Songea.
IMEELEZWA kuwa Watanzania na wananchi wa Msumbiji wametakiwa kuendelea
kudumisha uhusiano wao ambao uliasisiwa kwa muda mrefu na viongozi wa nchi
hizo mbili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Samora Machel, ikiwa
ndiyo hatua ya kuziwezesha nchi zao kupiga hatua kubwa ya kukuza uchumi na
maendeleo yao kwa ujumla.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko alisema
hayo jana mjini Songea wakati alipokuwa akifungua kikao cha kazi kwa wataalamu
na viongozi wa mikoa ya Tanzania na Msumbuji kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Hoteli ya Hunt Club iliyopo mjini hapa.
Bendeyeko alisema kuwa nchi hizo zimekuwa na uhusiano mzuri
kwa muda mrefu ambao wananchi wake wa pande hizo mbili wamekuwa wakishiriki kwa
pamoja katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii kama vile kilimo na
uvuvi.
“Nchi hizi mbili zimekuwa na uhusiano huu kwa muda mrefu sasa
tena wa damu ambao jamii wakati mwingine imekuwa ikiongea lugha moja
inayofanana”, alisema Bendeyeko.
Katika kikao hicho kwa upande wa Tanzania wataalamu walitoka mkoa
wa Ruvuma na Mtwara na upande wa Msumbuji mikoa iliyoshiriki ni Niassa na Cabo
Delegado ambapo Ruvuma jopo la wataalamu liliwakilishwa na Katibu tawala wa mkoa huo
Bendeyeko na upande wa Mtwara likiongozwa na Katibu tawala Alfred Luanda.
Vilevile kwa upande wa Serikali ya nchi ya Msumbiji, iliongozwa
na Jenerali Yusuph Omary pamoja na wataalamu wengine wa masuala
ya uchumi na kisiasa ambao kwa pamoja walijadili namna ya kuendelea kuimarisha
uhusino kwa nchi hizo.
Bendeyeko alifafanua kuwa mbali na wananchi kuongea lugha
inayofanana wamekuwa pia wakishirikiana kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa
pamoja wakitumia mto Ruvuma.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mecula nchini Msumbiji,
Almindo Alberto ametoa wito kwa Watanzania kudumisha uhusiano huo pamoja na kufanya
kazi mbalimbali nchini humo kwa kufuata sheria na taratibu husika.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kinafuatia baada ya kufanyika kikao cha mwaka 2006 kwa viongozi wa nchi hizo mbili na kujenga makubaliano ya kuunda ushirikiano endelevu kwa manufaa ya wananchi wake.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kinafuatia baada ya kufanyika kikao cha mwaka 2006 kwa viongozi wa nchi hizo mbili na kujenga makubaliano ya kuunda ushirikiano endelevu kwa manufaa ya wananchi wake.
No comments:
Post a Comment