Na Muhidin Amri,
Madaba.
WAZAZI na walezi katika Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani
Ruvuma, wameaswa kutambua wajibu wa malezi kwa watoto wao ikiwemo
kuzingatia uzazi wa mpango, ili kuweza kuepuka kuwa na idadi ya watoto
wengi katika familia zao ambao ni mzigo mkubwa kutokana na hivi sasa kupanda
kwa gharama ya maisha.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa endapo watazingatia ipasavyo
itawezesha watoto watakaozaliwa kupata haki yao ya msingi kama vile elimu, chakula,
mavazi na kumudu gharama ya matibabu jambo ambalo litachangia kuwa na familia
bora na yenye afya nzuri.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani
humo, Shafi Mpenda alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wazazi na walezi
katika kituo cha afya Madaba ambao walikuwa kituoni hapo kwa ajili ya kupata
huduma mbalimbali za matibabu.
Alisema kuwa baadhi ya wazazi hawana utaratibu na mazoea ya kuchagua
idadi ya watoto wa kuzaa ambao wataweza kumudu gharama za malezi yao na badala
yake kutokana na tamaa za mwili hujikuta wakiwa na idadi kubwa ya watoto ambapo
baadaye hushindwa kuwapatia huduma muhimu hivyo kuongezeka kwa idadi kubwa ya
watoto katika familia na huishia kuzurula mitaani.
Mpenda alieleza kuwa ni vizuri sasa wakati umefika kwa Watanzania
hususan kwa wakazi wa Madaba kuchagua idadi ya watoto wa kuzaa kwa
kupanga aina ya maisha unayotaka badala ya kuishi maisha ya ufahari na sifa
jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma maisha na ndoto ya kuwa na maendeleo.
Aliongeza kuwa kutokana na aina ya maisha wanayoishi baadhi
ya wakazi wa wilaya hiyo ya Madaba ni vigumu pia kupata hata viongozi bora
kwani hata wale waliopo huko vyuoni ambao wanategemewa kuwa viongozi wa kesho
tayari wameanza kujiingiza katika vitendo vya mambo ya anasa ambavyo kwa kiasi
kikubwa yamekuwa hayaendani na maadili na tamaduni zao.
“Ni jambo la kusikitisha kuona idadi kubwa ya wasichana
kuanzia miaka 16 hadi 18 wanapata ujauzito mapema wakiwa bado shuleni, mimba
katika kundi hili zinazidi kuongezeka kila kukicha huku wazazi na jamii ikiendelea
kufumbia macho vitendo hivi bila kuchukua hatua juu ya namna ya kudhibiti”,
alisema.
Kwa mujibu wa Mpenda alisema kutokana na tatizo hilo kuwa
sugu ndiyo maana idadi ya vitendo vya kutupa watoto pindi wanapozaliwa vinazidi
navyo kushamiri siku hadi siku huku akiiomba jamii kushirikiana na vyombo
husika kama idara ya ustawi wa jamii na Polisi kupambana navyo kwa kuwabana
watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani vimekuwa vikiliaibisha taifa.
No comments:
Post a Comment