Na Muhidin Amri,
Songea.
WAENDESHA Pikipiki wawili wamefariki dunia baada ya Pikipiki
zao walizokuwa wakiendesha kugongana wakiwa katika mwendo kasi katika kijiji
cha Hanga kata ya Hanga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gemini Mushy alisema kwamba tukio
hilo lilitokea juzi katika kijiji hicho majira ya usiku.
“Vifo vya watu hawa vilitokea baada ya Pikipiki aina ya
Yamaha yenye namba za usajili T 403 AGB iliyokuwa ikiendeshwa na Francis
Mbawala (26) mkazi wa Mfaranyaki Hanga kugongana na Pikipiki nyingine
ambayo haijafahamika namba zake za usajili”, alisema.
Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma alifafanua kuwa Pikipiki
nyingine ilikuwa ikiendeshwa na Sebastian Ngonyani (26) ambaye ni mkazi wa
kijiji cha Hanga kata ya Hanga wilayani Namtumbo, ambapo ilitoroshwa na watu
wasiofahamika mara baada ya tukio hilo kutokea hata hivyo Jeshi la Polisi
linaendelea kuwatafuta watu waliotorosha Pikipiki hiyo.
Aidha alisema kuwa Pikipiki hizo zilikuwa na mwelekeo mmoja
zikitokea kijiji cha Kitanda kuelekea Hanga na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni
ulevi baada ya waendesha Pikipiki hao kunywa pombe na kuendesha vyombo hivyo
vya moto wakiwa katika mwendo kasi.
Kamanda Mushy ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto waache
kutumia vileo wakati wanapoendesha vyombo hivyo, ili kuepusha kuweza kuleta
madhara kama vile ulemavu au vifo.
Pamoja na mambo mengine amewataka madereva wa Pikipiki
kuwasha taa muda wote wanapokuwa wanatumia vyombo hivyo wakiwa barabarani hasa nyakati
za usiku, ili kuwezesha watumiaji wengine wa barabara kuweza kuona Pikipiki hizo
zinapokuwa umbali mrefu na kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuleta madhara.
No comments:
Post a Comment