Saturday, May 31, 2014

WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wa shule  ya sekondari  Agustivo iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,  wametakiwa kuongeza juhudi katika masomo yao ili waweze kutimiza malengo waliyonayo katika maisha na kuacha kujiingiza kwenye mambo yatakayowaharibia malengo yao.


Ushauri huo umetolewa na mfanyabiashara maarufu  mkoani Ruvuma Abbas Herman, alipokuwa akizungumza  na wazazi na wanafunzi kwenye mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo huku akisisitiza umuhimu wa elimu.


Katika sherehe hizo za kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita, mfanyabiashara huyo pia aliwazawadia wanafunzi 14  kiasi cha shilingi 25,000  kila mmoja  waliokuwa wamefanya vizuri katika masomo yao na  kiasi cha shilingi 1,000,000 kwa ajili ya shule hiyo ikiwa ni zawadi ya kufanya vizuri kitaaluma mkoani Ruvuma.




Alisema wilaya ya Mbinga ni kati ya wilaya chache hapa nchini zenye fursa nyingi ambazo zinatoa nafasi kwa vijana kujiendeleza zaidi kielimu, kwani hata historia inaonesha kuna idadi kubwa ya viongozi waliosoma na kushika nafasi za juu hapa nchini lakini tatizo baadhi ya vijana wenyewe  hawataki kujituma na kuzingatia masomo yao.


“Nawasihi sana vijana ongezeni juhudi katika masomo yenu, na nyinyi tunaowaaga leo hakikisheni mnatumia muda huu kujiandaa na masomo ya juu zaidi badala ya kuridhika na hapa mlipofikia kwani kumbukeni elimu haina mwisho”, alisema Abbas.

Aliongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo imeanza kufungua milango ya uwekezaji, hivyo inahitaji wasomi wengi watakaofanya kazi katika sekta mbalimbali na ambao wanaelimu ya juu.


Hata hivyo aliwataka kujitambua na kuelewa kuwa vijana ndiyo nguzo kuu ya uchumi katika nchi, kwa hiyo ni vyema wasome kwa bidii ili taifa lipate wasomi wengi zaidi na wazalendo jambo ambalo  litasaidia kuwa na wataalamu wengi na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha wanacholipwa wataalamu wa fani mbalimbali wa nje.

No comments: