Wednesday, March 27, 2013

WANANCHI WA KATA YA NAMASAKATA TUNDURU WALILIA MAJI, WASEMA WAPO TAYARI KUTOA MTU KAFARA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATA ya Namasakata wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,  wametishia kutoa kafara ya mtu achinjwe, kwa ajili ya tambiko litakalosadia wananchi wa kata hiyo, kupata huduma ya maji safi na salama.

Diwani wa kata hiyo Masache Ally alisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kufuatia adha kubwa wanayopata wananchi wake juu ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Alisema wamechoshwa na danadana na ahadi hewa zinazotolewa na serikali juu ya utekelezaji na utatuzi wa tatizo hilo.


“Sisi wananchi wa kata ya Namasakata tumejiandaa na tuko tayari kumtoa hata mtu mmoja miongoni mwetu ili auawe kwa kuchinjwa, na damu yake imwagike na kutumika kama kafara itakayofanikisha kupatikana kwa maji na kuwaondolea kero wananchi wa kata hii”, alisema.

Masache alisema kuwa mbali na vijiji vilivyopo katika kata yake kushirikiana na wataalamu katika utafiti wa jambo hilo, lakini wameishia kuahidiwa kupatiwa kupelekewa miradi ya maji miaka mingi iliyopita, na hakuna utekelezaji uliofanyika mpaka sasa. 

Wakizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa kijiji cha Namasakata  Yusuf Mkali na mkazi wa kijiji cha Mkasale Nuru Hassan walisema kuwa vijiji hivyo, vinakabiliwa na hali mbaya ya upatikanaji wa maji tangu mwaka 1982 kiasi cha kutishia maisha ya wakazi wake.  

Walisema upande wa kijiji cha Mkasale hali ni mbaya zaidi kutokana na kuwepo kwa shubiri, ambayo huwapata akina mama wanaokwenda kujifungua katika kituo cha afya ambapo hulazimika kwenda kuchota maji mtoni umbali wa zaidi ya kilometa mbili, huku wakiwa katika hatari ya kujeruhiwa ama kuuawa na wanyama wakali ambao pia huyatumia maji hayo kunywa.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alimtaka Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo  Paschal Kidiku kushirikiana na wataalamu kufanya utafiti, na kutoa majibu ya uhakika kwa wananchi hao, ili wajue na kutoa maamuzi ya kukihama kijiji chao au la.

No comments: