Tuesday, June 24, 2014

MGOGORO WA MIPAKA NA ARDHI: MKUU WA WILAYA YA NYASA MKOANI RUVUMA ALALAMIKIWA NA WANANCHI WAKE


 
Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Ernest Kahindi, akiwa ofisini kwake wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

SAKATA la mgogoro wa kugombea ardhi na mipaka katika kitongoji cha Mshangano kijiji cha Liparamba tarafa ya Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, limechukua sura mpya kufuatia Wakazi wa maeneo hayo kumlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi huku wakimnyoshea kidole kwamba ameshindwa kumaliza mgogoro huo kwa kufuata taratibu husika  ikiwemo ridhaa ya wananchi, badala yake  anatumia nguvu kubwa  kunyanyasa viongozi wa kijiji hicho.  

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati  tofauti kijijini hapo, wakazi hao walisema Kahindi amefikia hata hatua ya kumweka mahabusu kwa siku tatu katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Nyasa, Mwenyekiti wa kijiji Joseph Komba bila kosa lolote huku akizuia dhamana.

Uchunguzi umebaini kuwa Mwenyekiti huyo aliwekwa mahabusu kuanzia siku ya Ijumaa Juni 20 na kudhaminiwa Juni 23 mwaka huu majira ya jioni, ambapo kufikia saa 11 jioni siku hiyo ndipo alichukuliwa maelezo na kuambiwa atafute mtu wa kumdhamini huku akipewa usumbufu wa kuendelea kuripoti kila siku katika kituo hicho cha polisi.


Kadhalika Mkuu wa Polisi wilaya ya Nyasa (OCD) Amiri Mganga alipopigiwa simu ili aweze kuzungumzia hali hiyo alikiri kushikiliwa kituoni hapo Mwenyekiti huyo na kusema; “hivi sasa siwezi kuzungumzia lolote nimebanwa na kazi nipo bize kidogo nipigie muda mwingine, na kuishia kukata simu".

Taarifa zinaeleza kuwa kuwekwa mahabusu kwa Mwenyekiti Komba kunatokana na kujenga msimamo wake wa kutotaka kugawa ardhi na mipaka ya kijiji bila kufuata taratibu husika, hivyo kuonekana kuwa mwiba kwa Mkuu huyo wa wilaya ya Nyasa.

Imeelezwa kuwa mtu ambaye  anazua mgogoro huo wa ardhi na mipaka katika kijiji cha Liparamba, ni Mwanajeshi mstaafu Florian Geuza ambaye alipoulizwa alisema kuwa maeneo anayoyadai ni ya kwake, familia yake na ndugu zake.

Geuza alisema yeye eneo hilo analolidai kijijini hapo linazaidi ya ekari 300 ambapo aliachiwa urithi na baba yake mzazi miaka mingi kabla hajafariki dunia.

Katika hatua nyingine kwa upande wao wananchi walisema kitendo hicho kinachofanywa na Mkuu huyo wa wilaya ya Nyasa hakipaswi kuvumiliwa hata kidogo, hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati ili kuweza kuepusha na kunusuru kutokea kwa mauaji ya kugombea ardhi na mipaka, kati ya wananchi wa kitongoji hicho na Mwanajeshi huyo mstaafu.

Walieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa kiongozi wa ngazi ya juu kutumia nguvu na unyanyasaji kwa viongozi wa maeneo hayo, wakati wenye maamuzi ya ugawaji wa maeneo ya kijiji ni wananchi wenyewe kupitia vikao halali vilivyoketi kisheria na sio vinginevyo.

Walisema kuwa mgogoro huo wa kugombea mipaka umedumu kwa miaka mitatu sasa, licha ya viongozi husika kuwa na taarifa juu ya tatizo hilo lakini kila kukicha kumekuwa ukifanyika mchezo mchafu ambao huzalisha matatizo yenye kuhatarisha misingi ya amani katika kijiji cha Liparamba.

Walifafanua kwamba hali hiyo inatokana tu na mstaafu huyo wa JWTZ kuvamia maeneo ya wananchi hao na kusema kuwa ni ya kwake anayamiliki tokea mwaka 1952 jambo ambalo linazua utata kila kukicha.

Pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kuanzia kwenye ngazi ya kata na wilaya, walisema bado hakuna dalili zinazoonesha kuzaa matunda badala yake muda mwingi viongozi wa wilaya hiyo wamekuwa wakiegemea upande wa Mwanajeshi huyo.

“Hali hii inasababisha tuishi kwa hofu na mashaka juu ya jambo hili, hasa pale tunapolazimika kwenda kwa ajili ya uzalishaji wa mazao yetu shambani”, alisema Sikitu Kawago mkazi wa kijiji cha Liparamba.

Naye mkazi mmoja wa kijiji hicho Lucas Ngonyani alisema kama uongozi wa wilaya hiyo utaendelea kufumbia macho tatizo hilo, kuna uwezekano wa kuwepo kwa mapigano na kusababisha umwagaji wa damu.

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Liparamba Denice Manyahi alipohojiwa ofisini kwake alikiri kuwepo kwa hali ya sintofahamu ya kugombea ardhi na mipaka, huku akisema tayari hali imekuwa mbaya kiasi ambacho inatakiwa hatua za busara zenye kufuata misingi na taratibu za kisheria ifuate ili kuweza kuleta amani kijijini hapo.

Manyahi alieleza kuwa hali hii inatokana na uzembe husika unaofanywa na viongozi wachache wilayani Nyasa, hivyo huenda tatizo hilo lisipotatuliwa kwa uharaka inaweza kutokea maafa makubwa ambayo baadaye kuigharimu serikali.

Naye Ofisa mtendaji wa kata ya Liparamba Philemon Ngaponda alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi, alithibitisha kuwepo kwa mgogoro wa kugombea ardhi na mipaka huku akiongeza kwamba taratibu husika zimeanza kuchukulia ili kuweza kumaliza tatizo hilo.

“Ni kweli mgogoro upo tunachosubiri ni maamuzi ya viongozi wa ngazi ya juu, mimi siwezi kuzungumzia sana juu ya jambo hilo tusubiri maamuzi yatakayotolewa”, alisema Ngaponda.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kahindi alipoulizwa juu ya tatizo hilo la wananchi wa kijiji cha Liparamba wilayani humo, alisema hawezi kuzungumzia lolote kwa sasa huku akiongeza kuwa linashughulikiwa kisheria.

Hata hivyo alipotakiwa kutolea ufafanuzi wa malalamiko ya kunyanyasa viongozi wa kijiji hicho alisema; “nimekuambia  naomba uvute subira Nyandindi, hili suala linashughulikiwa kisheria utapata taarifa kamili kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote”.

No comments: