Wednesday, March 27, 2013

WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE TUNDURU KUBURUTWA MAHAKAMANI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JUMLA ya kesi 1064 zinazowahusu wazazi na walezi walioshindwa kupeleka watoto wao shule, zimepangwa kuanza kusikilizwa ikiwa ni juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari, wanapelekwa shule.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alisema hayo huku akifafanua kuwa, kesi zote zimepangwa kufanyika katika vijiji husika vya wilaya hiyo.

Nalicho alisema hali hiyo imetokana na wazazi hao kuendelea kukaidi maelekezo ya kupeleka watoto wao shule, hali               iliyoisukuma serikali kumtafuta hakimu, ambaye atahamishia shughuli za mahakama vijijini, ili kurahisisha kazi za utekelezaji wa sheria.


Alisema wilaya yake ina shule 23 za Sekondari jumla ya watoto 2764 walipangiwa kusoma katika shule hizo, lakini cha kushangaza hadi sasa ni wanafunzi 1710 tu ndio walioripoti na kuanza masomo, ikiwa ni sawa na asilimia 63 ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na masomo mwaka huu.

Pamoja na msimamo huo wa serikali wa kuwashitaki na kuwachukulia hatua hizo za kisheria, mzazi atakayebainika kutompeleka mtoto wake shule kwa makusudi atahukumiwa kifungo cha miezi sita jela, kutozwa faini ya Tsh.300,000 au vyote kwa pamoja.

Mkuu huyo wa wilaya kufuatia hali hiyo amewaagiza maofisa tarafa na watendaji wa vijiji kujiandaa kutoa ushahidi dhidi ya kesi walizozifungua, kulingana na maelekezo ya ratiba ya kesi hizo pindi hakimu atakapotembelea na kuendesha kesi hizo katika vijiji husika.

No comments: