Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwa katika Mahakama ya mkoa wa Ruvuma jana, ambapo wamesomewa mashtaka mawili na kupelekwa Mahabusu ya gereza Songea mjini. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
VIONGOZI tisa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Katibu
Mkuu wa chama hicho Dokta Vicent Mashinji wamefikishwa katika Mahakama
ya Hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Ruvuma, kujibu mashtaka mawili yanayowakabili
na baadaye wamepelekwa katika gereza la Mahabusu Songea mjini huku
kukiwa kumegubikwa na hali ya utata.
Aidha viongozi hao wamefikishwa Mahakamani hapo jana
majira ya asubuhi na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa serikali
mwandamizi mkoani hapa, Renatus Mkude ambaye alikuwa akisaidiwa na
Wakili wa serikali Shaban Mwigole mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya
mkoa huo, Simon Kobelo.
Wakili Mkude aliwataja Mahakamani hapo washitakiwa hao
kuwa ni Dokta Vicent Mashinji ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA taifa, Cecil
Mwambe Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya kusini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la
Ndanda Mtwara, Philberth Ngatunga Katibu wa CHADEMA Kanda ya kusini, Irineus
Ngwatura Mwenyekiti CHADEMA mkoa wa Ruvuma pamoja na Delphin Gazia Katibu wa CHADEMA
mkoa wa Ruvuma.
Wengine ni Zubeda Sakuru Mbunge wa Viti
maalum mkoa wa Ruvuma, Sanguru Manawa Katibu wa Oganaizesheni na mafunzo,
Curthberth Ngwata Mwenyekiti CHADEMA wilaya ya Nyasa ambaye pia ni Diwani wa
kata ya Kipingu wilayani humo pamoja na Charles Makunguru Katibu mwenezi wilaya
ya Nyasa.
Mkude alidai Mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote kwa
pamoja wanakabiliwa na makosa mawili ambayo ni kosa la kwanza wote kwa pamoja
wakiwa wilayani Nyasa tarehe isiyofahamika walikula njama ya kutenda kosa ambalo
lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani ndani ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Alilitaja kosa la pili kwamba wanadaiwa kuwa mnamo Julai
15 mwaka huu katika eneo la mji wa Mbambabay washitakiwa wote kwa pamoja
walifanya mkusanyiko usio wa halali ambao ungepelekea kusababisha uvunjifu wa
amani katika jamii.
Vilevile aliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi
hiyo unaendelea na aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa na
kwamba washtakiwa wote wamekana mashitaka yote mawili na wamerudishwa mahabusu
katika gereza la Songea mjini.
Kwa upande wake Hakimu Kobelo alisema kuwa dhamana ya washitakiwa
ipo wazi hivyo kila mshtakiwa anapaswa kuwa na wadhamini ambao ni wakazi wa
Songea mjini ambao wanatakiwa wapeleke uthibitisho toka kwa Maafisa watendaji
wa mitaa wanayoishi mjini hapa, pia wadhamini hao wanatakiwa kudhaminiwa kwa shilingi
milioni mbili ya maneno.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 20 mwaka
huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa tena ambapo pia mara baada ya
Mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo na kuwataka mawakili wa upande wa
utetezi ambao ni Edson Mbogoro, Eliseus Ndunguru wote
wa Songea pamoja na mawakili wasomi waandamizi Barnabas Pomboma toka
Mbeya.
WAkati mawakili hao wakishughulikia masuala ya dhamana
za wateja wao Hakimu huyo alitoka na kudaiwa amekwenda Mahakama kuu kanda ya
Songea ambapo mawakili hao walimsubiri kwa muda mrefu na alipofika ilionekana
wakili wa serikali naye alitoka huku akiaga anatoka kwa muda na atarejea ili aweze
kusaini hati hizo za dhamana, lakini hakuweza kutokea na baada ya kupigiwa simu
yake ya mkononi ilikuwa imezimwa hakuweza kupatikana.
Kwa upande wake wakili msomi Edson Mbogoro aliwaeleza waandishi
wa habari kuwa viongozi hao wamefunguliwa kesi ya Jinai namba 173
ya mwaka 2017 wao walikwenda kumuona Hakimu ili aweze
kuthibitisha dhamana za wateja wake lakini cha ajabu hadi muda wa kazi wa Mahakama
unakwisha Hakimu hakuweza kutokea mahakamani hapo hivyo wanasubiri kesho waweze
kuzungumza na Hakimu huyo ili awaeleze nani aliyetoa hati ya wateja
wao kupelekwa mahabusu.
Pia Mbogoro alilalamikia kitendo cha watu 12 tu
kuruhusiwa kuingia mahakamani na wengine kuzuiwa ambao walikuja mahakamani hapo
kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Naye Wakili msomi Eliseus Nduguru amelalamikia wateja
wake kutoroshwa katika mazingira ya kutatanisha na kupelekwa mahabusu bila
kufuata taratibu ambapo hakuweza kuyaelewa mazingira hayo waliyoyafanya
walikuwa na nia gani kwani yeye na mawakili wenzake walikuwa wakishugulikia
dhamana ambapo alisema kuwa kuna mchezo mchafu ambao ukiendelea kuachwa ipo
siku utaweza kuleta madhara kwa wengine.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana taifa
(BAVICHA ) Patrick Ole Sosopi ameitaka Mahakama kutenda haki na siyo
kufanya mambo tofauti na sheria inavyotaka, pia Jeshi la Polisi lifanye kazi
kwa weledi na pia limeonyesha wazi kuvunja sheria za nchi tangu
mwanzo kwa sababu waliwazuia wananchi wengine waliofika Mahakamani kusikiliza
kesi hiyo pale walipotaka kuingia ndani ya Mahakama na badala yake waliruhusiwa
watu 12 tu.
No comments:
Post a Comment