Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SAKATA la Mgogoro wa fedha za mapato
yatokanayo na uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, limechukua sura mpya kufuatia baraza la Madiwani wa
halmashauri hiyo kumsimamisha kazi Afisa misitu wa mji huo, David Hyera ambaye
anadaiwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika ubadhirifu wa mapato hayo.
Aidha kusimamishwa kazi kwa afisa
huyo ni kwa ajili ya kupisha uchunguzi baada ya Madiwani hao kukubaliana kwamba
iundwe Kamati maalumu ya kuchunguza suala hilo ili kuweza kupata ukweli zaidi
wa jambo hilo na hatimaye hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika
watakaopatikana wameshiriki wizi huo.
Maamuzi hayo yalifikiwa juzi kwenye kikao
cha robo ya nne cha baraza lao kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo
uliopo mjini hapa, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndunguru Kipwele ambapo
walieleza kuwa makisio ya awali baada ya kufanyika upembuzi yakinifu na
mtaalamu huyo wa misitu na kuwasilishwa katika kikao cha baraza kilichoketi
Oktoba 12 mwaka jana, yalikuwa zipatikane zaidi ya shilingi milioni 325 ambazo
ni baada ya uvunaji huo kufanyika lakini wanashangaa kuelezwa kwamba
zimepatikana shilingi milioni 196.
Akichangia hoja katika kikao hicho diwani
wa kata ya Mpepai, Benedict Ngwenya alisema kuwa shughuli za uvunaji wa msitu
wa Mbambi kabla hazijaanza kufanyika kupitia vikao husika walikubaliana kwamba
Kamati husika ya mipango miji na mazingira ilibidi iende kwenye eneo la msitu
huo na kujiridhisha lakini kamati hiyo ilizuiwa isiende huko kwa ajili ya kuukagua msitu huo na badala yake
anadaiwa kwenda Mkurugenzi mtendaji, Robert Mageni na wataalamu wake.

























