Na Muhidin Amri,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka wananchi
na viongozi wa Tanzania na Msumbuji kuhakikisha kwamba wanapambana na tatizo la
umaskini ambao umekithiri katika nchi zao, ili kuweza kuendelea kuwa na hali ya
amani na utulivu katika nchi hizo.
Dokta Mahenge alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akifunga
mkutano wa ujirani mwema ambao ulishirikisha mikoa ya Ruvuma na Mtwara upande
wa Tanzania na Jimbo la Niassa na Cabo Delgado nchini Msumbiji ambao ulifanyika
juzi kwenye ukumbi wa Hunt Club uliopo mjini Songea mkoani Ruvuma.
“Kinachohitajika hivi sasa ni viongozi kushirikiana na
wananchi kwa pande zote mbili na kuhakikisha mnasimama imara ili tuweze kufanya
kazi kwa bidii na kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani, hatua ambayo
itasaidia vijana kujiepusha na vitendo vya uharibifu na ujangili”, alisema.
Alisema kuwa endapo hapatakuwa na mshikamano na utulivu huu
uliopo sasa wahalifu watakuwa na nafasi kubwa ya kuvuka mipaka na kujificha
nchi jirani, kwa lengo la kuvuruga amani iliyopo na hatimaye kurudisha nyuma
maendeleo ya wananchi.
Pia alibainisha kuwa harakati za wananchi kujiletea maendeleo
hazitafanikiwa endapo masuala ya usalama wa mipaka ya nchi hizo yatavurugwa,
hivyo pande zote mbili zitaendelea kuwa na umaskini.
Dokta Mahenge alisema kuwa hakuna sababu ya watu wa Msumbuji
kuagiza chakula kutoka nchi za Ulaya, kwa sababu Tanzania ndani ya mkoa wake wa
Ruvuma kuna chakula cha kutosha kinachoweza kutosheleza mahitaji ya wananchi.
Naye Gavana wa Jimbo la Cabo Delgado nchini
Msumbuji, Celmira Frederico Pena da Silva alisema kuwa hivi sasa kazi kubwa iliyopo
wanatakiwa kuendelea kudumisha amani kwa pande zote mbili na kuwawezesha
wananchi kukua kiuchumi.
Vilevile kwa upande wake Gavana wa Jimbo la Niassa Alindo
Chilundo aliongeza kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 wananchi
wa jimbo hilo walifanikiwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 5 za
mahindi na kuwataka wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenda Msumbiji kununua zao
hilo ikiwa ni njia mojawapo ya kudumisha umoja na uhusiano uliopo miongoni
mwao.
No comments:
Post a Comment