Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi mkoa wa Ruvuma jana imempa dhamana
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dokta Vicent
Mashinji pamoja na baadhi ya viongozi wenzake wa chama hicho, ambao hapo awali
walikuwa wakisota mahabusu katika gereza la mahabusu Songea baada ya kushindwa
kukidhi vigezo na kamilisha masharti ya dhamana.
Aidha mbali na Dokta Mashinji, viongozi wengine katika shauri
hilo ambao nao wapo nje kwa dhamana ni Mbunge wa Jimbo la Ndanda Fecil Daud
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya kusini Masasi, Mwenyekiti wa CHADEMA
mkoa wa Ruvuma Irineus Ngwatura, Katibu wa CHADEMA mkoa wa Ruvuma, Sang’uda
Manawa na Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Nyasa Curthbeth Ngwata.
Washitakiwa wengine ni Katibu mwenezi wa chama hicho Leonard
Makunguru, Katibu wa CHADEMA Kanda ya kusini Masasi Filbert Ngatunga, Mbunge wa
viti maalum, Zubeda Sakuro na Katibu mwenezi wa chama hicho Kanda ya kusini
Charles Leonard ambapo wote kwa pamoja wapo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili
waaminifu ambao wamesaini hati ya dhamana ya shilingi milioni 2 kila mmoja.
Mara ya kwanza washitakiwa hao wote walipelekwa katika
Mahakama ya Hakimu mkazi mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa
Ruvuma, Simon Kobelo kwa makosa mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali na
kufanya maandamano bila kuwa na kibali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Wakili mfawidhi wa serikali kutoka Ofisi ya mwanasheria mkuu
wa serikali Kanda ya Songea, Renatus Mkude alisema kuwa hana pingamizi juu ya
dhamana kwa washtakiwa wote na kwamba Hakimu wa mahakama hiyo, Kobelo ndipo
naye aliungana na maelezo hayo ya mwanasheria mkuu wa serikali na hatimaye
kuwapatia dhamana hiyo kwa sharti la kwanza kuwa na wadhamini wawili waaminifu
kila mmoja.
Kwa mujibu wa Hakimu huyo alifafanua kuwa sharti la pili,
wadhamini hao aliwataka wasaini hati ya dhamana ya shilingi milioni mbili kila
mmoja jambo ambalo waliweza kutekeleza na kukidhi vigezo husika kwa washtakiwa
wote na kwamba kesi hiyo itatajwa tena Agosti 21 mwaka huu.
Akizungumza nje ya Mahakamna baada ya kupata dhamana Dokta Mashinji
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kukamatwa na kufikishwa Mahakamani ni kama
mchezo mchafu wa serikali ya awamu ya tano ambao unataka kuviua vyama vya
upinzani hapa nchini.
Pia Dokta Mashinji alilitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumika
vibaya badala yake lifanye kazi kwa weledi na kuacha kutumika upande mmoja jambo
ambalo linaweza kuleta taswira mbaya kwa Watanzania.
Alisema kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kipo katika
jukumu la kuwa andaa wanachama wake kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa
chama hicho ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu, hivyo wapo katika ziara
mikoa ya Kanda ya kusini kuzungumza na wanachama wake ili wajiandae kushiriki vyema
katika chaguzi hizo.
Alibainisha kuwa katika kufanikisha zoezi hilo chama
kilimtuma Mbunge wake Zubeda Sakuro kwenda wilayani Nyasa kwa ajili ya kufanya kazi
hiyo, ndipo akiwa katika mkutano na wanachama wengine alikamatwa na Jeshi la Polisi
kwa kosa la kufanya mkutano huo.
Dokta Mashinji alieleza kuwa walianza ziara yao tangu Julai
14 mwaka huu wakiwa Mbamba bay Nyasa mkoani Ruvuma, ikiwa ni maandalizi ya
uchaguzi wa Chama hicho ambapo wakiwa wanajiandaa kufanya mkutano wa ndani
walipata taarifa kwa Zebeda Sakuru ambaye ni Mbunge wa viti maalum mkoa wa
Ruvuma amekamatwa na Polisi na walipo mtuma mtu mwingine naye aliwekwa ndani na
kila waliyemtuma alikamatwa na kufanyiwa hivyo.
Pamoja na mambo mengine amewataka wanachama na viongozi wa
chama hicho kote nchini kuwa imara hasa wakati huu ambao chama kimeamua
kuendelea kujiimarisha kwa ajili ya kushiriki vyema chaguzi za ndani ya
chama ili kuweza kupata viongozi ambao wataweza kushiriki katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment