Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
DOKTA Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma amewahimiza
Wananchi wa mkoa huo, kuwa na tabia yenye mazoea ya kutembelea vivutio mbalimbali
vya utalii vilivyopo mkoani humo badala ya kuwaacha wageni peke yao wakitumia
fursa hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, huku akisisitiza kwamba ndani
ya mkoa huo kumekuwa na vivutio vingi ambavyo vikitumika vyema vitasaidia
kukuza pato la mkoa na maendeleo ya wananchi wake.
“Vivutio hivi vikitumika ipasavyo vitaufanya hata mkoa wetu kupata
wageni ambao watachangia kukua kwa uchumi na pato la serikali na pia naviomba
vyombo vya habari hakikisheni mnatangaza fursa hizi kama vile mbuga ya Selou,
Ziwa Nyasa, Jiwe la Mbuji lililopo Mbinga ambalo linatajwa kuwa ndiyo refu
kuliko yote hapa nchini na vivutio vingine tulivyonavyo”, alisisitiza Dokta
Mahenge.
Dokta Mahenge aliongeza kuwa juhudi zinaendelea kwa serikali
ya mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo vinakuwa katika mazingira
rafiki ya kufikiwa na watu kutoka maeneo mbalimbali, tofauti na sasa ambapo
baadhi ya maeneo hayo hayafikiki kwa urahisi kutokana na miundombinu yake kama
vile barabara kuwa mibovu.
No comments:
Post a Comment