Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia,
wazee na watoto Dokta Khamis Kigwangala amemjia juu Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Robert Mageni kutokana na kushindwa
kutekeleza maagizo ya serikali ya kila kituo cha afya ni lazima ufanyike ujenzi
wa jengo la upasuaji na utoaji wa huduma za maabara.
Dokta Kigwangala alifikia hatua hiyo juzi akiwa katika ziara
yake ya kikazi baada ya kubaini kwamba haujafanyika ujenzi huo katika kituo cha
afya cha Said Kalembo kilichopo kata ya Kihungu kwenye halmashauri hiyo, ili
kuweza kuanzisha huduma ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni kwa mama mjamzito
pamoja na huduma za maabara kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
“Viongozi wazembe namna hii ndiyo mnaotuongezea vifo vya
akina mama wajawazito kwa sababu hamtimizi wajibu wenu ipasavyo na msipotimiza
wajibu maana yake inabidi mchukuliwe hatua hakuna chochote mnachokifanya mna
vituo vya afya vimechoka hamfanyi ukarabati,
“Sera ya afya ipo wazi inasema vituo vyote vya afya hapa
nchini vitapata usajili wa kuwa kituo cha afya endapo tu kama kutakuwa
inatolewa huduma ya upasuaji na uchunguzi wa magonjwa ya maabara, hapa misingi
ya uendeshaji wa kituo cha afya haifuatwi”, alisema Dokta Kigwangala.
Naibu Waziri huyo alifikia hatua pia ya kutaka kukishusha
hadhi kituo hicho cha afya kutokana na tokea kijengwe miaka mingi iliyopita hakijakidhi
vigezo husika na kwamba aliongeza kuwa kuna timu yake ya wataalamu ambayo
inazunguka nchi nzima kufanya tathimini vituo vyote vya afya ambapo kama
watakuta kuna kituo hakijatimiza matakwa yaliyotolewa na serikali viongozi wote
wazembe watawajibishwa.
Alisema kuwa ameshangazwa na uongozi wa halmashauri ya mji wa
Mbinga licha ya kuwa na kituo kimoja cha afya lakini umeshindwa kutekeleza
maagizo hayo ya serikali tokea yalipotolewa miezi sita iliyopita, ikiwemo hata
kukifanyia ukarabati kituo hicho hivyo serikali itahakikisha wale wote ambao
walipaswa kutekeleza agizo hilo na hakuna kilichofanyika watendaji husika
watawajibika.
“Wakati Rais Dokta John Magufuli anawapatia majukumu mlipaswa
kuyatekeleza lakini hamna mlichotekeleza mmebaki kukaa tu na kupuuza mimi kabla
sijatumbuliwa nitawatumbua ninyi kwanza, nitahakikisha nimewatoa wa chini yangu
kwa sababu inaonesha hamtilii maanani maagizo ya serikali ikiwemo hata hiki
kituo kimoja cha afya mlichokuwa nacho kinawashinda”, alihoji Dokta Kigwangala.
Alifafanua kuwa viongozi waliopewa dhamana na serikali
wanapaswa kumsaidia Rais Dokta Magufuli kwa kufanya kazi zao kwa bidii katika
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wananchi.
Vilevile aliongeza kuwa sera ya afya inawataka viongozi
waliopo katika ngazi ya halmashauri kusimamia majukumu yote ikiwemo kufanya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya sekta hiyo ili serikali
inapofanya ufuatiliaji wake ikute utekelezaji husika umekwisha fanyika na sio
kuiachia Wizara afya pekee.
Hata hivyo wakati wa kuhitimisha ziara hiyo ya Dokta Kigwangala kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye naye alisema kuwa atahakikisha anaendelea kusimamia maagizo hayo yaliyotolewa na serikali ikiwemo kuwabana watumishi wake wa ngazi ya chini ili waweze kuwajibika ipasavyo.
Hata hivyo wakati wa kuhitimisha ziara hiyo ya Dokta Kigwangala kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye naye alisema kuwa atahakikisha anaendelea kusimamia maagizo hayo yaliyotolewa na serikali ikiwemo kuwabana watumishi wake wa ngazi ya chini ili waweze kuwajibika ipasavyo.
No comments:
Post a Comment