa kwamba atavifutia usajili wake.

Friday, April 14, 2017

UGONJWA UNAOUA NGURUWE WAINGIA MBINGA NA KUSHAMBULIA NGURUWE KATIKA KIJIJI CHA KITURA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

UMETOKEA ugonjwa wa nguruwe aina ya African Swain Fever, katika kijiji cha Kitura kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma na kusababisha nguruwe 18 kufa katika kijiji hicho, baada ya kuripotiwa wakiwa na ugonjwa huo.

Aidha imeelezwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo kutokea kijijini hapo umesababishwa na mama mmoja ambaye hakutajwa jina lake akitokea mkoa wa Njombe, baada ya kusafirisha nyama ya nguruwe na kupeleka katika kata hiyo kwa lengo la kubadilishana na zao la kahawa kwa wananchi wanaoishi huko.

Hayo yalisemwa jana na Daktari Mkuu wa mifugo halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Patrick Banzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake huku akieleza kuwa hauna madhara kwa binadamu lakini endapo ukiingia sehemu yoyote ile yenye wanyama hao umekuwa ukiua nguruwe wengi kwa muda mfupi.

HDT WAFANIKIWA KUWARUDISHA WALIOPOTEA KUMEZA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI WILAYANI MBINGA

Ofisa unasihi na upimaji wa shirika la Health Promotion Tanzania (HDT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Zawadi Mtambo.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT) lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) limefanikiwa kuwarudisha watu 1,229 ambao walipotea kumeza dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo na kuwarudisha katika Vituo vya tiba (CTC) kwa ajili ya kupata huduma endelevu.

Aidha kati ya hao taarifa za awali zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 717 waliopotea ambapo HDT walifanikiwa kuwarudisha wagonjwa 507 ambao sasa wanaendelea kumeza dawa hizo.

Kadhalika katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu kulikuwa na wagonjwa 1,684 waliopotea na sasa wamerudishwa wagonjwa 722 hivyo zoezi hilo utekelezaji wake umefikia asilimia 42.9 ambapo malengo ya shirika katika utekelezaji huo ni kufikia asilimia 80 na kwamba kazi hiyo bado inaendelea.

Thursday, April 13, 2017

MBUNGE WA MADABA AWATAKA WALIMU KUFUNDISHA KWA BIDII

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

MBUNGE wa Jimbo la Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Joseph Mhagama amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kuona umuhimu wakufanya kazi kwa bidii, katika kuwafundisha watoto darasani masomo ya sayansi na kuacha visingizio kwamba wilaya hiyo ina uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo.

Kauli hiyo ya Mbunge huyo aliitoa juzi wakati alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali katika jimbo hilo, ikiwemo ujenzi wa madarasa manne ya shule ya sekondari Mahanje na shule ya msingi Nkwera zilizopo wilayani hapa.

Mbunge huyo ambaye alichangia pia shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujenzi wa majengo hayo ili yaweze kukamilika ujenzi wake kwa wakati na yaweze kuanza kutumika.

MBINGA YAONGOZA KWA KASI YA MAAMBUKIZI UGONJWA WA UKIMWI MKOANI RUVUMA

Dkt. Joachim Henjewele.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

IMEELEZWA kwamba, hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, inaendelea kukua kwa kasi ambapo hivi sasa kwa pamoja halmashauri hizo zimekuwa zikiongoza kwa asilimia 9.6 ya maambukizi ya ugonjwa huo, ukilinganisha na kiwango cha mkoa huo ambacho ni asilimia 7.2.

Takwimu hizo zimetolewa katika kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana hadi Machi mwaka huu, ambapo jumla ya watu 2,890 waliweza kupimwa na kwamba waliogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo kati ya hao walikuwa ni watu 278.

Hayo yalisemwa na Dkt. Joachim Henjewele ambaye ni Meneja Mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT) lililopo mjini hapa, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ndani ya halmashauri hizo wakati alipokuwa akizungumza juzi na waandishi wa habari ofisini kwake.

Monday, April 10, 2017

GAMA AVIMWAGIA MAMILIONI VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI MANISPAA YA SONGEA

Na Julius Konala,   
Songea.

MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama ametoa mkopo wa shilingi milioni 13 kwa ajili ya vikundi mbalimbali 26 vya ujasiriamali jimboni humo, kwa lengo la kuvisaidia kukua kiuchumi ili waweze kuondokana na umaskini.

Akikabidhi hundi hizo mwishoni mwa wiki kwa viongozi wa vikundi vya ujasiriamali kwa niaba ya Mbunge huyo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea, Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema amewataka wajasiriamali hao kutumia mikopo hiyo kwa kazi iliyokusudiwa.

Mgema aliwaonya wajasiriamali hao kuacha tabia ya kutumia fedha hizo kwa mambo ya anasa ikwemo kwenye mambo ya ulevi, mashindano ya kuvaa nguo pamoja na kucheza mchezo wa kupeana jambo ambalo alidai kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha wakashindwa kurejesha mkopo huo kwa wakati.

SERIKALI YALALAMIKIWA KWA KUTOIFANYIA UKARABATI SHULE KONGWE YA SEKONDARI KIGONSERA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

WANAFUNZI wa shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia serikali kwa kutoifanyia ukarabati shule hiyo kwa muda mrefu kutokana na majengo yake kuwa chakavu jambo ambalo linahatarisha hata usalama wao.

Aidha walisema kuwa majengo mengi yakiwemo mabweni ya kulala wanafunzi hao, vyumba vya madarasa ya kusomea pamoja na vyoo yapo katika hali mbaya na kwamba kuna kila sababu sasa kwa serikali kuchukua hatua juu ya namna ya kuyafanyia ukarabati ili waweze kuondokana na adha hiyo.

Malalamiko hayo yalitolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, katika mahafali yao ya 18 ya wahitimu kidato cha sita yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani hapa.

Salum Hassan ambaye ni mwanafunzi anayetarajia kuhitimu mwaka huu alisema kuwa katika kipindi chote cha miaka miwili ambayo yeye na wenzake wameishi shuleni hapo, wamekuwa wakikumbana na adha hiyo huku wakati mwingine wakihofia hata kuangukiwa na majengo ya shule hayo kutokana na uchakavu uliopo.

Sunday, April 9, 2017

MANISPAA YA SONGEA KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAJI SAFI NA SALAMA

Na Julius Konala,      
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.325 katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji, kwa lengo la kuwafikishia wananchi wa Manispaa hiyo huduma ya maji safi na salama.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Songea, Samwel Sanya alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake kwa lengo la kuelezea utekelezaji mbalimbali wa miradi ya maji katika Manispaa hiyo.

Sanya alisema kuwa tangu mwaka 2007 halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza programu ya maji na usafi wa mazingira katika mitaa 10 ikwemo Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Muungano, Mahinya, Ngandula, Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa, Ruhila kati na Liwumbu.

WADAU MBALIMBALI WATAKIWA KUCHANGIA UJENZI WA HOSPITALI NAMTUMBO

Na Kassian Nyandindi,      
Namtumbo.

KATIKA kuhakikisha kwamba huduma za tiba zinaendelea kuboreshwa, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imejiwekea mikakati ya kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo, ili ujenzi huo uweze kufanyika kwa urahisi.
Luckness Amlima.

Aidha kampeni ya uhamasishaji huo itafanyika kuanzia mwezi Julai mwaka huu na kwamba fedha zitakazopatikana, zitaweza kufanya kazi ya ujenzi wa majengo ya hospitali pamoja na kuimarisha miundombinu mingine katika sekta ya afya wakati ujenzi huo utakapofanyika.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi juu ya mikakati yake ya kukuza maendeleo katika sekta hiyo ya afya wilayani humo.

Amlima alisema kuwa wananchi waliopo ndani ya wilaya hiyo na nje ya wilaya anawaomba wajitokeze kwa wingi wakati kampeni hiyo itakapozinduliwa ili kuweza kufikia malengo ambayo wilaya imejiwekea katika kupambana na kufikia malengo ya ujenzi wa hospitali hiyo.