Na Mwandishi wetu,
Madaba.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani
Ruvuma Shafi Mpenda amefanikiwa kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu, kati
ya wakulima wanaozalisha mahindi na uongozi wa serikali ya kijiji cha Madaba wilayani
humo ambao walikuwa wakigombea umiliki wa ghala la kuhifadhia mahindi lililopo
kijijini humo.
Mgogoro huo ambao umedumu kwa muda wa miaka miwili,
ukihusisha pande mbili kati ya wakulima hao kupitia kikundi chao cha KIWAMA
ulisababisha wakulima kutokuwa na sehemu ya kuhifadhia mahindi yao katika
kipindi cha mavuno baada ya ghala hilo kutumiwa na Wakala wa taifa wa hifadhi
ya chakula.
Alisema kuwa ghala hilo limejengwa na serikali kwa gharama ya
shilingi milioni 85 kupitia halmashauri ya wilaya ya Songea kabla ya kugawanywa
na kuzaliwa halmashauri mpya ya wilaya ya Madaba, ili liweze kuwasaidia
wakulima hao kupitia vikundi vyao vya kukusanyia mazao ya chakula na biashara hasa
mahindi wakati wanapokuwa wakisubiri soko la kuyauza.
Mpenda ameuagiza uongozi wa kijiji cha Madaba kuweka
utaratibu maalum wa kutumia ghala hilo ili kila upande uweze kulitumia badala
ya kunufaisha upande mmoja.
Hali kadhalika aliongeza kwa kuwataka viongozi wa vijiji na
kata ndani ya wilaya hiyo, kuhakikisha kwamba wanahimiza wananchi wao kufanya
shughuli za kimaendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Selina Kilumile ambaye ni Mweka hazina wa kikundi
cha KIWAMA alisema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 kikundi hicho
kimeweza kuzalisha ekari 991 za zao la mahindi, lakini changamoto kubwa
inayowasumbua hivi sasa ni sehemu ya kuhifadhi mazao hayo pamoja na soko la
kwenda kuyauza ili waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao.
No comments:
Post a Comment