Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga
mkoani Ruvuma, inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa
wanaopata rufaa hasa kwa upande wa akina mama wajawazito, ili waweze kupelekwa
hospitali ya ya mkoa Songea na misheni Litembo au Peramiho zilizopo mkoani humo
kwa matibabu zaidi.
Kufuatia hali hiyo yamekuwa yakitumika magari ambayo hayapo katika
mfumo rasmi wa kusafirisha wagonjwa hao ambayo pia ni chakavu, hali ambayo
imekuwa ni kero kubwa katika jamii ikiwemo utekelezaji wa majukumu husika.
Hayo yalisemwa na Kaimu mganga Mkuu wa hospitali hiyo,
Aristachius Nkwenge wakati alipokuwa akitoa maelezo mafupi mbele ya Mbunge wa
Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda, ambaye alitembelea hospitalini hapo kwa
ajili ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali na kujionea changamoto zilizopo.
Nkwenge alimweleza Mbunge Mapunda kuwa changamoto nyingine
wanayokabiliana nayo ni kutokamilika kwa ujenzi wa jengo la wodi ya wagonjwa
mahututi (ICU) na uchakavu wa vichomea taka.
Alisema kuwa pia hospitali ya mji wa Mbinga haina jokofu la
kuhifadhia maiti licha ya uwepo wa jengo maalumu ambalo limejengwa kwa muda
mrefu kwa ajili ya kuhifadhia miili hiyo.
“Hospitali yetu inakabiliwa pia na changamoto ya kutokuwepo
kwa jengo la wodi ya watoto na uchakavu wa miundombinu ya majengo ya hospitali
pamoja na upungufu wa watumishi hususan wa kitengo cha mionzi na vifaa tiba”,
alisema Nkwenge.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Mapunda aliweza
kupunguza changamoto zilizokuwa zinaikabili hospitali ya mji huo kwa kukabidhi msaada
wa vifaa kama vile vitanda 25, magodoro ya kulalia wagonjwa 25, vitanda vya
kujifungulia akina mama wajawazito 2 pamoja na mashuka ya kujifunika wagonjwa
105 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 5,050,000.
“Utoaji wa vifaa hivi utasaidia kupunguza baadhi ya
changamoto zilizokuwa zinaikabili hospitali yetu, pia nitajitahidi kufanya
ufuatiliaji serikalini juu ya changamoto nyingine ambazo zinahitaji kutatuliwa
ili kuweza kuboresha mahitaji muhimu yanayotakiwa kuwepo na kutekelezwa katika
hospitali hii”, alisisitiza Mapunda.
No comments:
Post a Comment