Saturday, May 24, 2014

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA YAZITAKA HALMASHAURI ZA WILAYA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE IPASAVYO

Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano na TFDA katika ukumbi wa hospitali ya mkoa wa Mbeya.

 Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Charys Ugullum,(aliyesimama) akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari Jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Baadhi ya Waandishi wa habari na Wahariri wa Nyanda za juu Kusini, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA). (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbeya.

HALMASHAURI za wilaya hapa nchini kupitia kamati zake za udhibiti wa ubora wa chakula na dawa, zimetakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kulinda afya za wananchi.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA) Charys Ugullum alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa siku moja, Wahariri na Waandishi wa habari wa mikoa ya Nyanda za juu Kusini Jijini Mbeya.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Hospitali ya mkoa huo, ambapo ulilenga kuwaelimisha Wahariri na Waandishi wa habari  namna ya kuibua matatizo ya bidhaa feki ambazo huuzwa maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo la kuleta ufanisi na ubora wa chakula na dawa.


“Niwaombe ndugu zangu kwa kutumia wadau kama ninyi tutaweza kudhibiti ubora wa dawa zetu, fanyeni uchunguzi maduka mengi yamekuwa yakiuza bidhaa ambazo hazijasajiliwa na ni hatari kwa afya zetu”, alisema Ugullum.

Naye Mkurugenzi wa kitengo cha uendeshaji huduma kutoka TFDA udhibiti wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba Chrispin Severe alisema kumekuwa na tatizo la wafanyabiashara wengi, ambao sio waaminifu wamekuwa wakiuza bidhaa hizo ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Alisema Mamlaka hiyo itaendelea kuteketeza kila bidhaa ambayo itaona haifai kwa matumizi ya binadamu, ambapo alieleza kuwa tatizo la bidhaa duni na bandia Nyanda za juu kusini limekuwa kubwa.

“Tutaendelea kuteketeza na kuchukua hatua za kisheria pale tunapobaini sehemu fulani kuna tatizo, na ndio maana leo tumeamua kuwashirikisha waandishi wa habari ili muweze kutoa matangazo juu ya mambo haya”, alisema.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo ambao ulikuwa wa siku moja, TFDA ilikutana na Wahariri na Waandishi wa habari wa Nyanda za juu kusini kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Katavi.






No comments: