Tuesday, June 10, 2014

CHADEMA YAPATA PIGO MBINGA WASEMA NI CHAMA AMBACHO HAKINA MWELEKEO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Alhaj Abdallah Bullembo akihutubia leo mamia ya wakazi wa Mbinga mjini katika uwanja wa soko kuu mjini hapa.

Alhaj Abdallah Bulembo akimkabidhi kadi ya CCM aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Desderius Haulle katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa, baada ya kurejesha kadi ya CHADEMA.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Desderius Haulle akiwa amebebwa na Wafuasi wa CCM baada ya kurejesha kadi ya chama hicho pinzani na kuhamia chama tawala. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wake wa chama hicho wilayani humo Desderius Haulle kujitoa uanachama na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tukio hilo limejitokeza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soko kuu uliopo mjini hapa, ambao ulikuwa ukihutubiwa na Mwenyekiti wa taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Alhaj Abdallah Bulembo.

Sambamba na hilo katika mkutano huo pia alijitokeza mwanachama mmoja wa Chama Cha wananchi CUF, Maria Ndimbo naye alirejesha kadi yake ya chama hicho na kuhamia CCM.

Haulle alirudisha kadi ya CHADEMA na kukabidhiwa ya CCM, ambapo alipopewa nafasi ya kuzungumza alisema amechoshwa na sera za chama hicho pinzani ambazo hazina utekelezaji.

“Leo nimeamua kurejesha kadi hii na kuhamia katika chama hiki tawala kwa sababu nafahamu mambo mengi yanayofanywa na CHADEMA, hivyo nilivumilia kwa muda mrefu lakini leo imefikia mwisho wake naomba tuungane pamoja tujenge taifa letu”, alisema Haulle.


Alisema chama hicho pamoja na kuitwa ni cha kidemokrasia, hakuna ukweli wowote juu ya hilo na badala yake kimekuwa kikiendeshwa kiukabila ambapo mtu au kiongozi yeyote anayetoka nje ya mikoa ya Kaskazini hathaminiwi ndani ya chama hicho.

Pamoja na mambo mengine akihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika katika eneo la uwanja wa soko hilo mjini hapa, Bulembo alimpongeza Haulle kufuatia uamuzi wake wa kurudi CCM chama ambacho kinafuata misingi bora ya kidemokrasia bila ubaguzi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, alisema ubinafsi na ukabila ndani ya CHADEMA umejionyesha wazi Bungeni ambapo kila kiongozi aliye juu anaye ndugu yake ambaye ni Mbunge ndani ya bunge.

Bulembo aliwataka wananchi ambao wamepotea njia na kwenda upinzani, warudi CCM kwani ndicho chama chenye sera zinazolenga kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania na kudumisha amani na utulivu uliodumu tangu nchi ilipopata uhuru.





No comments: