Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka
Wakurugenzi na Maafisa elimu Sekondari wa Halmashauri za wilaya mkoani humo,
wahakikishe kwamba fedha zilizotolewa na serikali shilingi bilioni 2.6 kwa
ajili ya shughuli ya ukarabati wa majengo ya maabara kwa shule hizo zinafanya
kazi husika na sio vinginevyo.
Dokta Mahenge alitoa agizo hilo kwa kile alichoeleza kuwa
anazotaarifa kwamba baadhi ya shule ambazo zimepelekewa fedha tokea mwezi Machi
mwaka huu, kwa ajili ya kukarabati majengo ya kusomea wanafunzi wa kidato cha
tano na sita pamoja na majengo ya maabara hakuna kazi zilizofanyika mpaka sasa.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa mkoa wakati alipofanya
ziara yake ya kushitukiza katika wilaya ya Mbinga mkoani hapa, kwa lengo la
kukagua ukarabati wa majengo ya shule ya sekondari Ruanda iliyopo katika kata
ya Ruanda wilayani humo ambayo serikali imetoa shilingi milioni 259 kwa ajili
ya kuweza kukamilisha kazi hiyo.
Aidha Dokta Mahenge alisikitishwa na kasi ya ukarabati wa
majengo ya shule hiyo ambapo alieleza kuwa licha ya kupewa fedha hizo, hakuna
kazi iliyofanyika na hilo lilitokana na viongozi husika kukaa muda mwingi
ofisini bila kwenda kukagua maendeleo ya kazi hiyo.
“Ni lazima tunavyokuwa tumepanga mipango tunapaswa
kukamilisha kwa wakati kama utekelezaji hakuna hapa hatuelewani, fedha hizi
ziliingizwa kwenye akaunti ya shule hii muda mrefu lakini hakuna kazi
iliyofanyika mnataka niwafanye nini?”, alihoji Dokta Mahenge.
Kwa upande wake alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali
hiyo Afisa elimu wa shule za sekondari wilaya ya Mbinga, Joseph Kapere alisema
kuwa ucheleweshaji huo wa ukarabati wa majengo hayo umetokana na miongozo
husika ilichelewa kuwafikia ili waweze kufanya kazi hiyo.
Kapere aliongeza kuwa kutokana na kuchelewa kwa miongozo hiyo
hawakuweza kufanya hata miamala ya fedha ambazo wangezitoa kwenye akaunti ya
shule hiyo na kuweza kuanza kumlipa mkandarasi husika ili aweze kufanya kazi.
Hata hivyo kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta
Mahenge alitoa mwezi mmoja kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga
wahakikishe kwamba ukarabati wa majengo kwa shule ya sekondari Ruanda unakamilika
haraka iwezekanavyo na kwa viwango vinavyotakiwa na endapo usipofanyika hivyo hatua
kali zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment