Na Muhidin Amri,
Madaba.
KITUO cha utafiti wa Sayansi tiba asili kinachofahamika kwa
jina maarufu la The King Solomon of Sanitarium, ambacho kinajishughulisha na
upimaji wa afya za binadamu na kutibu magonjwa mbalimbali katika wilaya ya
Madaba mkoani Ruvuma, kimefungwa kisiendelee kutoa huduma hizo hadi pale
Wataalamu wa afya watakapojiridhisha na uhalali wa uwepo wake wilayani humo.
Aidha hatua ya kukifunga huko imetekelezwa juzi na Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Shafi Mpenda baada ya kubaini mapungufu
husika ikiwemo kutokuwepo kwa vibali halali vinavyoruhusu kituo hicho kufanya
kazi hizo.
Mbali na hayo Mpenda alisema kuwa atawachukulia pia hatua
kali baadhi ya wataalamu wake wa idara ya afya, ambao wanadaiwa kushiriki kutoa
vibali feki vilivyoruhusu kituo hicho kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mmiliki wa
kituo cha The King Solomon of Sanitarium, Seleman Nzaganya amekuwa akifanya
shughuli zake kinyume na taratibu ambapo hata leseni kutoka Baraza la tiba asili
imekwisha muda wake tangu ilipofika mwezi Januari mwaka huu na kwamba, amekuwa
akiendelea kufanya shughuli za upimaji wa afya za binadamu bila kuwa na leseni
mpya jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
“Nimelazimika kukifunga kituo hiki ili kuweza kuokoa maisha
ya wananchi kwani inaonesha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa mtindo wa kutapeli
wananchi kwa sababu hata mtu tuliyemkuta akihudumia wagonjwa, hana taaluma
yoyote ile inayomwezesha kutoa huduma jambo ambalo ni hatari kwa afya ya
binadamu”, alisema Mpenda.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa hii ni mara ya
pili kufunga kituo kama hicho na kwamba ni kampeni endelevu kwa wale
wote wanaowatapeli wananchi wa wilaya ya Madaba, huku akitoa onyo kali kwa watu
wengine wenye tabia kama hiyo kuacha mara moja na watafute maeneo mengine ya
kufanya shughuli zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotaja
majina yao ambao ni wakazi wa wilaya hiyo walipongeza hatua hiyo iliyochukuliwa
na serikali ambayo inalenga kuokoa maisha ya watu wake.
Walisema kituo hicho kilikuwa sehemu ya tatizo kwani hata
wananchi waliokuwa wakienda hapo kwa ajili ya kupata ushauri na matibabu, wamekuwa
wakiamini kwamba watapata suluhu ya matatizo yao kumbe wamekuwa wakizidisha
ukubwa wa matizo waliyonayo.
Kwa upande wake akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa kituo
hicho, mtu mmoja aliyekutwa akitoa huduma katika kituo hicho Ezakiel
Mwakatumbula alipohojiwa na mwandishi wetu alisema kuwa wamekuwa wakitoa huduma
za matibabu kwa magonjwa mbalimbali hasa magonjwa sugu kwa kutumia dawa za
mimea, chakula na matunda.
Hata hivyo alikanusha kufanya shughuli zao kitapeli huku akisisitiza
kwamba, huduma wanazotoa zimekuwa zikiwasaidia wananchi wengi katika kuokoa
maisha yao pale wanapougua.
No comments:
Post a Comment