Wednesday, March 27, 2013

MKUU WA WILAYA ALIA NA WANAOKWAMISHA MRADI WA USHOROBA, JESHI LA POLISI LAAGIZWA KUWACHUKULIA HATUA WAHUSIKA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JESHI la polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeagizwa kuhakikisha kwamba linafanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu walioshiriki katika zoezi la hujuma za kubomoa jengo la mradi wa Ushoroba na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 36.9.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alitoa agizo hilo katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama, kilichoketi kwa ajili ya kujadili hasara za uharibifu wa mradi huo, ambao unajengwa kijiji cha Lukala kilichopo Kata ya Mchesi tarafa ya Lukumbule wilayani humo.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na nchi ya Ujerumani, unajengwa ikiwa ni juhudi ya mwendelezo mradi wa ushirikiano wa kudhibiti vitendo vya ujangili, ambao umekuwa ukifanywa na wawindaji haramu katika nchi za Tanzania na Msumbiji.


Taarifa za utekelezaji wa mradi huo zitahusisha ujenzi wa nyumba moja na ofisi, itakayotumiwa na maafisa watakaoshiriki katika zoezi la ulinzi na uzuiaji wa wawindaji haramu na kwamba fedha hizo zimetolewa serikali ya ujenrumanin kwaajili ya kifanikisha zoezi hilo.

Naye Mbunge wa Tunduru Kusini Alhaji Mtutura alisema kuwa baada ya kubaini kuwepo kwa hujuma na uharibifu huo, alimuamuru mkandarasi anayejenga majengo ya nyumba ya kuishi watumishi unaogharimu shilingi milioni 19,746,500 na ofisi itakayotumiwa na maafisa hao itakayogharimu shilingi milioni 17,195,562 hadi kukamilika kwake kusimamisha ujenzi huo hadi atakavyo taarifiwa.

Alisema awali mradi huo ulipangwa kujengwa katika kijiji cha Wenje mpakani mwa nchi za Msumbiji na Tanzania, eneo ambalo wananchi wake waliukataa na baada ya kukaa vikao               vilivyowashirikisha wananchi hao, ilikubaliwa ujengwe katika kijiji cha Lukala lakini inashangaza wao kuukataa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka katika kijiji hicho zinaeleza kuwa majengo hayo, yalibomolewa na kundi la vijana zaidi ya 100 wanadaiwa kuwa walishawishiwa na kundi la wawindaji haramu, ambao wanadaiwa kuendelea kuwashawishi wananchi wa kijiji hicho, wasiukubali mradi huo kwa madai kwamba wakizubaa na kuacha mradi huo uendelee, wananchi hao hawatafanya shughuli zozote za kibinadamu katika mapori hayo.   
 

No comments: