Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VIONGOZI ambao wamepewa dhamana na serikali ya kuongoza
Halmashauri za wilaya mkoani Ruvuma, wameonywa kuacha mara moja tabia ya kukaa
muda mwingi Ofisini badala yake watembelee na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ya wananchi vijijini ili iweze kujengwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Onyo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith
Mahenge wakati alipokuwa wilayani Mbinga katika ziara yake ya kukagua baadhi ya
miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya shule za sekondari wilayani humo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa umefika wakati sasa kwa kila
kiongozi aliyekuwa katika nafasi yake mkoani humo anapaswa kutekeleza ipasavyo
majukumu aliyopewa na serikali, ili kuweza kufikia malengo ya serikali ya awamu
ya tano hususan katika kukuza sekta ya elimu kwa faida ya kizazi cha sasa na
kile kijacho.
“Nimetembelea baadhi ya shule zetu za sekondari hapa Mbinga nahitaji
kuona kasi ya kusimamia ukarabati na ujenzi wa majengo ya shule hizi uwe mzuri,
natoa mwezi mmoja kuanzia sasa nitakapofika siku nyingine kukagua tena nikute kazi
zilizopangwa kufanyika ziwe zimetekelezwa ipasavyo, vinginevyo viongozi mliopewa
dhamana mjiandae kuwajibishwa na hili ni agizo la mkoa mzima”, alisisitiza
Dokta Mahenge.
Vilevile kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye akichangia hoja wakati wa kuhitimisha ziara hiyo alimweleza Mkuu wa
mkoa wa Ruvuma, Dokta Mahenge kwamba yeye na viongozi wenzake wilayani humo
watahakikisha wanazingatia maagizo hayo ikiwemo kusimamia vizuri miradi yote ya
wananchi iliyotengewa fedha na serikali ili iweze kutekelezwa kwa viwango
vinavyokubalika.
“Maswali yote yaliyoulizwa leo hapa yalitakiwa yajibiwe na
watu wa Ofisi ya mipango niwaombe badala ya kuwataka, Ofisi hii ijipange upya
kufanya ufuatiliaji na itoe taarifa kwa sababu inaonekana kuna mambo
yanafanyika kwa wananchi kule vijijini lakini hatuyafahamu”, alisema Nshenye.
Kwa ujumla mkoa wa Ruvuma hivi sasa una wilaya sita ambazo ni wilaya ya Songea, Mbinga, Tunduru, Namtumbo, Nyasa na
Madaba zikiwemo pamoja na Manispaa ya Songea na halmashauri ya mji wa
Mbinga.
No comments:
Post a Comment