Na Mwandishi wetu,
UMMY Mwalimu ambaye ni Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia,
wazee na watoto amesema kwamba kiu yake kubwa katika sekta ya afya anataka
kuona kila Mtanzania katika maisha yake anamiliki bima ya afya.
Hayo yalisemwa leo na Waziri huyo wakati alipokuwa kwenye uzinduzi
wa kadi ya bima ya afya katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dara es Salaam kwa mtoto yenye jina maarufu
“Toto Kadi” ambapo alisema kuwa ili taifa liweze kuwa na maendeleo itatokana na
kuwa na misingi bora ya afya.
Alifafanua kuwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ni
lazima pia kuwa na msingi mzuri wenye watoto wanaopata huduma bora za afya.
Vilevile alieleza kuwa kuwepo kwa bima hiyo na watoto kuweza
kupata matibabu ya uhakika, kutaifanya familia kuwa na furaha wakati wote hasa
pale panapotokea ugonjwa fulani ambapo bima hiyo ndiyo itaweza kumaliza
matatizo hayo.
“Wakati naingia madarakani nilikutana na Rais Dokta John
Pombe Magufuli tuliweza kuondoa gharama za upatikanaji wa bima na msingi wetu
mkubwa ulikuwa ukilenga jinsi ya kusaidia Watanzania kuwa na bima itakayoweza
kuwasaidia wapate matibabu kwa urahisi”, alisema.
Pia Waziri huyo aliuomba Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF)
kuunda mfumo wa bima ya mama mjamzito ambayo mama huyo ataweza kuitumia wakati
wa ujauzito wake na baada ya kujifungua.
Ummy aliongeza kuwa kampeni hiyo inapaswa kuwa endelevu kwa
nchi nzima ili watoto wote waweze kuwa na bima ya afya ili kuweza kujenga taifa
lenye afya bora, huku akiutaka mfuko huo kubandika mabango kwenye kumbi za
starehe ambapo wanaotumia vinywaji wataweza kuona kama watoto wao wana kadi ya
bima ya afya.
Hata hivyo naye Mwenyekiti wa bodi ya NHIF, Anne Makinda alisema
kuwa watahakikisha utekelezaji unafanyika mapema ikiwemo kila Mtanzania anapata
huduma za afya kwa mfumo wa bima ya afya.
No comments:
Post a Comment