Na Muhidin Amri,
Songea.
Songea.
WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wametakiwa kuondoa woga katika utendaji wa kazi zao za kila siku badala yake wameshauriwa kufanya shughuli zao kwa kujiamini na kufuata maadili yao ya kazi, kwa kuzingatia taratibu husika ikiwemo kuepuka kuandika habari za uongo au za kupika.
Cresencia Kapinga. |
Mwito umetolewa jana na diwani wa kata ya Ndilimalitembo Manispaa
ya Songea mkoani humo, Cresencia Kapinga wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi
wa habari hizi mjini hapa kuhusiana na mwelekeo na mchango wa vyombo vya habari
katika kuleta maendeleo hapa nchini.
Kapinga alisema kuwa mwandishi mzuri wa habari ni yule ambaye
anaandika habari zenye kuleta tija katika jamii na kuibua maovu yanayofanywa
na baadhi ya watendaji wa taasisi, idara, mashirika ya umma na jamii kwa jumla
dhidi ya vitendo vya rushwa, wizi na hata ukatili na unyanyasaji wa watoto na
wanawake.
Mbali na diwani huyo kuwataka kufichua maovu yanayotokea katika
jamii lakini pia amewaasa kuacha tabia ya kuandika habari zenye mrengo wa
kushoto ambazo huchafua majina ya watu bila sababu yoyte ile ya msingi au kuwakwaza
watu wengine katika jamii kwa misingi ya chuki zimepitwa na wakati kwa kile
alichoeleza kuwa haziwezi kuleta tija na mafanikio katika taifa letu.
Alisema kwa kuwataka wanahabari mkoani humo kuacha tabia ya
kuandika habari nyepesi kama vile za Polisi, Mahakamani na zile za viongozi
kwani nyingi wananchi wamezichoka kutokana na muda mwingi zinalenga kumjenga
mtu na haziibui matatizo ya wananchi kama vile za uchunguzi ambazo hasa hulenga
kuibua matatizo ya jamii vijijini.
“Aina ya uandishi wa sasa hakuna jambo la maana linaloweza
kuibadili jamii yetu kifikra kwani ninyi waandishi wa habari mara kwa mara
mmekuwa vibaraka wa watu wengi wenye uwezo kifedha, kwa kuwasemea mambo yao na
mmejisahau hata kukumbuka majukumu yenu ya msingi yatakayoliletea tija taifa
kwa kuibua matatizo ya wananchi”, alisema Kapinga.
Alifafanua kuwa licha ya heshima ambayo wamekuwa wakiipata wanahabari
kwa jamii hata hivyo heshima hiyo hivi sasa haikustahili kwenda kwao kwa sababu
ni muda mrefu jamii imeshindwa kupata kile wanachotarajia kutoka katika mchango
wa vyombo vya habari na ndiyo maana idadi kubwa ya vitendo vya ufisadi, unyanyasaji,
ubakaji kwa wanawake, watoto na dhuluma dhidi ya wanyonge vimekuwa vikiongezeka
kila kukicha licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuzuia au
kupambana navyo.
Pamoja na mambo mengine Kapinga ambaye kitaaluma ni Mwandishi
wa habari alitolea mfano katika mkoa wa Ruvuma ni kati ya maeneo yenye matukio
mengi ya unyanyasaji yakiwemo hasa yale ya wanawake kutelekezwa na waume zao,
lakini imekuwa nadra kusikia vitendo hivyo vinaandikwa kwenye vyombo vya habari
licha ya uwepo wa idadi kubwa ya waandishi wa habari ambao kama wangetimiza wajibu
wao vitendo hivyo vingepungua kama sio kwisha kabisa.
No comments:
Post a Comment