Na Muhidin Amri,
Madaba.
MWENYEKITI wa Serikali ya kijiji cha Mateteleka kata ya Wino
Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Remigius Njafula anatuhumiwa
kugawa ardhi ya kijiji hicho kwa wageni, kinyume na taratibu husika jambo
ambalo linasababisha kuzuka kwa mgogoro mkubwa kijijini hapo.
Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo Shafi Mpenda, katika kikao kilichowajumuisha Wazee pamoja na uongozi
wa kijiji wazee hao walifafanua kuwa vitendo hivyo vya dhuluma ya ardhi amekuwa
akiwafanyia hasa wanawake na vijana.
Aidha wazee hao wamelalamikia kitendo cha Mwenyekiti huyo
kutumia nguvu na kupokonya msitu wa kijiji ambao uliuzwa kwa kikundi cha Jitegemee
kilichopo kijijini humo, miaka 15 iliyopita na kuanza kugawa maeneo ya msitu
huo bila kushirikisha wamiliki husika.
Wakizungumza kwa niaba ya wazee wenzao mzee, Lucas Mayemba na
Evolius Mbilinyi walisema kuwa Mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na baadhi ya
wajumbe wa serikali ya kijiji analalamikiwa pia kwa ubadhirifu wa shilingi milioni
9 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji na shilingi 600,000
zilizotolewa na mfuko wa Mbunge wa jimbo la Madaba na wahisani wengine kwa
ajili ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi shuleni.
Walisema Njafula kwa kushirikiana na viongozi wengine wa
kijiji wamehamisha fedha na kwenda kuziweka kwenye akaunti ya mkandarasi kabla
hajaanza kutekeleza mradi husika.
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo alipoulizwa alikiri kuhamisha
fedha hizo hata hivyo alieleza kuwa maamuzi hayo, yalifikiwa mbele ya mkutano
mkuu wa kijiji ambao uliamua fedha zielekezwe huko ili kuepusha wajanja
wachache kuzitafuna.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Shafi
Mpenda mbali na kusikitishwa na tabia hiyo iliyofanywa na Mwenyekiti huyo ameahidi
kulifikisha tatizo hilo kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze
kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment