Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya Wananchi waishio katika Halmashauri ya wilaya ya
Madaba mkoani Ruvuma wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwajengea hospitali ya
wilaya ambayo wataweza kupata huduma za matibabu, ikiwemo kuhudumia wananchi
wengi badala ya kuendelea kutegemea kituo cha afya Madaba ambacho kinaonekana
kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wa aina mbalimbali.
Aidha walisema kuwa hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la
watu hasa baada ya serikali kuanzisha halmashauri hiyo, hivyo kuna umuhimu wa
kusogezewa karibu huduma hiyo ili wasiendelee kupata usumbufu kama wanaoupata
sasa wa kufuata huduma ya matibabu umbali mrefu mjini Songea.
“Kituo hiki cha afya Madaba kwa sasa hakina uwezo wa
kuhudumia wagonjwa wanaokuja hapa kwa ajili ya kupata matibabu, njia pekee tunaiomba
serikali kujenga hospitali kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia
wananchi wengi kwa wakati mmoja sambamba na kuweka vifaa tiba na wataalamu”, walisisitiza.
Alphonce Danda alifafanua kuwa wakati umefika kwa serikali kuanza
kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa wilaya hiyo, kujenga miundombinu ya
kutosha ya afya kama vile huduma ya maji, afya na barabara jambo ambalo litasaidia
kuboresha maisha na maendeleo ya wananchi wake.
Danda alibainisha kuwa serikali imeamua kuanzisha halmashauri
ya wilaya miaka miwili iliyopita kwa lengo la kusogeza karibu huduma za kijamii
ikiwemo matibabu kwa wananchi wake, lakini halmashauri hiyo bado pia inakabiliwa
na matatizo kama vile ukosefu wa watumishi wa kutosha katika kada mbalimbali, makazi
ya watumishi hao ikiwemo nyumba ya kuishi Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya.
Naye John Mlelwa alisema mbali na tatizo la makazi ya kuishi watumishi
pia kuna upungufu mkubwa wa watumishi hasa wakuu wa idara mbalimbali kwani
waliopo ni wale wanaokaimu tu na kusababisha shughuli nyingi kukwama kutokamilika
kwa wakati.
Mlelwa aliwapongeza watumishi wachache waliopo kwa utendaji
kazi mzuri kwani licha ya uchache wao hata hivyo wamesaidia kuboresha huduma husika
na kuleta tija sehemu ya kazi.
No comments:
Post a Comment