Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa uzalishaji wa makaa ya mawe yanayochimbwa
katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, unakabiliwa na changamoto kubwa ya soko la kuuzia makaa
hayo kutokana na viwanda vinavyotumia nishati hiyo hapa nchini kupunguza kasi
ya ununuaji wa mkaa huo.
Aidha imefafanuliwa kuwa viwanda vya saruji ambavyo kwa kiasi
kikubwa vilikuwa vikitumia mkaa huo, hivi sasa vimekuwa vikinunua kiasi kidogo
cha mkaa jambo ambalo limekuwa likisababisha kuyumba kwa soko la ndani la
bidhaa hiyo.
Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa Kampuni ya Tancoal Energy,
Edward Mwanga baada ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge kutembelea
mgodi huo juzi kwa lengo la kutaka kujiridhisha juu ya hali ya uzalishaji wa
mkaa huo.
Mwanga alisema kuwa uzalishaji hivi sasa umekuwa mkubwa
ambapo kwa siku wamekuwa wakichimba tani 2,000 hadi 2,500 lakini changamoto
kubwa wanayokabiliana nayo ni wateja waliopo hapa nchini huyatumia makaa hayo
kwa kiasi kidogo tofauti na uzalishaji wanaoufanya.
“Hivi sasa uzalishaji tunaoufanya kinachotuyumbisha hapa ni
soko la kuyauza kwa ujumla uzalishaji wa mkaa umekuwa mkubwa hakuna tatizo, kwa
takwimu nilizonazo hapa ndani ya mwezi tumekuwa tukizalisha tani 60,000 na
kuendelea”, alisema Mwanga.
Alisema kuwa hapo awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
alipofanya ziara ya kutembelea mgodi huo aliwataka kuboresha mitambo na
kuongeza kasi ya uzalishaji wa mkaa, hivyo wameweza kutekeleza agizo la Waziri
huyo lakini kinachowayumbisha ni wapi kwa kwenda kuyauza makaa hayo kutokana na
soko la ndani kutokuwa na uwezo wa kuyanunua.
Hapo awali alieleza kuwa walikuwa wakizalisha tani 80 hadi
100,000 kwa mwezi lakini hivi sasa tatizo hilo halipo tena kutokana na kuongeza
mitambo hiyo ya uzalishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo, Dokta Mahenge mara baada ya
kushuhudia uzalishaji unaofanywa kwenye mgodi wa Ngaka, aliyaomba makampuni na
wawekezaji wenye viwanda mbalimbali hapa Tanzania kwenda kununua mkaa huo ili
waweze kuendeshea mitambo ya viwanda vyao kwani uzalishaji wa mkaa umekuwa
mkubwa tofauti na hapo awali.
“Niwaombe wawekezaji wetu wajitokeze kwa wingi kuja kununua
makaa haya ili tuweze kukuza soko letu la ndani, hivi sasa hakuna matatizo tena
ya uzalishaji wa mkaa katika mgodi huu”, alisema Dokta Mahenge.
No comments:
Post a Comment