Friday, May 2, 2014

TATIZO LA MIMBA LATISHIA USTAWI WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA ELIMU MBINGA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TATIZO la mimba mashuleni kwa shule za msingi na sekondari wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lisipotafutiwa mbinu ya kudhibitiwa mapema, hakika maendeleo katika sekta ya elimu wilayani humo huenda yakadorola.

Imefafanuliwa kuwa wazazi na walimu katika shule husika ndio chanzo kikuu cha tatizo hilo ambapo kwa kiasi kikubwa, wamekuwa wakifumbia macho kwa kutowachukulia hatua za kisheria watu wanaohusika kuwapatia wanafunzi wa kike ujauzito.  

Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoani humo, walisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambaye alikuwa Mwenyekiti katika kikao cha tathimini ya elimu, kilichoketi katika ukumbi wa Jimboni uliopo mjini hapa.


Akizungumza katika kikao hicho Ngaga alionesha kusikitishwa na tatizo hilo, ambapo alisema kwa mwaka wamekuwa wakipata kesi za mimba zaidi ya 160 na hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayekamatwa kutokana na wazazi kutotoa ushirikiano wa kutosha katika vyombo vya sheria ambavyo vinashughulikia tatizo hilo.
 
“Tatizo la mimba katika wilaya yetu ni kubwa mno ukijumlisha kwa shule za msingi na sekondari, kwa mwaka tumekuwa tukizalisha mimba nyingi haiwezekani watoto wetu wa kike wanaendelea kupewa mimba halafu tunakaa kimya”, alisema Ngaga.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, pia aliwanyoshea kidole Watendaji wa vijiji na kata kwa kile alichoeleza kuwa, tatizo hilo la mimba wamegeuza kama ni mtaji wao wa kujipatia fedha na kumaliza mambo kienyeji, huku wakiacha kuwachukulia hatua wahusika.

“Wazazi tusikubali kurubuniwa kwa vijipesa vidogo vidogo halafu watoto wetu wa kike wanaharibika kwa kukatisha masomo yao kutokana na tatizo hili”, alisema.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbinga Damas Kayera alieleza kuwa , watoto wengi wanaokwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya hiyo ni mabinti wadogo wadogo, ambao wamekatisha masomo yao shuleni kutokana na kupewa ujauzito.

“Mheshimiwa mwenyekiti wa kikao hiki, kesi nyingi za mimba ninazozipokea pale hospitali ni za watoto hasa wa kidato cha pili”, alisema Kayera.

Wadau hao wa elimu walijiwekea mkakati wa kuhakikisha kwamba hatua madhubuti sasa zichukuliwe dhidi ya wahusika wenye kusababisha tatizo hilo, ikiwemo kufikishwa Mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

No comments: