Tuesday, June 10, 2014

UNYAMA WA KUTISHA: WATOTO WATEKETEA KWA MOTO BAADA YA KUFUNGIWA NDANI


Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

SIMANZI na majonzi vilitawala katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia wanafunzi wawili wakazi wa mji huo wanaosoma shule ya msingi Mbamba bay wilayani humo kufariki dunia, baada ya kuteketea kwa moto katika chumba walichokuwa wamelala ambacho inadaiwa kuwa walifungiwa nje kwa kufuli na kuwafanya washindwe kujiokoa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari vimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 23 mwaka huu majira ya usiku, ambapo chanzo cha moto huo hadi sasa hakijulikana na kwamba watoto hao walifungiwa kwenye chumba ambacho ni duka la bidhaa mbalimbali ambalo vitu vilivyokuwa ndani yake navyo viliteketea kabisa.

Watoto waliokumbwa na mkasa huo ni Sharifa Nurudin (13) ambaye anasoma darasa la saba na Ismail Nurudin (11) wa darasa la tano katika shule hiyo, imedaiwa kuwa walikuwa wakifungiwa mara kwa mara kwenye duka hilo lenye jina maarufu ‘Kwa mjomba Nuru’ nyakati za usiku, kwa lengo la kulinda  mali zilizomo ndani yake.

“Watoto hawa walikuwa siku zote wanafungiwa nje na kufuli na baba yao mzazi Nurudin Mohamed, licha ya watu kumweleza acha kuwatumikisha watoto hawa kwa mtindo huu alikuwa hataki kusikia na leo watoto wamepoteza maisha kwa sababu ya ujinga wa huyu baba”, alisema mama mmoja mkazi wa mji mdogo wa Mbamba bay ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakazi wa mji huo walifafanua kuwa watoto hao walikuwa wanaishi na mama yao wa kambo, waliyemtaja kwa jina la Anna Pilly ambapo muda mwingi walikuwa wakitumikishwa kufanya kazi ngumu na kukosa malezi bora.

Walibainisha kuwa walikuwa wakiishi na mama huyo katika mazingira magumu, baada ya mama yao mzazi Fulale Msumba ambaye hivi sasa anaishi Songea mjini, kuachana na huyo baba yao miaka kadhaa iliyopita.

Mazishi ya miili ya watoto hao imefanyika katika makaburi yaliyopo hapo Mbamba bay Mei 24 mwaka huu, majira ya mchana.

Aidha Kamanda wa polisi wilayani Nyasa Amiri Mganga hakuweza kupatikana ofini kwake, lakini alipoulizwa kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hawezi kutolea maelezo ya kina kwa sababu yupo katika ziara ya kikazi.

“Unajua hivi sasa unavyonipigia nipo kati kati ya ziara ya katibu wa wazazi taifa, nitashindwa kukupatia maelezo juu ya jambo hili tupo na mgeni huyu wa chama cha mapinduzi (CCM) hapa wilayani kwetu, naomba nitafute muda mwingine”, alisema Mganga.

Hata hivyo gazeti hili lilipozungumza na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, kamishina msaidizi wa polisi Akili Mpwapwa alisema kuwa yeye hana taarifa juu ya tukio hilo, mpaka atakapowasiliana na mkuu huyo wa kituo cha polisi wilaya ya Nyasa.

No comments: