Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SAKATA la Mgogoro wa fedha za mapato
yatokanayo na uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, limechukua sura mpya kufuatia baraza la Madiwani wa
halmashauri hiyo kumsimamisha kazi Afisa misitu wa mji huo, David Hyera ambaye
anadaiwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika ubadhirifu wa mapato hayo.
Aidha kusimamishwa kazi kwa afisa
huyo ni kwa ajili ya kupisha uchunguzi baada ya Madiwani hao kukubaliana kwamba
iundwe Kamati maalumu ya kuchunguza suala hilo ili kuweza kupata ukweli zaidi
wa jambo hilo na hatimaye hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika
watakaopatikana wameshiriki wizi huo.
Maamuzi hayo yalifikiwa juzi kwenye kikao
cha robo ya nne cha baraza lao kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo
uliopo mjini hapa, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndunguru Kipwele ambapo
walieleza kuwa makisio ya awali baada ya kufanyika upembuzi yakinifu na
mtaalamu huyo wa misitu na kuwasilishwa katika kikao cha baraza kilichoketi
Oktoba 12 mwaka jana, yalikuwa zipatikane zaidi ya shilingi milioni 325 ambazo
ni baada ya uvunaji huo kufanyika lakini wanashangaa kuelezwa kwamba
zimepatikana shilingi milioni 196.
Akichangia hoja katika kikao hicho diwani
wa kata ya Mpepai, Benedict Ngwenya alisema kuwa shughuli za uvunaji wa msitu
wa Mbambi kabla hazijaanza kufanyika kupitia vikao husika walikubaliana kwamba
Kamati husika ya mipango miji na mazingira ilibidi iende kwenye eneo la msitu
huo na kujiridhisha lakini kamati hiyo ilizuiwa isiende huko kwa ajili ya kuukagua msitu huo na badala yake
anadaiwa kwenda Mkurugenzi mtendaji, Robert Mageni na wataalamu wake.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kamati yako
haikupata nafasi ya kwenda kule mlimani kuona ule msitu kabla ya kuuvuna
walizuiwa wasiende leo baraza hili sisi tuna mashaka na kitendo hiki
kilichofanyika huu ni wizi uliokuwa wazi kimsingi mimi sijaridhika na shughuli zilizokuwa
zinafanywa kule mlimani,
“Mbinga tunalaana kubwa leo hii ni
mara ya pili kutokea tatizo kama hili kipindi cha nyuma wakati unavunwa msitu
wa Ndengu kulikuwa na matatizo kama haya mheshimiwa Mwenyekiti jambo hili ni
zito linaharufu ya ufisadi mkubwa, ambao haujawahi kutokea katika mji wa Mbinga
binafsi nina haki ya kutoa hoja ya thamani ya fedha za msitu ule ni zaidi ya
fedha zinazosemwa hapa leo”, alisema Ngwenya.
Naye diwani wa kata ya Kilimani Simon
Ponera alisema kuwa msitu huo ulikuwa na hekta 135 ambazo ndani yake kuna ekari
75 huku kila ekari ikiwa na miti 640 endapo ikichanwa mbao ilibidi zipatikane
mbao nyingi ambazo kama zingeuzwa ipasavyo kwa usimamizi mzuri mapato yake
yangeweza kumaliza kero mbalimbali za miradi ya maendeleo ya wananchi ndani ya
halmashauri ya mji wa Mbinga.
Raphael Kambanga diwani wa kata ya Masumuni
na Kelvin Mapunda wa kata ya Betherehemu kwa nyakati tofauti walichangia hoja
wakisema kuwa ni ajabu kuona kwamba pamoja na msitu huo kuvunwa, lakini hata wafanyakazi
waliokuwa wakifanya shughuli za upasuaji mbao wanadai fedha zao zaidi ya
shilingi milioni 20 kwa kazi ya upasuaji walioufanya huku wakifafanua kuwa hata
fedha hizo zilizopatikana shilingi milioni 196 baada ya mavuno kufanyika mpaka
sasa hazijulikani zipo wapi.
Pia afisa misitu huyo, David Hyera alipotakiwa
kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo alionekana kutoa taarifa ambazo zinapishana
na maelezo yaliyonukuliwa kwenye makabrasha ya vikao vya madiwani hao ambapo baadaye
aliamrishwa akae chini na kuzuiwa asiongee chochote kutokana na takwimu zake
alizokuwa akizitoa mbele ya baraza hilo kutoendana sawa na makubaliano ya vikao
husika.
Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya
mipango miji na mazingira, Leonard Mshunju naye alithibitisha mbele ya baraza
hilo la Madiwani huku akifafanua kuwa licha ya kutoa maazimio ambayo hata
wafanyakazi waliofanya kazi ya uvunaji wa msitu ule wanapaswa kulipwa fedha zao
lakini hakuna kilichotekelezwa mpaka sasa.
Mshunju alibainisha kuwa ni kweli
kamati hiyo ilizuiwa kwenda kukagua msitu wa Mbambi kabla kazi ya uvunaji haijaanza
kufanyika na kwamba licha ya kuomba wakaangalie nini kinachofanyika kule
walizuiwa na hali hiyo alieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu
husika za baraza hilo.
Alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya
tuhuma hizo naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga Robert
Mageni alisema, “mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati nayakubali ni kweli
tuliwasilisha bajeti ya kupasua mbao zenye thamani ya shilingi milioni 325 lakini
suala la kukaidi kamati kuizuia kuipeleka kule msituni sio la kweli ila kule msituni
hata mimi binafsi nakumbuka nilishawahi kwenda baada ya kupata fununu kwamba
kuna mabaya yanafanyika”.
Hata hivyo kwa upande wake Mwenyekiti
wa baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo, Ndunguru Kipwele aliunga mkono
hoja zilizotolewa na Madiwani hao na kueleza kuwa kuna kila sababu ya suala
hilo kuunda Kamati maalumu, ambayo itafanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo kwa
muda wa mwezi mmoja na baadaye litaitwa baraza la dharula kwa ajili ya kutolea
ufafanuzi juu ya majibu ya uchunguzi walioufanya.
No comments:
Post a Comment