Na Muhidin Amri,
Songea.
SERIKALI imewaagiza Wakurugenzi watendaji katika Halmashauri
za wilaya, miji manispaa na majiji hapa nchini kutenga maeneo katika halmashauri
zao ili kuweza kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana na makundi mengine
yenye mahitaji maalumu ili yaweze kujiajiri na kufanya shughuli zao za
maendeleo.
Jenista Mhagama. |
Agizo hilo limetolewa jana mjini Songea mkoani Ruvuma na
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu sera, bunge, ajira, vijana na watu wenye
ulemavu Jenista Mhagama wakati alipokuwa akizindua awamu ya pili mpango wa
urasimishaji wa ujuzi (RPL) uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa
vijana 173 kutoka wilaya zote za mkoa huo.
Mhagama alisema kuwa serikali imekusudia kufikia nchi ya
viwanda na uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2020 hadi 2025 na kwamba mpango huo
hauwezi kufanikiwa endapo halmashauri za wilaya hazitaunga mkono juhudi
hizo za serikali kuu kwa kuwaandaa na kuwapatia vijana ujuzi, nyenzo
na maeneo ya kufanyia shughuli zao.
Alisema kuwa kutokana na mafunzo hayo serikali inaamini kwamba
watu wengi watapata ujuzi na kuwawezesha kuwa na sifa ya
kufanya kazi zilizorasmi na zisizo rasmi, kwani watakuwa wamepata ujuzi na
uzoefu utakaoweza kuharakisha kukua kwa uchumi wa Tanzania.
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amempongeza Mkuu wa mkoa
wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge kwa kile alichoeleza kuwa amekuwa na mipango
mingi ya maendeleo ambayo inalenga kuharakisha kukua kwa maendeleo ya mkoa huo na
kujali makundi mengine ya kijamii hususan kwa yale yenye mahitaji maalumu.
Alibainisha kuwa ni hatua nzuri sasa kuona serikali ya mkoa huo
chini ya Dokta Mahenge imewatafutia mradi wa kuku wa nyama kikundi cha watu
wenye ulemavu wa ngozi (Albino) katika Manispaa ya Songea mkoani humo huku
akiitaka mikoa mingine kuiga utendaji kazi wa Dokta Mahenge kwa kutafuta vyanzo
vya mapato na kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi wao na sio kuisubiri
serikali peke yake itekeleze maendeleo ya wananchi.
Aidha katika hatua nyingine ametoa mwezi mmoja kwa Kaimu Mkurugenzi
msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu Robert
Masatu kuandaa andiko ambalo litawezesha kupata fedha kwa ajili ya kuunda
kiwanda kidogo cha kutengeneza chakula cha kuku kwa ajili ya kikundi cha watu
hao wenye ulemavu wa ngozi waliopo mjini hapa.
“Mkurugenzi nakuagiza juu ya jambo hili analofanya Mkuu wa
mkoa huu sio kazi yake bali ni jukumu la sisi Wizara husika, nakupatia mwezi
mmoja wewe shirikiana na watendaji wengine kuandaa andiko litakalosaidia
kupata fedha za kuunda kiwanda cha kutengeneza chakula cha kuku hawa kwa ajili
ya kuunga mkono juhudi hizi zinazofanywa hapa”, alisisitiza Mhagama.
Awali Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge
amempongeza Rais Dokta John Magufuli kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi
zake ikiwemo ya kuzalisha ajira kwa wingi kwa vijana hapa nchini.
Dokta Mahenge alisema kuwa nchi kubwa duniani ikiwemo
Ujerumani imepiga hatua kubwa ya kiuchumi baada ya kuwekeza nguvu kubwa katika
ujenzi wa kazi za mikono na kuiomba serikali kupitia ofisi ya Waziri
Mkuu sera, bunge, ajira, vijana na wenye ulemavu kusaidia mpango maalumu
wa kilimo ujulikanao kwa jina la Green House, ambao uliibuliwa na serikali ya
mkoa wenye lengo la kuinua shughuli za kilimo cha matunda na mboga mboga.
Pia Mkuu huyo wa mkoa huo alieleza kuwa tayari serikali
imetoa fedha kwa kikundi cha watu hao wenye matatizo ya ngozi katika Manispaa
ya Songea kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji kuku wa nyama, katika eneo la
nane nane lililopo mjini hapa ambapo mradi huo utawawezesha kuongeza kipato chao
na kuboresha lishe.
No comments:
Post a Comment