Wednesday, June 4, 2014

MBINGA WACHUKIZWA NA MALUMBANO YA VIGOGO WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA KATI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameshauri na kulitaka Jeshi la polisi mkoani humo, lijiepushe  kufanya kazi zake kwa kusikiliza majungu na maneno ya fitina katika utendaji wake wa kazi za kila siku na endapo wasipozingatia hilo, mwisho wa siku huenda jeshi hilo linaweza kujikuta likabaki na askari wachache wasiokuwa na sifa au weledi.

Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima ambayo yanaendelea kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya na askari polisi.

Walieleza kuwa hali hiyo imesababisha hata baadhi yao kutoelewana ambapo kigogo mmoja ambaye ni Ofisa usalama wa taifa (jina tunalo) na Mkuu wa polisi wa wilaya ya Mbinga (OCD) Justine Joseph wanadaiwa kutoelewana na Mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo Geofrey Ng’humbi.

Walisema malumbano ya vigogo hao hayana faida katika jamii na yanatokana na Ng’humbi kufanya kazi zake kwa kuzingatia utawala bora, hivyo kuonekana kuwa mwiba kwa wenzake.


Uchunguzi uliofanywa na timu ya Waandishi wa habari umebaini kuwa viongozi hao wa ngazi ya juu wilayani hapa ambao wanalalamikiwa ndio wanaodaiwa kujenga fitina, majungu na njama za hapa na pale huku mambo ya chini kwa chini yakisukwa na kusababisha Mkuu huyo wa kituo cha polisi Mbinga, aonekane kwamba ni tatizo hatimizi majukumu yake ya kazi ipasavyo na kusababisha ahamishwe kwenda makao makuu ya polisi mkoani Ruvuma yaliyopo Songea mjini.

Vilevile walieleza kuwa ni vyema serikali ikachunguza jambo hili kwa makini, na ikiwezekana uhamisho huo ufanywe kwa hata jeshi nzima la polisi wilayani Mbinga kwa ngazi ya viongozi, kwa kile walichodai kuwa mkuu huyo wa polisi wa wilaya hiyo amekuwa akishirikiana na ofisa huyo wa usalama kujenga uonevu kwa wananchi wa kawaida ambao hawana tatizo lolote.

Kwa mujibu wa malalamiko yaliyotolewa katika kikao kati ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga na Madereva wa Pikipiki wilayani humo, ambacho kiliketi hivi karibuni kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa walisema licha ya Ngaga kufikishiwa ofisini kwake malalamiko yao dhidi ya vigogo hao hawaoni utekelezaji uliozaa matunda.

Madereva hao walieleza kuwa endapo hatua husika zisipochukuliwa wapo tayari kwenda ngazi ya juu, ili waweze kupeleka malalamiko yao na yaweze kufanyiwa kazi.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, sisi tupo tayari kwenda ngazi ya juu, maana inaonekana hapa hakuna muafaka tuliofikia kwa sababu muda mwingi umekuwa ukiwatetea hawa watu wakati sisi wanatunyanyasa”, alisema Bern Mangeni Katibu wa umoja wa waendesha pikipiki wilayani Mbinga. (UWAMBI)

Waendesha pikipiki hao ambao walionesha kukerwa na hali hiyo walizidi kumnyoshea kidole ofisa usalama huyo wakidai kwamba hata uendeshaji wa gari lake la ofisi awapo barabarani sio wakistaarabu, ambapo muda mwingi  amekuwa akiendesha kwa mwendo kasi hata akiwa hapa mjini na kunusurika kusababisha ajali au kugonga watu.

Walisema kama ataendelea kufanya hivyo itakuwa sio busara kwa kiongozi wa serikali kama yeye ambaye amepewa dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wa Mbinga wanakuwa katika hali ya usalama, hivyo ni vyema arakebishe tabia hiyo na kuleta taswira nzuri katika jamii.

Kwa upande wa OCD Justine Joseph walifafanua kuwa aache kujenga makundi yasiyokuwa ya lazima kwa jeshi la polisi wilayani humo, na endapo tatizo hilo litaendelea walitishia wakisema watadhamiria kugomea shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo suala la polisi jamii na ulinzi shirikishi.

Walifafanua kuwa wamepanga kwenda kumuona Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu na Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Kamishina msaidizi wa polisi Akili Mpwapwa ili kumueleza masikitiko yao  juu ya tabia na mienendo ambayo inaendelea kufanywa na viongozi hao wilayani Mbinga.

“Tutaenda kumuona mkuu wa mkoa tunajua ni kiongozi shupavu na mpenda haki licha ya kuelezwa majungu mengi juu ya mgogoro huu unaoendelea hapa Mbinga, tunaamini amedanganywa hakuna ukweli halisi aliopewa mezani kwake juu ya mahusiano mabaya ya viongozi hawa wawili”, walisema.

Hata hivyo katika kikao hicho hapakufikiwa muafaka wowote kutokana na waendesha pikipiki hao, kuonekana kuja juu na kutoridhika na mwenendo mzima wa mambo wanayofanyiwa.

Nao baadhi ya askari ambao pia hawakutaka kutaja majina yao wamesikitishwa na hatua ya jeshi la polisi mkoani humo kumuhamisha Mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo, Geofrey Ng’humbi ambaye walisema alikuwa msaada mkubwa kwao kwa kila jambo, na sababu za kumhamisha kwake walieleza kwamba ni kwa mtindo wa majungu na hawaoni sababu ya msingi badala yake ni uonevu na mbinu ambazo zilipangwa na watu wachache.

Waliongeza kuwa uongozi husika wa polisi ungefanya busara kama ni uhamisho kuwaondoa  wote hao lakini siyo ilivyofanya kumuhamisha mtu mmoja kwani haukumtendei haki japo kuwa uhamisho ni sehemu ya mtumishi wa umma.


No comments: