Sunday, May 11, 2014

NGAGA AWAWEKA KITIMOTO VIGOGO WA HALMASHAURI YA MBINGA

Na Muhidin Amri,

Mbinga.


MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amegeuka mbogo na kuwaweka kiti moto baadhi ya vigogo wa wilaya hiyo kufuatia kuwepo kwa matokeo mabaya, yaliyopatikana kwenye maeneo wanayo yaongoza katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana. 

Ngaga alisema hali hiyo imesababisha wilaya hiyo kushika nafasi ya pili kimkoa  kinyume na maadhimio waliyojiwekea ya kushika nafasi ya kwanza  katika mtihani huo.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wa kikao cha tathimini ya elimu ambapo Mkuu huyo wa wilaya hakuridhishwa na hali ya ufaulu katika kata zinazoongozwa na vigogo hao ambao ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga Christantus Mbunda, ambaye ni diwani wa kata ya Mbangamao.

Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy diwani wa kata ya Kipapa na diwani wa kata  ya Ngima Winfrid Kapinga ambaye ni makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngima wote kupitia tiketi ya chama hicho.


Ngaga aliwataka viongozi hao  watoke mbele wakiambatana na maafisa tarafa, walimu wa kuu wa shule zilizofanya vibaya pamoja na watendaji wa kata ambazo nazo zilichemsha katika matokeo hayo  na kuwaita viongozi hao mbele ya wajumbe wengine wa kikao hicho   ili waeleze sababu iliyofanya kata zao kupata matokeo mabaya huku wao wakiwa viongozi wa ngazi ya juu katika wilaya hiyo.

“Jamani nimewaita mbele siyo kwa lengo la kuwahukumu  au kuwafedhehesha hapana…….. bali ninachohitaji  kusikia kutoka kwenu nyinyi wenyewe sababu kubwa iliyowafanya mpate matokeo mabaya   katika kata zenu mkiwa viongozi tena wa ngazi ya juu katika wilaya yetu, matokeo  haya hayaridhishi hata kidogo hivyo ni  lazima wote kwa pamoja tutafute njia ya kumaliza tatizo hili kwani ni kinyume na maadhimio yetu ya mwaka uliopita”, alisema Ngaga.

Katika matokeo hayo kata ya Mbangamao ambayo  diwani wake ni  Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi ilishika nafasi ya mwisho katika matokeo hayo kiwilaya  kwa kupata  alama 20 ambayo ni chini ya wastani unaotakiwa huku ikifuatiwa na kata ya  Ngima na  Kipapa ambazo nazo zilipata alama chini ya  11 hivyo kuwa miongoni mwa kata zilizofanya vibaya zaidi katika mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi kitaifa.

Kata nyingine zilizofanya vibaya zaidi ni Nanswea, Kipata, Kitanda, Kihangamahuka, Kihungu, Mpepai, Mbuji na kata ya Kitumbalomo ambapo Mkuu huyo wa wilaya aliwataka viongozi wa kata  hizo  kueleza sababu kubwa iliyopelekea kata zao kuvurunda ili kupata majawabu ya  kumaliza tatizo hilo la ufaulu kwa kuwa matokeo hayo yanaitia aibu wilaya hiyo.

Aliwaagiza kuhakikisha wanamaliza changamoto zilizosababisha kupata matokeo mabaya, ili mwakani ziweze kufanya vyema na kuisogeza wilaya ya Mbinga hadi nafasi ya kwanza kimkoa jambo ambalo kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya  linawezekana kutokana na rasilimali  mbalimbali zilizopo.

Licha ya kuwataka watoe  sababu za kufanya vibaya lakini pia   kueleza mikakati waliyonayo kukabiliana na tatizo la utoro, ukosefu wa chakula cha mchana, nyumba za walimu, madarasa na hata matundu ya vyoo  ambazo zimeonekana kuwa ni moja ya tatizo la kufanya vibaya katika mitihani iliyopita.

Aidha katika kikao hicho, ambacho kilivutia wajumbe wengi kutokana na namna mkuu huyo  wa wilaya  pamoja  na wajumbe walivyokuwa wakichangia hoja zao, walishindwa kuficha hisia zao kwa kumpongeza afisa elimu ya msingi Daud Mkali  kutokana ubunifu wake hasa katika  kuanzisha makambi kwa watoto wa darasa la nne na saba, pamoja na shule zilizofanya vizuri ambapo shule sita kati ya kumi bora kimkoa zimetoka katika wilaya ya Mbinga.

No comments: