Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia,
wazee na watoto Dokta Khamis Kigwangala amempa mwezi mmoja Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Robert Mageni ahakikishe kwamba
jengo la upasuaji katika hospitali ya halmashauri ya mji huo linafanyiwa
ukarabati haraka ili liweze kuwa katika hali nzuri.
Agizo hilo limetolewa juzi na Dokta Kigwangala alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi ambapo kufuatia jengo hilo kuwa chakavu katika maeneo
mbalimbali ya ndani na nje hususan kwa yale yanayotumika kuoshea vifaa vya
kutibu wagonjwa ameagiza pia yajengewe marumaru ili kuweza kuzuia uzalishaji wa
wadudu ambao ni hatari kwa afya ya binadamu.
Vilevile ametaka pia chumba cha kunawia pamoja na miundombinu
ya maji katika jengo hilo nayo vifanyiwe ukarabati mapema ikiwemo milango yake ili
iweze kufunguka upande wa ndani na nje.
Dokta Kigwangala alisisitiza pia katika maeneo ya ndani ya
jengo kuwepo na alama maalumu ili kuweza kuzuia watu wasiweze kuingia hovyo
hasa muda ambao shughuli mbalimbali za upasuaji zinafanyika.
“Milango ya jengo hili ifanyiwe ukarabati upya ili iweze
kufunguka vizuri ndani na nje, chumba cha kunawia na masinki ya maji nayo yafanyiwe
ukarabati”, alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine alipoingia katika jengo la maabara
katika hospitali hiyo ya halmashauri ya mji wa Mbinga, alipongeza miundombinu
ya jengo hilo ikiwa katika hali nzuri na kuwataka iendelee kuwa katika hali
hiyo ili wagonjwa waweze kuhudumiwa katika mazingira mazuri.
No comments:
Post a Comment