Friday, March 1, 2013

WAZEE WA TUNDURU WAIJIA JUU CCM


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la wazee wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeazimia kufanya kikao cha dharula na kuiteua tume itakayo kwenda kuonana na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya kikwete na kupeleka kilio na kero za wananchi wa wilaya hiyo.

Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti Mwenyekiti mstaafu wa CCM wilaya hiyo Kanduru Kassim,  na mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kapopo walisema kuwa hali
hiyo imetokana na kuwepo kwa tabia za viongozi wa chama na serikali wilayani humo, kupuuza kero na malalamiko ya wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema licha ya malalamiko hayo ambayo yanafahamika, lakini chama na serikali vikiwa vimekaa kimya, hivyo baraza hilo limeadhimia kukutana na kuainisha kero zote na kuzianisha tayari kwa safari hiyo zikiwa ni juhudi za kukinusuru chama cha mapinduzi.



Wakitoa kauli hiyo kufuatia chama kutozingatia na kufanyia kazi kero na malalamiko kukithiri kwa vitendo vya kudharauliwa na viongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wazee hao wamebainisha baadhi ya vitendo ambavyo vimekuwa vikifanywa na viongozi wa chama hicho, kuwa ni pamoja na viongozi hao kuchelewa kufika kwa wakati katika mikutano ambayo huiitisha, kutopokea maoni na kero za wazee hali ambayo waliieleza kuwa ni dharau kwao.

Wazee hao waliendelea kufafanua kuwa miongoni mwa vitendo vinavyowapa kero wazee hao ni pamoja na viongozi wa chama kutotoa nafasi na kuchukua maoni na kero za wazee.

Walisema nchi nzima inajengwa kwa kutegemea baraka na maoni ya wazee ambao pamoja na mambo mengine, wameona mengi na kutahadharisha kuwa endapo wakiendelea kudharauliwa ipo hatari kwa chama hicho kufanya vibaya katika matokeo ya chaguzi zijazo.

Akijibu kero hizo katibu wa CCM wilaya ya Tunduru Ramadhan Ameir pamoja na kukiri kuwepo kwa mapungufu hayo, aliwaomba wazee hao kurudi na kukaa chini kujipanga upya kwani tatizo hilo linaweza kutatuliwa kupitia vikao vya ndani.

No comments: