Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
wamesikitishwa na kitendo cha serikali kuchukua hatua ya kuhamisha watumishi
wake wa kada ya afya ambao walikuwa wakitoa huduma kwenye hospitali, vituo vya
afya na zahanati zilizokuwa chini ya mamlaka ya Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani
humo.
Aidha wameiomba serikali kuwarejesha watumishi hao
katika maeneo waliyokuwa wakifanyia kazi kwenye Jimbo hilo, ili kuweza kunusuru
hali za wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu katika vituo hivyo vya kutolea
huduma za afya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari
walisema kuwa hivi sasa uongozi wa Jimbo Katoliki la Mbinga unashindwa
kuendelea kutoa huduma za afya katika vituo hivyo kutokana na kukosa wauguzi na
wataalamu wenye uwezo wa kutibu wagonjwa.
Pia walidai kuwa kufuatia hali hiyo hospitali ya misheni
Litembo na vituo vingine vinavyoendeshwa na Jimbo hilo muda wowote kuanzia sasa
huenda vikafungwa visitoe huduma kwa wagonjwa kutokana na kukosa watumishi
wenye uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali.
Vilevile akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake,
Aidan Challe ambaye ni mkazi wa kijiji cha Myangayanga kata ya Myangayanga
wilayani hapa alisema kuwa kutokuendelea na utiaji wa saini kwa mikataba mipya
ya ubia baina ya serikali na vituo vya kutolea huduma vya binafsi ni sawa na
kuumiza wananchi, kwani ndani ya wilaya ya Mbinga tegemeo kubwa la watu
kupatiwa matibabu ya uhakika yapo katika hospitali hiyo ya Misheni Litembo.
Challe alisema vituo vya serikali vya kutolea huduma za
afya vilivyopo wilayani humo vingi vimekuwa havitoi huduma bora kutokana na
kuwa na upungufu wa madawa na vifaa tiba vya kutibu wagonjwa hivyo watu wengi
wamekuwa wakikimbilia kwenye vituo vya Jimbo Katoliki la Mbinga kupatiwa
matibabu kutokana na huduma zao kuwa bora.
“Tunaiomba serikali iangalie upya namna ya kurejesha
mikataba hii ya ubia na hawa wenzetu wa Jimbo hili, leo vituo vyao vya kutolea
huduma za afya kama vile hospitali hii ya Litembo ambayo ndiyo tegemeo kubwa
kwa wilaya yetu jimbo linataka kuifunga kutokana na agizo hili lililotolewa la
kuwahamisha watumishi wake mimi binafsi nahoji je tutakimbilia wapi kuokoa uhai
wetu pale tutakapougua?”, alisema Challe.
Kadhalika naye Joackimu Kinemela ambaye ni mkazi wa
kijiji cha Mapera kata ya Maguu alisema kuwa uamuzi huo uliochukuliwa na
serikali unapaswa kuangaliwa upya kwani kwa kiasi kikubwa ni sawa na kuwapa
mateso wananchi ambao hawana hatia mbele ya Mungu.
Mratibu wa afya Jimbo hilo la Mbinga, Padri Raphael
Ndunguru naye aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wapo katika hatua ya
kuvifunga vituo vyao vya kutolea huduma za afya kutokana na kuwa na upungufu
mkubwa wa watumishi wenye sifa ya kuhudumia wagonjwa.
Padri Ndunguru aliongeza kuwa uongozi wa jimbo unatambua
kwamba kitendo hicho kilichofanywa na serikali kuwahamisha watumishi wake
watakaoathirika kwa kiasi kikubwa katika tukio hili ni wananchi hivyo kuna
umuhimu wa kukaa na kujadili suala hilo kwa pamoja kati ya serikali na jimbo
ili kuweza kufikia muafaka mzuri juu ya jambo hilo.
“Sisi hatuoni kama kuna sababu ya msingi ya kuwahamisha
watumishi hawa, tumeishi nao vizuri kwa miaka mingi na kufanya nao kazi pamoja
hivyo tunaiomba serikali iturejeshee tena watumishi hawa ili tuweze kuendelea
kuhudumia wananchi wetu”, alisema Padri Ndunguru.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko
alipoulizwa juu ya watumishi wa serikali kutokuendelea utiaji wa saini kwa
mikataba mipya ya ubia na vituo vya kutolea huduma binafsi alikiri kuwepo kwa
jambo hilo huku akikataa kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo licha ya ofisi
yake ndiyo iliyohusika kutoa maagizo hayo ya kuhamisha watumishi hao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu unathibitisha kuwa agizo hilo lilitolewa na ofisi ya Katibu tawala huyo kupitia barua ya Aprili 18 mwaka huu ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba EC. 124/138/01/A/31 kwenda kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya hapa mkoani Ruvuma kwa ajili ya utekelezaji wa suala hilo.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu unathibitisha kuwa agizo hilo lilitolewa na ofisi ya Katibu tawala huyo kupitia barua ya Aprili 18 mwaka huu ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba EC. 124/138/01/A/31 kwenda kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya hapa mkoani Ruvuma kwa ajili ya utekelezaji wa suala hilo.
No comments:
Post a Comment