Na Muhidin Amri,
Madaba.
WANANCHI wanaoishi katika vijiji vilivyopo kwenye Halmashauri
ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, wanatarajia kuanza kunufaika na mradi wa
nishati ya umeme ambao utasambazwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Mradi huo unatarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti mwaka huu,
ambapo serikali imepeleka Jenereta kubwa ambalo litajengwa kwa ajili ya
kusambaza nishati hiyo muhimu.
Aidha mbali na kuusambaza kwenye vijiji hivyo, pia utapelekwa
makao makuu ya Ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kusaidia kuimarisha
mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya Kielektroniki.
Shafi Mpenda ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Madaba alisema hayo kuwa Jenereta hilo limetolewa ikiwa ni sehemu ya
ahadi ya Rais Dokta John Magufuli ya kupeleka nishati ya umeme nchi nzima kwa ajili
ya kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Mpenda aliongeza kwa kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya
maandalizi ya kuupokea umeme huo kwa kujenga miundombinu husika kwenye nyumba
zao ili waweze kuunganishiwa nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ni kwamba dhamira ya Serikali
ya awamu ya tano ni kutaka kuona umeme huo unatumika kwa ajili ya kuanzisha viwanda
vidogo na vikubwa ili kukuza na kuharakisha ukuaji wa maendeleo ya wananchi
wake.
Pia umeme huo utawasaidia wananchi wa Madaba kuweza kuanzisha
viwanda vidogo vidogo vya kusindika matunda kutokana na hivi sasa wengi wao
huzalisha matunda mengi na huishia kuoza kutokana na kutokuwepo kwa viwanda
hivyo kwa ajili ya usindikaji.
No comments:
Post a Comment