Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA kudaiwa kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za mapato
yatokanayo na uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe
Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani
humo Cosmas Nshenye naye ameapa akisema kuwa Ofisi yake itachukua hatua kali za
kisheria ikiwemo kulifanyia uchunguzi jambo hilo na kulifikisha kwenye vyombo
husika vya kisheria.
Nshenye alisema yeye binafsi hakubaliani na hali hiyo kwani
dhahiri inaonesha kuwa kumekuwa na vitendo viovu ambavyo vinatia shaka juu ya
mwenendo wa uvunaji wa msitu huo kwani ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu
husika bila kufuata miongozo ya serikali umefanyika.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisema hayo juzi alipokuwa
akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo
kilichofanyika mjini hapa, baada ya kuibuka hoja ya kumtuhumu Afisa misitu wa
mji huo David Hyera kuwa anadaiwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika
ubadhirifu wa mapato hayo.
“Mimi nilitarajia mtaalamu huyu wa misitu atatuambia ni kwa
nini mbao nyingi zimetumika kwenye taasisi binafsi, hapa anatuletea taarifa
ambayo haina ukweli juu ya uvunaji wa msitu huu badala yake anatumia mbinu za
kusahisha mbele ya baraza hili, hii itakuwa ni taarifa ya uongo,
“Kwa sababu taarifa hii haijakaa vizuri nafikiri tungefikia
maamuzi mimi nilazima suala hili nikalifanyie kazi kwanza zile shughuli za
uvunaji mbao kule mlimani kuanzia sasa zisimame kwa maana ya kupisha uchunguzi
ufanyike”, alisema Nshenye.
Katika hatua nyingine hata hivyo afisa huyo alisimamishwa
kazi mbele ya baraza hilo ili aweze kupisha uchunguzi baada ya Madiwani hao
kukubaliana kwamba iundwe Kamati maalumu itakayofanya kazi kwa kipindi cha
mwezi mmoja kuchunguza tatizo hilo.
Nshenye aliwataka pia halmashauri wafanye uchunguzi wao peke
yao na yeye ofisi yake itafanya uchunguzi wake binafsi na hatimaye endapo
kutakuwa na ukweli juu ya jambo hilo wahusika watakaopatikana watafikishwa
kwenye mkono wa sheria yaani Mahakamani ili kuweza kujibu tuhuma
zinazowakabili.
“Niwaombe halmashauri mtengeneze timu ya kwenu ya uchunguzi
na mimi nitengeneze timu ya kwangu, ili niweze kujua nawasilisha wapi na ninyi
halmashauri mtajua mnawasilisha wapi”, alisema.
Vilevile kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini
Sixtus Mapunda akichangia hoja katika kikao cha baraza hilo aliunga mkono
mawazo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye huku akieleza kuwa
kamati hiyo itakayoundwa inapaswa kuitwa kamati maalumu ambayo itajumuisha
wataalamu wa kutoka katika sekta mbalimbali ikiwemo mwanasheria wa halmashauri
hiyo.
Pamoja na mambo mengine, ilielezwa kuwa makisio ya awali
baada ya kufanyika upembuzi yakinifu na mtaalamu huyo wa misitu na kuwasilishwa
katika kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi Oktoba 12 mwaka jana, yalikuwa
zipatikane zaidi ya shilingi milioni 325 ambazo ni baada ya uvunaji wa mbao
katika msitu wa Mbambi kufanyika lakini walishangazwa kuelezwa kwamba
zimepatikana shilingi milioni 196 ndipo mgogoro huo uliibuka ndani ya baraza
hilo.
Naye Afisa misitu huyo, David Hyera alipotakiwa kutolea
ufafanuzi juu ya madai hayo alionekana kutoa taarifa ambazo zinapishana na
maelezo ya awali yaliyonukuliwa kwenye makabrasha ya vikao vya madiwani hao,
ambapo baadaye aliamrishwa akae chini na kuzuiwa asiongee chochote kutokana na
takwimu zake alizokuwa akizitoa mbele ya baraza hilo kutoendana sawa na
makubaliano ya vikao husika vilivyofanyika.
Mwenyekiti wa Kamati ya mipango miji na mazingira, Leonard
Mshunju naye alithibitisha mbele ya baraza hilo huku akibainisha kuwa licha ya
kutoa maazimio ambayo hata wafanyakazi waliofanya kazi ya uvunaji wa msitu ule
wanapaswa kulipwa fedha zao, lakini hakuna kilichotekelezwa ambapo mpaka sasa
bado wanadai zaidi ya shilingi milioni 20.
Mshunju alisema kuwa kamati yake ilizuiwa kwenda kukagua
msitu huo kabla kazi ya uvunaji haijaanza kufanyika na kwamba licha ya kuomba
wakaangalie nini kinachofanyika kule walikataliwa na hali hiyo alieleza kuwa ni
ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu husika za baraza hilo.
No comments:
Post a Comment