Sunday, May 4, 2014

TATIZO LA MAJI MBINGA MBIUWASA YANYOSHEWA KIDOLE

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga.



















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

UHABA wa maji ni tatizo ambalo limekuwa likiendelea kutesa Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, na kusababisha wakazi hao kuinyoshea kidole Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (MBIUWASA) iliyopo katika mji huo, ambayo ndio tegemeo kubwa katika utoaji wa huduma hiyo muhimu.

Kufuatia hali hiyo wameitaka Mamlaka kuhakikisha kwamba inatatua kero hiyo mapema, ili wakazi hao waweze kuondokana na adha wanayoipata sasa ya mgao mkali wa maji.

Walisema ni jambo la kushangaza mji huo kukosa maji kwa kile walichoeleza kuwa, ni kipindi cha masika na maji yamekuwa mengi kiasi ambacho hawakutakiwa kukumbwa na karaha hiyo, huku wakifafanua kuwa muda mwingi maji hayo ya mgawo yamekuwa yakielekezwa katika nyumba za vigogo huku watu wa kawaida wakiendelea kuteseka.

Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi mjini hapa, huku wakidai kuwa wakati mwingine inawalazimu kufuata maji umbali mrefu katika vijito vidogo vidogo, ambavyo huzunguka mji wa Mbinga.


Uchunguzi uliofanywa na Gwiji la matukio Ruvuma, umebaini kuwepo kwa tatizo hilo ambalo sasa limedumu kwa muda mrefu na mgawo mkubwa wa maji umekuwa ukiendelea kufanyika, licha ya chanzo kikuu cha maji Ndengu, ambacho hutumika kuleta maji mjini hapa kuwa na maji mengi.

Meneja wa MBIUWASA Patrick Ndunguru alipoulizwa juu ya tatizo hilo alikiri kuwepo na kusema kwamba, limetokana na bomba kuu la kuleta maji katika mji huo kuwa na tatizo la kiufundi ambalo limekuwa likiwatesa mara kwa mara.

Ndunguru alisema bomba hilo ni chakavu na kwamba mradi huo wa maji ambao ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa mji huo, haujajengwa katika kiwango kinachotakiwa ili kuweza kukidhi mahitaji halisi.

“Tatizo letu kubwa katika mradi huu haukujengwa katika ‘standard’ inayotakiwa, mpaka juzi tuligundua kuna mahali ambako bomba hili limepita katika eneo lenye mto na kuna maji mengi, lilikuwa limepasuka hivyo hatua zimechukuliwa na bado tunaendelea kufanya kazi ya ufuatiliaji”, alisema.  

Hata hivyo maeneo mengi ya mji huo kwa sasa yanakosa huduma ya maji safi ambapo maji yanayozalishwa ni kidogo, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuchukuliwa ili wakazi wa mji wa Mbinga waweze kuondokana na kero hiyo.



No comments: