Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa
Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda amepongeza jitihada zinazoendelea kufanyika
na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, juu ya ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhia maji na miundombinu mingine ya
kusambaza maji katika mji huo.
Aidha pamoja
na ujenzi huo unaendelea kufanyika pia uchimbaji wa mitaro nayo inajengwa kwa
ajili ya kuweza kufukia mabomba makubwa yatakayoleta maji kwa wingi zaidi
katika mji wa Mbinga.
Mapunda
alitoa pongezi hizo jana wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kutembelea mradi
huo, ambao tanki hilo linajengwa katika chanzo cha maji kilichopo kwenye milima
ya Lupembe iliyopo katika kijiji cha Tukuzi kata ya Luwaita.
Vilevile
Mbunge huyo anaeleza kuwa katika kuendeleza na kuboresha mradi huo anaishukuru
Serikali, kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji kutenga shilingi Bilioni 1
katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ambazo zitawezesha kupanua bomba kuu la
uzalishaji maji hivyo kumudu ongezeko kubwa la mahitaji ya maji kufika katika
eneo la mji huo.
“Katika kupambana
na tatizo hili ndio maana Wizara ya maji na umwagiliaji kwa kushirikiana na
Mamlaka hii, imeanza sasa kuboresha miundombinu ambayo ni chakavu ili kuweza
kuondokana na changamoto hii ambayo imedumu kwa miaka mingi sasa”, alisema
Mapunda.
Kwa upande wake
naye Meneja wa MBIUWASA, Patrick Ndunguru alipohojiwa na mwandishi wa habari
hizi alifafanua kuwa changamoto kubwa waliyonayo sasa ni uchakavu wa
miundombinu ya kuleta maji hayo kutoka kwenye chanzo cha Ndengu hadi Mbinga
mjini, ambapo miundombinu yake ni ya zamani imejengwa mwaka 1970 hivyo imekuwa
ikisababisha upotevu mkubwa wa maji ambayo yanapaswa kuwafikia walaji.
Ndunguru alisema
kuwa hayo yote yanatokana na uwezo mdogo wa uzalishaji maji unaosababishwa na
kupanuka kwa mji na kwamba mradi huo unahitaji kupanuliwa miundombinu hiyo
haraka, kwani uzalishaji uliopo sasa ni mita za ujazo 2,100 kwa siku
ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayohitajika ni mita za ujazo 5,248.
“Wizara
imekuwa ikitupatia fedha za ujenzi wa mradi huu kwa awamu kwa lengo la kuweza
kukamilisha ujenzi ambao tumeanza kuujenga, hapa lengo kuu ni kuongeza uwingi
wa maji, katika mwaka 2017 hadi 2018 malengo yetu pia ni kujenga machujio
ambayo kazi yake kubwa yatakuwa ni kutibu maji kabla hayajasafirishwa kwenda
kwa watumiaji”, alisema Ndunguru.
Kadhalika aliongeza
kuwa mradi huo unalenga pia kupanua huduma kwa kuyafikisha maji katika maeneo
mengine ya mji wa Mbinga ambayo hayajafikiwa na huduma, ambapo ujenzi wake
utakuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na kiasi cha fedha watakachokuwa
wanapata hivyo aliiomba serikali kupitia wizara husika iendelee kutoa fedha za ujenzi
wa miundombinu hiyo ili mradi uweze kukamilika ujenzi wake kwa wakati.
No comments:
Post a Comment