Saturday, June 7, 2014

MALUMBANO YA VIGOGO MBINGA YAENDELEA KUIBUA MAPYA

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

























Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

IMEBAINIKA kwamba kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima, kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya hiyo, askari polisi na madereva wa pikipiki.  

Hali hiyo imefikia hatua kwa baadhi yao kudaiwa kunyanyasa madereva wa pikipiki wa wilaya hiyo huku uongozi wa umoja wa madereva hao (UWAMBI) uliopo wilayani hapa, ukijipanga kwenda kwa mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu ili waweze kufikisha kilio chao.

Ukweli juu ya mgogoro huo ulijitokeza hivi karibuni katika kikao kilichoketi Mei 22 mwaka huu mjini hapa, endelea kufuatilia mkasa huu kama ifuatavyo;

UWAMBI wanena kwenye kikao hicho:

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Katibu wa umoja huo Bern Mangeni mbele ya mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kwa niaba ya wanachama wenzake alisema wamekuwa wakinyanyaswa na Ofisa mmoja wa usalama wa taifa wilayani hapa (jina tunalo) na Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Justine Joseph.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya sisi tutaendelea kusonga mbele ngazi ya juu kwa sababu inaonesha umeshindwa kutusaidia, tumebaki kwenye hali ya sintofahamu juu ya tatizo hili”, alisema Bern Mangeni.

Walalamikia juu ya Manyanyaso:

Mangeni katika kikao hicho anasema Ofisa huyo wa usalama anadaiwa kumgonga mjini hapa dereva wa pikipiki Hassan Said, kutokana na uendeshaji wa gari lake la ofisi awapo barabarani sio wakistaarabu, huku muda mwingi  amekuwa akiendesha kwa mwendo kasi hata akiwa katika maeneo ya hapa mjini.

Alieleza kuwa baada ya kumgonga alipiga simu polisi kwa lengo la kuita askari waje wamkamate dereva huyo wa pikipiki, huku akiwa amemkamata na kumtolea vitisho vya hapa na pale kwamba dereva huyo wa pikipiki alikuwa na makosa barabarani wakati sio kweli, ambapo askari hao walipowasili eneo la tukio walimchukua Hassan Said na kwenda kumweka mahabusu. 

Ushuhuda watolewa:

Katika kikao hicho Hassan Said alitoa ushuhuda mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambapo alisema wakati anagongwa na gari na Ofisa usalama huyo, alishuka katika gari lake na kumkamata kisha kumtandika makofi, huku akimtishia na silaha aliyoitaja mbele ya kikao hicho kuwa ni bastola.

Wakati tukio hilo likiendelea alisema alikuwa akipiga simu akiita askari polisi waje eneo la tukio ambao baada ya kuwasili walimkamata dereva huyo wa pikipiki na kumweka mahabusu kwa siku mbili, huku dhamana ikizuiliwa hadi alipopelekwa Mahakamani ambako nako ilikuwa ni tatizo kupewa dhamana na akaishia kusota mahabusu kwa muda wa miezi miwili huku kesi yake akihudhuria mahakamani kwa kadiri ya siku ilivyokuwa ikitajwa hadi alipohukumiwa.    

Hassan Said alisema wakati kesi inaendelea katika mahakama ya wilaya ya Mbinga licha ya kueleza ukweli juu ya tukio lenyewe, ilishindikana kuweza kujinasua kutokana na mpango mchafu uliopangwa wa kuendelea kumkandamiza aishie jela.

“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya askari mmoja ambaye namtambua kwa jina moja la Seif, alikuja kwangu na kuniambia kwamba afisa usalama alikuwa anataka hela ili aweze kufuta kesi ambayo ilifunguliwa kule mahakamani,

“Mimi mwenyewe niliwasiliana na ndugu zangu wakati nikiwa bado mahabusu niliwaagiza wauze baadhi ya vitu vyangu; kitanda changu cha kulalia, godoro, redio, Tv, ili niweze kupata fedha nijinasue na mkasa huu”, alisema Hassan Said.

Alifafanua kuwa baada ya ndugu zake kuuza vitu hivyo wakati yeye akiwa bado mahabusu, waliweza kufanikiwa kupata fedha tasilimu shilingi 500,000 ambazo baadae alikabidhiwa askari huyo aliyemtaja kwa jina la Seif, ili akazipeleke kwa Ofisa usalama huyo na yeye aweze kujinasua katika kesi hiyo.

Lakini cha kushangaza licha ya kutoa fedha hizo hakuna kitu kilichoendelea, zaidi ya yeye kuendelea kusumbuka na kesi ambayo ilikuwa ikimkabili na hatimaye aliishia kwenda kutumikia kifungo jela miezi sita.

Vilevile alisema mkasa huo alikumbana nao mwaka 2012 ambapo alisota mahabusu kwa miezi miwili hadi kesi yake ilipohukumiwa na kufungwa tena jela miezi sita, na baadaye alipomaliza kifungo chake alirudi nyumbani kuendelea na majukumu yake ya kazi za kila siku.

Mlalamikaji:

Wakati Hassan Said anatoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, bado alionekana kutoeleweka ambapo Ngaga alikuwa akionesha kuendelea kumtetea kiongozi huyo wa usalama ambaye amepewa dhamana ya kushikilia mhimili wa dola wilayani humo, kuhakikisha kwamba wananchi wake wanakuwa salama wakati wote.

Mkuu wa polisi wilaya ya Mbinga:

Madereva hao wa pikipiki walizidi kutoa malalamiko yao dhidi ya askari wa barabarani, ambapo walisema wamekuwa wakitozwa faini za makosa ya barabarani bila kukatiwa stakabadhi (risiti).

Walisema pamoja na kufikisha kilio chao kwa mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Justine Joseph hakuna utekelezaji unaonesha kuzaa matunda, badala yake muda mwingi anaonekana kuwatetea askari wake pale anapofikishiwa malalamiko.

Diwani kata ya Mbinga mjini athibitisha:

Aidha pamoja na Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda kuthibitisha juu ya matukio wanayotendewa madereva hao wa pikipiki wilayani humo, bado alionekana kutoeleweka na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga na kufikia hatua kikao hicho kuvurugika na kutofikia muafaka.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga:

Baada ya Diwani huyo kuonesha kwamba anaeleza ukweli juu ya tukio hilo, Senyi Ngaga alikuwa na jazba huku akisema “diwani leo unanisaliti...............” na kwamba kufuatia hali hiyo kikao hicho ambacho kilidumu kwa muda wa masaa manne kilivunjika bila kupatiwa ufumbuzi.

No comments: