Thursday, May 8, 2014

ASKOFU ALIA NA WANASIASA AWASIHI WATIMIZE MAJUKUMU YA WANANCHI KWANZA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma John Ndimbo, amewataka Madiwani wa wilaya ya Mbinga mkoani humo kuacha itikadi za kisiasa pale wanapotekeleza mambo ya msingi ya wananchi, na endapo wasipozingatia hilo huenda wakasababisha machafuko katika jamii.

“Mwanasiasa yeyote ambaye hana kanuni na hazingatii mambo ya msingi huyo anaipoteza jamii, tuache itikadi za kisiasa tutekeleze kwanza majukumu tuliyopewa na wananchi”, alisema Ndimbo.

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu huyo katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi hivi karibuni, kwenye ukumbi wa jimbo katoliki la Mbinga ambacho kilikuwa kikiendeshwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga.


Ndimbo alisema lengo la kikao hicho ni kutaka kuboresha masuala ya elimu wilayani Mbinga, hivyo wanasiasa na watendaji husika katika sekta mbalimbali wilayani humo, hawana budi kujenga ushirikiano ili kumpiga vita adui ujinga ambaye bila elimu hakuna maendeleo.

“Nawasihi katika elimu tusifanye siasa, popote pale penye mafanikio ni lazima pawepo na jitihada ambayo inafanyika”, alisisitiza.

Aidha alieleza kuwa wanasiasa kuendelea kupigana vijembe majukwaani au katika vikao mbalimbali, wadau wa elimu wanavunjika moyo badala yake kila mtu atimize wajibu wake na sio kuingiliana katika majukumu ya kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Ngaga, alisema wilaya hiyo imejiwekea mikakati kabambe kwamba suala la elimu linapewa kipaumbele kwanza katika kuhakikisha mambo ya msingi yanatekelezwa ipasavyo, kwa kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments: