Wednesday, June 11, 2014

KASI YA UPIMAJI VVU MBINGA NI NDOGO BULEMBO AUTAKA UONGOZI WA WILAYA KUHAMASISHA WANANCHI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Alhaj Abdallah Bulembo, akipokea vazi na kadi ya chama cha upinzani kutoka kwa mama Maria Ndimbo ambaye alikuwa mfuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) na kuhamia CCM. Tukio hilo lilifanyika katika uwanja wa soko kuu mjini hapa.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Alhaj Abdallah Bulembo, amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inaweka mikakati madhubuti ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Agizo hilo lilifuatia baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, ambayo ilionesha kwamba watu 300,000 tu ndio waliopima afya zao katika kipindi cha mwaka 2013 hadi mwaka huu, ili waweze kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya ukimwi kiasi ambacho ni kidogo kutokana na wilaya hiyo kuwa na watu wengi.

“Nimegundua hapa hamasa ya upimaji VVU ni ndogo ukizingatia kwamba Mbinga kuna watu wengi sana, kuanzia sasa tengenezeni hili liwe kama agenda katika vikao vyenu sio tuna kaa kimya tuweke mazingira ambayo yenye programu ya muda mrefu na endelevu”, alisema Bulembo.


Aidha kwa wilaya hiyo kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo imekuwa kubwa ambapo imefikia asilimia 7 tofauti na takwimu za kitaifa asilimia 5, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuweza kupunguza kasi hiyo.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti huyo aliutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga kupitia idara yake ya afya, kuweka utaratibu wa kusambaza kondomu kwenye nyumba za kulala wageni na suala hilo liwe la lazima na sio hiari.

“Hoja ya kuwa na kondomu katika kila nyumba za kulala wageni halina mjadala hususan kwa hapa mjini, ni jambo ambalo mnapaswa kuliweka katika mikakati yenu ya wilaya kufanya hivi tunaweza kupunguza kasi hii ya maambukizi”, alisema.

Kwa upande wake akijibu hoja za Mwenyekiti huyo wa Wazazi Taifa, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Ngaga alisema atatekeleza hilo haraka kwa kushirikiana na timu yake ya wilaya, ikiwemo kuweka mikakati ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kuwapa elimu juu ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

No comments: