Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA kuhamishwa kwa watumishi wa serikali kada ya afya
waliokuwa wakitoa huduma kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati
zilizokuwa chini ya mamlaka ya Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma uongozi
wa jimbo hilo unashindwa kuendelea kutoa huduma katika baadhi ya vituo vyake vya
afya na hatimaye huenda vikafungwa wakati wowote kuanzia sasa na wananchi
kukosa huduma husika.
Mwandishi wa habari hizi amebaini kuwa hata katika orodha ya
watumishi hao ambao nakala yake tunayo, waliohamishwa wapo pia Watawa (Masista)
kutoka mashirika mbalimbali katika jumuiya zao na kupelekwa kwenye vituo
ambavyo havina Kanisa jambo ambalo imeelezwa kuwa ni kinyume na taratibu zao.
Vilevile kufuatia hali hiyo kumekuwa na mkanganyiko mkubwa
kwa Wakuu wa mashirika ya jumuiya hizo na kuathiri kwa kiasi kikubwa huduma za
afya zinazotolewa na Jimbo hilo kutokana na watumishi wengi kuhamishwa.
Mratibu wa afya Jimbo Katoliki la
Mbinga, Padri Raphael Ndunguru alisema kuwa baadhi ya vituo hivi sasa wanapaswa
kuvifunga mara moja kutokana na kukosa watumishi wenye sifa ya kuhudumia
wagonjwa.
Alisema kuwa idara ya afya Jimbo Katoliki la Mbinga ambayo
imeshirikiana vizuri na serikali kwa miaka mingi, leo inashangaa kuondolewa kwa
watumishi hao wa serikali ambao walikuwa wameingia mikataba ya ubia baina yao na
vituo hivyo binafsi.
“Kuondolewa kwa watumishi hawa Jimbo linaona kwamba ni ishara
wazi kuwa huduma za afya tunazohudumia wananchi hazihitajiki tena, ikiwa na
maana kwamba serikali ina uwezo mkubwa wa kuendelea kutoa huduma hizi hivyo
sisi itatupasa kusitisha mara moja huduma tuzitoazo”, alisema Padri Ndunguru.
Alisisitiza kuwa katika kuendelea kujenga mahusiano mazuri ya
kuhudumia wananchi, Jimbo linaiomba serikali iwarejeshe watumishi hao ili
huduma za afya ziweze kuwa endelevu na wagonjwa wasiweze kupata usumbufu wa
aina yoyote ile.
Pia Mwandishi wetu alipozungumza na Katibu tawala wa mkoa wa
Ruvuma, Hassan Bendeyeko juu ya watumishi wa serikali kutokuendelea utiaji wa
saini kwa mikataba mipya ya ubia na vituo vya kutolea huduma binafsi, alikiri
kuwepo kwa jambo hilo na kukataa kutolea ufafanuzi licha ya ofisi yake ndiyo
iliyohusika kutoa maagizo hayo ya kuhamisha watumishi hao.
Hata hivyo inathibitisha kuwa agizo hilo limetolewa na ofisi
ya Katibu tawala huyo kupitia barua ya Aprili 18 mwaka huu ambayo nakala yake
tunayo yenye kumbukumbu namba EC. 124/138/01/A/31 kwenda kwa Wakurugenzi
watendaji wa halmashauri za wilaya mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa agizo
hilo.
No comments:
Post a Comment