Monday, March 25, 2013

MAKAA YA MAWE YAMPONZA GAUDENCE KAYOMBO, ATAMANI KUJIUZURU

Gaudence Kayombo Mbunge Mbinga Mashariki.


















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI siku zote wamekuwa wakiamini kwamba, kiongozi yeyote aliyewekwa madarakani, ni mtetezi na msimamizi mkuu wa maendeleo yao katika eneo husika.

Kana kwamba hilo halitoshi, baadhi yao wakishawekwa madarakani wanaonekana kuwa mwiba kwa wananchi, na hata kutotimiza ipasavyo majukumu yao ya kazi.

Jamii siku zote hufikia hatua ya kupoteza imani kwa viongozi wao endapo tu, pale wanapobaini msimamizi wao wa maendeleo tayari yupo katika mrengo wa kushoto dhidi yao, wakimuona akijijengea maslahi yake binafsi na kusahau wananchi anaowatumikia.

Tatizo hili likigundulika ndio maana utakuta migogoro au malalamiko ya hapa na pale huanza kujitokeza, na kiongozi husika kunyoshewa kidole wakati mwingine kusababisha kutokea kwa vurugu zinazoweza kuhatarisha amani katika eneo husika.


Mwandishi wetu wa makala haya, anapenda kuelezea juu ya mgogoro uliojitokeza katika kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo hivi karibuni ametishia kujiuzuru wadhifa huo, kwa kile kinachodaiwa kufuatia kushushiwa tuhuma nzito dhidi yake.

Tuhuma hizo zinatokana na wakazi wa kata hiyo kumtuhumu Mbunge huyo kwamba anashindwa kuyafanyia kazi matatizo ya wananchi wa kata hiyo kwa kile kinachodaiwa kwamba, kutokana na kuwa na mahusiano ya karibu na mwekezaji wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ruanda katika kata hiyo.

Tuhuma hizo za wananchi ziliwasilishwa katika kikao cha  Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kilichoketi Februari 26 mwaka huu, kwenye ukumbi wa jengo la Mfuko wa maendeleo ya jamii(TASAF) liliopo katika kata hiyo.

Wajumbe wa kikao hicho ndio waliowasilisha tuhuma husika, ambapo kikao kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda na kwamba licha ya Mbunge Kayombo kupewa mwaliko wa kuhudhuria kikao, lakini hakuweza kujitokeza na haikujulikana ni kwa sababu gani.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vimeendelea kueleza kuwa pamoja na Mbunge huyo kuwa karibu na mwekezaji huyo, pia inadaiwa amejengwa nyumba ya gorofa moja kijijini kwao Ruanda na kujimilikisha ekari 400 za ardhi katika kata ya Ruanda bila kufuata taratibu husika.

Kayombo ni mzaliwa wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda, ambako ndiko hivi sasa uchimbaji na usafirishaji wa makaa ya      mawe katika mgodi wa Ngaka umekuwa ukiendelea kufanyika na mgodi huo, unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali, kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Baada ya kikao hicho kuwasilisha tuhuma hizo, imeelezwa kuwa Mbunge Kayombo alipigiwa simu na mmoja kati ya wajumbe waliokuwepo katika kikao hicho(jina tunalo) wakimtaka waonane naye.

Kufuatia hilo Mbunge huyo aliwajibu yupo safarini akitokea mjini Songea na kuelekea huko kijijini kwao alikozaliwa, hivyo anaomba wamsubiri ili waweze kuzungumzia tatizo hilo.

Baadhi ya wajumbe walipoona muda mrefu unazidi kwenda na hajitokezi, waliamua kuchukua uamuzi wa kuanza kurudi wakiwa katika gari lao na kwamba kwa bahati nzuri wakiwa njiani walifanikiwa kuonana naye akitokea safari yake aliyowaeleza ndipo wakaamua kusimama na kumueleza yaliyojiri katika kikao hicho.

Chanzo chetu cha habari kinasema, Kayombo alipoelezwa shutuma hizo alionekana kuwajia juu, huku akionesha kusikitishwa na kuwaeleza wajumbe hayo ni malalamiko ambayo si ya kweli.

“Mheshimiwa Mbunge baada ya kusimama pale na kumweleza hili alikuja juu na kusema, yeye nyumba wanayomtuhumu amejengewa na mwekezaji alisema ameijenga mwenyewe na suala la kumiliki ardhi ekari 400 sio la kweli, na alikana kwamba hana mahusiano yoyote ya karibu na mwekezaji wa mgodi huo”, kilisema chanzo chetu ambacho kiliomba kisitajwe gazetini.

Habari zinaarifu kuwa eneo hilo ambalo walisimama kati ya Kayombo na wajumbe waliotoka katika kikao hicho, hapakuwa na amani wala maelewano hadi wana achana, kutokana na Mbunge huyo kung’aka na kujawa jazba huku mwishoni akiwaeleza na kutishia wenzake kwamba ni vyema ajiuzuru kutokana na kashfa wanazomtuhumu kutokuwa  na ukweli.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa hadi habari hizi zinaenda mitamboni, tayari jopo la uongozi wa CCM wilayani Mbinga mnamo tarehe 1 mwezi Marchi mwaka huu, lilikwenda nyumbani kwa Kayombo kijijini kwao na kumsihi asijiuzuru na inadaiwa kwamba huenda asijiuzuru pamoja ya kwamba Mbunge huyo awali kuweka msimamo wa kutaka kuachia madaraka hayo.

Tumeendelea kubaini pia hilo, linatokana na wakazi wa kata ya Ruanda wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu na kupinga kusafirishwa kwa makaa hayo ya mawe ambayo yanachimbwa katika kijiji cha Ntunduaro katika kata hiyo, wakitaka watekelezewe kwanza madai yao ya msingi ambayo mwekezaji husika anaonekana kutoyatimiza.

Kwamba madai yao ni nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa mazingira yakiwemo maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini hayo.

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia kutokana na wachimbaji wa makaa ya    mawe kutiririsha maji yenye mkaa kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe kama vile samaki kupoteza maisha.

Wakati hilo linatokea serikali wilayani Mbinga licha ya kutuma wataalamu wake wa mazingira kwenda huko na kufanya upembuzi yakinifu juu ya tatizo hilo, bado majibu ya uhakika juu ya madhara ya maji hayo yaliyochanganyika na mkaa wa mawe, hayajatolewa kwa wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo.

Kamati ya ulinzi na usalama, hivi karibuni ilienda kule na kuwatuliza tu wananchi wale na kutoa kauli kwamba madai yao yapo kwenye ngazi husika yanashughulikiwa, baada ya kuonekana hali ya kutaka kuhatarisha amani kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy.

Pia jukumu lililochukuliwa na kamati hiyo ni kwenda huko na kuamuru wachimbaji hao, kuzuia maji hayo yenye mchanganyiko na mkaa huo yasielekezwe tena katika mto huo ili kunusuru maisha ya wakazi hao.

Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo alipoulizwa juu ya tuhuma na malalamiko hayo, alisema yeye hawezi kuzungumzia lolote kwa sasa.

Vilevile ofisa ardhi na maliasili wa wilaya hiyo Richard Mwaiseje, alipotakiwa kutolea maelezo juu ya Mbunge huyo kujimilikisha ekari zaidi ya 5,000 za ardhi, alisema hana uthibitisho juu ya tuhuma hizo.

“Si dhani kama ni taarifa ya kweli, kwa sababu na sisi tunalisikia tu hivyo mpaka nifanye utafiti kama ni kweli anamiliki maeneo makubwa au vipi”, alisema Mwaiseje.

Kadhalika kumekuwa na vumbi kali la mkaa wa mawe limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa jirani na mgodi huo pale unaposafirishwa kwenda bandari ya Ndumbi iliyopo katika ziwa Nyasa, Kiwira mkoani Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji Tanga kilichopo mkoani Tanga, huenda hali ya kiafya kwa wananchi wale ikawa hatarini endapo hatua husika hazitachukuliwa kwa uharaka.

Nimezungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ntunduaro ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, wakidai kwamba wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na utekelezaji wake unaonesha ukifanywa taratibu licha ya hata Mbunge wao Gaudence Kayombo kufikishiwa mezani kwake na hakuna hatua alizozichukua ndio maana leo hii wanakosa imani naye.

Viongozi wa serikali wa kata ya Ruanda wamezungumza na mwandishi wa makala haya kwa nyakati tofauti, wamesema ni kweli malalamiko hayo yapo na hata kwa mbunge wao yamefikishwa na majibu yanayotolewa ni ahadi tu, kwamba yanafanyiwa kazi huku siku zikiendelea kuyoyoma utekelezaji wake hauonekani.

Pia walisema kampuni ya  Tancoal Energy ambayo inachimba mkaa huo kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi kuifanya ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, ni jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko yasiyo na msingi badala yake wamemtaka mwekezaji huyo atimize mambo ya msingi ili kumaliza mgogoro huu uliopo sasa usiweze kuendelea.

Mwandishi wa makala haya ameshuhudia hata katika eneo linalotumika na baadhi ya wafanyakazi wenye asili ya kitanzania, wamekuwa wakitengwa ambapo wengi wao wamekuwa wakilalamika hawajajengewa vyoo na muda wa chakula unapowadia hujisetiri katika eneo la wazi kutokana na kubaguliwa na mwekezaji husika na kulazimika kutumia vyoo vya majirani wanaoishi kuzunguka eneo lilipo ofisi za mgodi huo. 

Madereva wanaoendesha magari ya kampuni hiyo ndio wamekuwa wakitengwa kwa kiasi kikubwa,  ambapo walitolea mfano kwa gari aina ya Pickup mtanzania huruhusiwa kupanda nyuma ya bodi la gari hilo ambalo liko wazi, na katika sehemu nzuri ya gari katikati hubebwa mnyama aina ya nyani, kitendo ambacho baadhi yao wanasema ni ubaguzi uliokithiri.

Hata hivyo jitihada ya kumpata Meneja wa Tancoal Energy Injinia Isaac Mamboleo, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya hali hii inayolalamikiwa zilishindikana.

Binafsi nashauri kukalia kimya malalamiko ya wananchi ni kutowatendea haki, kila mtu anapenda na kutaka kusifiwa lakini hakuna anayetaka kupokea lawama au hata wajibu wa kuwajibika wengine wakifanya mabaya kwa niaba yao.

No comments: