Na Kassian Nyandindi,
Songea.
VIONGOZI nane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
akiwemo Katibu Mkuu taifa wa chama hicho, Dokta Vicent Mashinji wameripoti kwa
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma jana majira saa nne asubuhi na wapo nje kwa dhamana wakisubiri hatma yao.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gemini Mushy alisema kuwa
viongozi hao waliripoti Ofisini kwake majira hayo ambapo alikuwa akisubiri Jalada
la kesi yao ambalo lipo kwa Wakili wa serikali mfawidhi mkoa wa Ruvuma.
Aliwataja viongozi hao wanaotuhumiwa kuandamana na
kufanya mkutano bila kibali katika wilaya ya Nyasa kuwa ni Cecil Mwambe ambaye ni
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya kusini na Mbunge wa jimbo la Ndada,
Philbert Ngatunga Katibu wa Kanda ya kusini CHADEMA, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa
wa Ruvuma Ereneus Ngwatura na Delphin Gazia ambaye ni Katibu wa chama hicho mkoa
wa Ruvuma.
Wengine ni Zubeda Sakuru Mbunge Viti maalum mkoa wa
Ruvuma kupitia tiketi ya chama hicho, Sang’uda Moses Mkuu wa Organization na
mafunzo CHADEMA, Carthberth Ngwata Mwenyekiti wilaya ya Nyasa wa chama hicho pamoja
na Charles Makunguru Katibu mwenezi wilaya ya Nyasa.
Kadhalika Kamanda Mushy aliwataka wanachama na wapenzi
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kuwa watulivu wasivunje sheria, bali
waendelee kuwa watulivu.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Chama hicho Dokta
Mashinji akizungumza na mwandishi wetu nje ya Ofisi za CHADEMA mkoani Ruvuma zilizopo
katika mtaa wa Matarawe Manispaa ya Songea, alisema kuwa walikamatwa na
kuambiwa wamevunja sheria kwa kufanya maandamano na mkutano jambo ambalo
halikuwa la kweli kwani wao walikwenda Mbambabay kwa kutaka kufanya kikao cha
ndani ambapo walipotaka kuanza ndipo waliposhitukia kuona askari wakiwazunguka
na kuwakamata.
“Hii inaonyesha ni mikakati ya wazi na ya makusudi kuwavuruga wanachama
wetu ili wasifanye maendeleo yao ndani ya chama chetu wakati Chama Cha Mapinduzi
kinaendelea kufanya mikutano ya ndani na wala hakisumbuliwi”, alisema Mashinji.
Aliiomba serikali ione umuhimu wa kujali siasa za mfumo
wa vyama vingi na siyo kuwawekea vikwazo pale wanapojaribu kujipanga kwa ajili
ya chaguzi zijazo huku akiongeza kwa kuwataka wanachama wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo kote nchini waendelee na shughuli za chama kwa kufuata
taratibu na sheria zilizopo na wasiogope mtu yeyote.
Hata hivyo hadi kufikia leo viongozi hao wapo nje kwa dhamana wakisubiri taratibu zingine za kufikishwa kesho Mahakamani.
Hata hivyo hadi kufikia leo viongozi hao wapo nje kwa dhamana wakisubiri taratibu zingine za kufikishwa kesho Mahakamani.
No comments:
Post a Comment