Monday, March 25, 2013

WALIA NA MWEKEZAJI WA MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TANZANIA  ni nchi ambayo imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika kwa ufasaha, taifa hili wananchi wake kwa asilimia kubwa wanaweza kuondokana na umasikini ambao umekuwa ukiitesa jamii nyingi miongoni mwao.

Lakini inashangaza kuona licha ya kuwa na rasilimali hizo kama vile madini ya aina mbalimbali, bado wananchi wake wamekuwa wakilalamika kila kukicha kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Malalamiko hayo yamekuwa yakielekezwa hasa kwa viongozi wa serikali ambao ndio wamepewa dhamana na kusimamia misingi na taratibu nzuri ambazo zitamfanya Mtanzania aweze kunufaika nazo.

Chakusikitisha baadhi ya viongozi wetu ambao ndio wamepewa jukumu hilo, wanaonekana kutozingatia taratibu husika, na kusababisha kelele na hata maandamano yasiyokuwa ya lazima ambayo yanafanywa na wananchi wa eneo fulani ambako kero husika inatokea, yakilenga kudai haki zao.


Katika makala haya napenda kuelezea juu ya mgogoro uliojitokeza wilayani Mbinga  mkoa wa Ruvuma, ambapo wananchi wa kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani humo Januari 29 mwaka huu, walitaka kuandamana kwa masaa kadhaa kupinga kusafirishwa kwa makaa ya mawe ambayo yanachimbwa kijijini humo, wakidai watekelezewe kwanza madai yao ya msingi ambayo mwekezaji husika anaonekana kutoyatimiza.

Maandamano ya mtindo huu ya wananchi kudai madai yao ya msingi ni tatizo ambalo sasa nimeshuhudia limekuwa likijitokeza mara kwa mara hapa nchini, ambapo hata mgogoro wa kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam hali imekuwa bado ni tete hadi leo hii.

Makundi yenye misimamo mikali yamekuwa yakiandamana huko Mtwara na kuitaka serikali itimize ahadi zake ambazo ilizitoa kwa wananchi wale, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi kabla haijasafirishwa, ujenzi wa  miundombinu ya barabara, umeme, kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa wajasiriamali na viwanda vidogo vidogo vya ubanguaji wa korosho lakini havijatekelezwa na ndio maana vinazua gumzo na maandamano yasiyokuwa ya lazima.

Lakini tatizo hili limehamia hapa Mbinga na linatokana na wakazi hao kudai nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa mazingira yakiwemo maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini hayo.

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia kutokana na wachimbaji wa makaa hayo kutiririsha maji yenye mkaa wa mawe kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe kama vile samaki kupoteza maisha.

Wakati hilo linatokea serikali wilayani Mbinga licha ya kutuma wataalamu wake wa mazingira kwenda huko na kufanya upembuzi yakinifu juu ya tatizo hilo, bado majibu hayajatolewa hadi leo hii kwa wananchi wanaoishi jirani na makaa hayo juu ya athari za maji yenye kuchanganyika na madini hayo yanavyoweza kuathiri afya zao, ambayo baadhi yao huendelea kuyatumia na ndio maana walitaka kuandamana kudai haki yao.

Uongozi wa wilaya hiyo ukiongozwa na kamati ya ulinzi na usalama, umeenda kule na kutumia mbinu za kuwatuliza tu wananchi wale na kutoa kauli kwamba madai yao yapo kwenye ngazi husika yanashughulikiwa, baada ya kuonekana hali ya kutaka kuhatarisha amani kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy katika mgodi wa Ngaka, uliopo kijijini humo na wananchi hao kwa ujumla.

Pia jukumu lililochukuliwa na kamati hiyo kwenda huko na kuamuru wachimbaji hao kuzuia maji hayo yenye mchanganyiko na makaa ya mawe yasielekezwe katika mto huo ili kunusuru maisha ya wakazi hao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kwamba vumbi kali la mkaa wa mawe limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa jirani na mgodi huo pale unaposafirishwa kwenda bandari ya Ndumbi iliyopo katika ziwa Nyasa, Kiwira mkoani Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji Tanga kilichopo mkoani Tanga, huenda hali ya kiafya kwa wananchi wale ikawa hatarini endapo hatua husika hazitachukuliwa kwa uharaka.

Nimezungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ntunduaro ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, wakidai kwamba wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na utekelezaji wake unaonesha ukifanywa taratibu.

Wanasema madai yao wanahitaji majibu yatolewe haraka juu ya uchafuzi wa maji ya mto Nyamabeva, ambao maji yake baada ya kuchafuliwa na mkaa wa mawe wataalamu wa mazingira kutoka wilayani humo walikwenda na kuchukua kiasi kidogo kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi wa kina, ili waweze kubaini madhara yake na kwamba hadi sasa ni muda mrefu umepita hakuna majibu yaliyotolewa.

Ofisa mtendaji wa kata ya Ruanda Matilda Nchimbi anasema mgogoro huo wa wakazi kijiji cha Ntunduaro, unatokana pia na kampuni hiyo ya Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko yasiyo na msingi badala yake wamemtaka mwekezaji huyo atimize mambo ya msingi ili kumaliza malumbano hayo.

Wengine wametishia endapo hali hii itaendelea kudumu huenda sasa kukatokea vurugu kubwa kama zile za Mtwara, wakidai wamechoshwa na “longolongo” nyingi ambazo hazina manufaa kwao.

Wakati hilo likiendelea kufukuta, tafiti kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza kwamba katika eneo hilo la mgodi wa makaa ya mawe kampuni hiyo ya Tancoal Energy inamilikiwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy, wameanza kuchimba kisima cha kwanza cha utafiti wa kuzalisha gesi ya makaa ya mawe hapa nchini, katika mradi huo wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo wilayani Mbinga.

Kisima hicho kinachimbwa katika eneo la Mbuyula kijiji hicho cha Ntunduaro na ni miongoni mwa visima vitano vitakavyochimbwa na Tancoal Energy katika mradi huo wa makaa ya mawe wa Ngaka.

Intra Energy ambao ndio wabia wanamiliki asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Tancoal Energy, kila kisima kitakachochimbwa katika eneo hilo kitaweza kuzalisha megawati moja ya umeme, na huenda hapo eneo hilo litazalisha megawati tano kwa siku za hivi karibuni baada ya kukamilisha ujenzi wa mitambo hiyo ya kufua nishati umeme.

Kisima hicho cha kwanza hapa nchini, kuzalisha gesi ya makaa ya mawe, gesi hiyo hupatikana mita zaidi ya 500 kwenda chini ya ardhi ambayo inaitwa Coal Bed Methane.

Wakati uchimbaji huo wa kwanza wa kisima cha gesi ya makaa ya mawe ukiendelea, kampuni ya Tancoal Energy ambayo ipo katika mchakato wa kuanza kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ifikapo mwaka 2015, imetangaza kuongeza kiasi cha kwanza cha umeme utakaozalishwa katika mradi wake wa Ngaka kwa kufikia megawati 240 badala ya megawati 120 zilizotangazwa awali.

Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa mashapo ya mkaa wa mawe ardhini katika eneo hilo, kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa ambapo imethibitika kuwa eneo la Ngaka wilayani Mbinga, lina mashapo mengi ya makaa yanayofikia tani milioni 356.

Endapo hilo litatimia manufaa kwa nchi yetu ni kwamba kutoagiza tena makaa ya mawe kutoka nje ya nchi, na kwamba viwanda vya saruji vilivyokuwa vikinunua makaa ya mawe kwa dola 250 kwa tani, sasa vinapata makaa hayo kwa nusu ya bei hiyo tena mkaa wenye ubora zaidi.

Wakazi wa kijiji cha Ntunduaro walionesha hofu ya kutotimia hilo kwa wakati kutokana na ubabaishaji wanaofanyiwa sasa wa hata kutolipwa fidia zao kwa wakati, huku wakitoa shutuma nzito dhidi ya shirika la TANESCO nchini kwamba ndio chanzo cha matatizo ya upatikanaji umeme.

Wamesema kwamba serikali endapo itatilia mkazo, shirika hilo linaweza kuondokana na umeme wa dharula linaohangaika nao hivi sasa, endapo litaamua kwa dhati kujikita katika uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe katika mgodi huo wa Ngaka hapa wilayani Mbinga na kuunganisha kwenye mtandao wa gridi ya Taifa.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali, kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Nionavyo kukalia kimya malalamiko ya wananchi ndipo ulipo msingi wa matatizo mengi ya nchi hii, kila mtu anapenda na kutaka kusifiwa lakini hakuna anayetaka kupokea lawama au hata wajibu wa kuwajibika wengine wakifanya mabaya kwa niaba yao.

Hii leo sio Tanzania ile ya wanyonge ambao wanataka ukombozi wa kweli katika mambo yanayohusu maisha yao na hawana muda wa kusikiliza hadithi za kulindana na kupuuza malalamiko ya wananchi kama vile tunavyoona sasa ulegevu katika kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika na malalamiko haya ya makaa yam awe Mbinga na hata ile gesi yetu ya Mtwara.

Kuendelea kwa matukio ya wananchi kuandamana kudai haki zao za msingi, kunaonesha serikali yetu kutochukua hatua za haraka pale wananchi wanapowasilisha matatizo yao ya msingi hivyo yatupasa tubadilike tutekeleze mambo kwa vitendo na uhalisia uonekane sio kupiga porojo.

No comments: